1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka China inunue bidhaa zake kwa wingi

Zainab Aziz
2 Juni 2018

Waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross amewasili mjini Beijing, China katika ziara yenye lengo la kufanikisha kupata makubaliano kwa China kuweza kununua bidhaa zaidi za Marekani pamoja na nishati.

https://p.dw.com/p/2yqWg
USA China US-Handelsminister Wilbur Ross zu Besuch in Peking
Picha: Reuters/T. Peter

lakini baada ya kuonekana kwamba kuna uwezekano wa kupatikana suluhu kati ya nchi hizo mbili zenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani, Marekani hata hivyo imeonya kwamba itaendelea kutekeleza azma yake ya kuwekea China ushuru zaidi wa dola bilioni 50 za thamani ya uagizaji kutoka nchini humo pamoja na kuweka vikwazo dhidi shughuli za uwekezaji za China nchini Marekani na pia kuweka udhibiti mkali na kufuatilia shughuli za kusafirisha bidhaa nje.

Ross, ambaye ameandamana na maafisa zaidi ya 50, anatarajiwa wakati wa ziara yake ya siku mbili kujaribu kupata hakikisho la China juu ya ununuzi wa muda mrefu wa bidhaa za Marekani ya kilimo na nishati ili kusaidia kupunguza tofauti ya mapato ya biashara ya jumla ya kiasi cha dola Bilioni 375 liyopo kati ya China na Marekani. Rais Donald Trump ameitaka China ichukue hatua ya kupunguza pengo hilo kwa kiasi cha dola bilioni 200 kila mwaka hadi kufikia mwaka 2020.

Rais wa Marekani Donald Trump, nyuma yake kushoto ni bi Maryllyn Hewson mkurugenzi mtendaji wa Lockheed Martin katikati nyuma ni waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross na mwakilishi wa biashara wa Marekani Robert Lighthizer
Rais wa Marekani Donald Trump, nyuma yake kushoto ni bi Maryllyn Hewson mkurugenzi mtendaji wa Lockheed Martin katikati nyuma ni waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross na mwakilishi wa biashara wa Marekani Robert LighthizerPicha: Reuters/J. Ernst

Ujumbe huo wa Marekani pia unataka kuhakikisha kuwa Marekani inapata ulinzi zaidi wa mali na China isitishe mfumo wake wa ruzuku ambao Marekani inaonelea kuwa ndio unachangia uzalishaji zaidi wa bidhaa za chuma na bati.

Wakati nchi nyingi zinakubaliana kuchanganyikiwa kwa Marekani kutokana na shughuli za kibishara na uchumi za China, wakosoaji wa sera za Marekani chini ya rais Trump hata hivyo wameonya kwamba Marekani iko katika hatari ya kujitenga na washirika wake wa nchi za Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico kutokana na kuanzisha ushuru zaidi wa asilimia 25 kwa bidhaa za bati na silimia 10 zaidi kwa bidhaa za chuma.

Umoja wa Ulaya hapo jana ulianzisha mipango ya kukabiliana na kitendo cha Marekani cha kuongeza kodi za bidhaa za chuma na bati kutoka nchi wanachama wa umoja huo huku Marekani ikianza mikutano nchini Canada na mawaziri wa fedha wa nchi zilizoathirika na nyongeza hiyo ya kodi.

Rais wa tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker
Rais wa tume ya Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Getty Images/AFP/J. Thys

Trump amesema kuna uwezekano wa kufutilia mbali makubaliano ya biashara huru kati ya Marekani na nchi za Amerika Kaskazini ambayo yamedumu kwa miaka 24 na badala yake kupendelea kuwa na makubaliano kati yake na Canada au Mexico.

Umoja wa Ulaya na Canada zimewasilisha kesi kupinga uamuzi wa Marekani wa kuongeza kodi katika shirika la biashara duniani WTO.

Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico pia zimetishia kuongeza kodi dhidi ya bidhaa za Marekani. Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema ameshangazwa na hatua hiyo ya Marekani huku Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May akisema amevunjwa moyo na uamuzi wa Marekani.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz amesema nyongeza hiyo ya kodi haikubaliki na kwamba vita hivi vya kibiashara vinaweza kusababisha hasara kubwa kwenye sekta zote.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE
Mhariri: Caro Robi