1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaibinya Urusi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran

18 Septemba 2009

Kimegeuka kile kisa cha nipe nikupe. Marekani sasa inaishinikiza Urusi iache kuwauzia Iran makombora na pia iunge mkono azimio kali la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

https://p.dw.com/p/JjOt
Rais Barack Obama akizungumza kuhusu makombora ya kujihami nchini Poland and Jamhuri ya ChekiPicha: AP

Hii ni baada ya Rais Barack Obama kuufutilia mbali mpango wa Marekani kujenga mfumo wa kujihami dhidi ya makombora huko Ulaya ya Mashariki, mpango uliokuwa na mvutano kati ya Urusi na Marekani.

Waswahili walisema mkono mtupi haurambwi- baada ya Marekani kuunyoshea mkono Urusi kwa kusitisha ujenzi wa mfumo wa kujihami dhidi ya makombora uliokuwa ujengwe nchini Poland na katika Jamhuri ya Cheki, sasa ni zamu ya Moscow kurejesha fadhila.

Kulingana na afisa mmoja wa ngazi juu katika wizara ya mambo ya nchi za nje wa Urusi- Marekani sasa inataka fadhila mbili kutoka Urusi na zote zinahusiana na Iran. Kwanza Marekani inataka Urusi iache kuwauzia Iran makombora na pili Urusi iunge mkono azimio la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Urusi ambaye ni mwanachama wa kudumu na mwenye kura ya turufu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imekuwa ikipinga swala la Iran kuwekewa vikwazo.

Kuna ripoti kwamba Urusi na Iran zilitia saini mkataba kuwa Moscow iipe Tehran makombora watakaoweza kuzuia mashambulizi yeyote ya makombora mwaka wa 2005, lakini bado Urusi haijawasilisha mzigo huo kwa Iran. Ni mkataba huu ndio unawatia joto nchi za Magharibi ikiwemo Marekani wanauona kwamba utaboresha zaidi kinga ya Iran. Nchini Urusi magazeti nchini humo yameusifu uamuzi huo wa Rais Obama wakisema utachangia zaidi kuboresha uhusiano kati ya Marekani na Urusi- kwani mpango huo ndio ulikuwa kiini cha mvutano kati ya nchi hizo mbili tangu ulipoanzishwa na Rais George Bush. Rais wa Urusi Dimitry Medveded alikuwa mwingi wa pongezi kwa hatua ya Marekani.

Poland na Jamhuri ya Cheki ambao walikuwa wanautegemea mpango huo wa Marekani kama kinga kwao, wametoa wasiwasi wao. Waziri mkuu wa Poland Donald Tusk anasema la muhimu sasa ni usalama Poland

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Cheki Jan Fischer alisema ana imani hatua hii haitobadili ushirikiano kati ya Marekani na nchi yake.

Akitangaza hatua ya kuusimamisha mradi huo wa rais Obama alisema Marekani itaanzisha mradi mpya ambao utakabiliana vilivyo na vitisho vya makombora ya masafa marefu kutoka nchini Iran. Wakati huo huo Rais Mahmoud Ahmedinejad amenukuliwa na kituo kimoja cha Televisheni cha Marekani NBC akisema nchi yake haitolegeza kamba katika ari yake ya kuwa na mradi wa nyuklia.

Mwandishi : Munira Muhammad/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman.