1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaimarisha ulinzi wa makombora

4 Aprili 2013

Marekani kuimarisha ulinzi wake wa makombora huko Pasifiki kwa kujiandaa kutuma mitambo ya kujikinga na makombora huko Guam baada ya Korea Kaskazini kuidhinisha mipango ya mashambulizi ya nuklea dhidi ya Marekani.

https://p.dw.com/p/189W3
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck HagelPicha: REUTERS

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema kuongezeka kwa vitisho vya shari vya serikali ya Korea Kaskazini kukichanganishwa na uwezo wao wa kijeshi kunatowa tishio la kweli na la wazi kwa Marekani na washirika wake Korea Kusini na Japani.Hagel amesema wana uwezo wa silaha za nuklea hivi sasa wana uwezo wa kurusha makombora hivi sasa na wanavichukilia vitisho hivyo kwa makini.Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema itatuma mizinga ya kujikinga na makombora ardhini kuzihami kambi zake zilioko Guam ambalo ni eneo la ardhi ya Marekani lilioko kama kilomita 3,380 kusini mashariki mwa Korea Kaskazini na ni makaazi ya wanajeshi elfu sita wa Marekani vikiwemo vikosi vya wanamaji na mizinga.

Mizinga kusaidiwa na meli za kivita

Mizinga hiyo ya kujikinga na makombora itasaidiana na meli mbili za kivita za kudukiza makombora ambazo tayari zimetumwa katika eneo hilo.Muda mfupi baada ya kutolewa kwa tangazo hilo la kutumwa kwa mizinga ya kujkinga na makombora jeshi la Korea Kaskazini limesema limepata idhini ya mwisho ya kuchukuwa hatua ya kijeshi dhidi ya Marekani ambayo inaweza kuhusisha silaha za nuklea.Generali wa Jeshi la Wananchi wa Korea Kaskazini amesema kwamba wakati wa mripuko umekuwa unakaribia kwa haraka kujibu kile ilichokiita uchokozi wa Marekani wa kutumia ndege za kivita chapa B-52 na B-2 zenye uwezo wa kubeba mabomu ya nuklea wakati wa mazoezi ya kijeshi ya pamoja yanayoendelea na Korea Kusini.

Ndege ya kivita ya Marekani chapa B-2 yenye uwezo wa kubeba mabomu ya nuklea.
Ndege ya kivita ya Marekani chapa B-2 yenye uwezo wa kubeba mabomu ya nuklea.Picha: picture-alliance/dpa

Korea Kaskazini yahamisha makombora

Wakati vitisho vichache vya Korea Kaskazini vimetekelezwa kwa vitendo repoti zinasema kwamba inaonekana nchi hiyo hapo Jumatano (03.04.2013) imehamisha makombora yake ya masafa ya kati yenye uwezo wa kupiga Korea Kusini na Japani katika mwambao wake wa mashariki. Korea Kaskazini Alhamisi (04.04.2013) imeendelea kufunga njia za kuingia kwenye eneo la viwanda la pamoja na Korea Kusini kwa siku ya pili mfululizo na kutishia kuwaondowa wafanyakazi wake 53,000 kutokana na kukasirishwa na tangazo la Korea Kusini la mpango wa kijeshi wa kuwalinda wafanyakazi wake walioko katika eneo hilo.Korea Kaskazini imesema Wakorea Kusini 800 ambao hivi sasa wako huko Kaesong kilomita 10 ndani ya mpaka wa Korea Kaskazini wanaweza kuondoka wakati wowote ule wanaotaka lakini wengi wao wameamuwa kubakia kuvifanya viwanda hivyo viendelee kufanya kazi.

Jeshi la Korea Kaskazini likiwa tayari limejiandaa kwa vita.
Jeshi la Korea Kaskazini likiwa tayari limejiandaa kwa vita.Picha: picture-alliance/dpa

Mzozo kuishia wapi ?

Yun Duk -Min profesa katika Chuo cha Taifa cha Korea chaTaaluma ya Kidplomasia mjini Seol anasema tatizo ni iwapo Kim Jong -Un kiongozi wa Korea Kaskazini ambaye bado ni kijana na hana uzoefu anajuwa jinsi ya kushughulikia hali hii ya kupamba moto kwa mvutano huo.Unaishia wapi ?Hilo ndio suala la kutia mashaka!

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un.Picha: Reuters

Mwandishi: Mohamed Dahmam/AFP

Mhariri: Josephat Charo