1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Urusi kutuliza hali Ukraine

5 Desemba 2014

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry amesema Urusi inaweza kujenga upya mahusiano yake na nchi za Magharibi kama “itasaidia tu kutuliza hali” katika mpaka wake na Ukraine

https://p.dw.com/p/1DzZh
OSZE Außenminister Konferenz 04.12.2014 Basel
Picha: AFP/Getty Images/S. Bozon

Ukraine na waasi wanaoiunga mkono Urusi wamesema wamekubaliana kusitisha mapigano mnamo Desemba tisa chini ya masharti ya muafaka unaolenga kumaliza mojawapo ya migogoro mikubwa ya uwamgaji damu kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya katika miongo mingi. Tangazo hilo ambalo halikutarajiwa limetoa matumaini ya kufikia kikomo mapigano mashariki mwa Ukraine ambayo yamedumu kwa zaidi ya miezi minane na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 4,300, na kuvuruga uhusiano wa Urusi na nchi za Magharibi.

Kerry mit Lawrow OSZE Außenminister Konferenz 04.12.2014 Basel
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters/F. Coffrini

Akizungumza mjini Basel, Uswisi, katika mkutano wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani UIaya - OSCE, Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Mmarekani John Kerry ametoa wito kwa Urusi kuuheshimu muafaka wa awali wa kusitisha mapigano, ambao unatoa wito wa kuwacha kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigana mashariki mwa Ukraine, na kuwashawishi wawaachienhuru mateka. Marekani na Umoja wa Ulaya zimewawekea vikwazo Warusi kadhaa na wanaharakati kama adhabu kutokana na vitendo vyao. Kerry alikutana kwa muda mfupi katika vikao tofauti na Mawaziri wa mambo ya Nchi za Kigeni wa Ukraine Pavlo Klimkin, Sergei Lavrov wa Urusi na Tamar Beruchashvili wa Georgia. Marekani na Urusi ni washirika wa OSCE.

Lakini katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, Rais Vladmir Putin amezishutumu nchi za Magharibi kwa kuutumia mgogoro wa Ukraine katika kuidhoofisha serikali ya Urusi. Putin ameutetea uamuzi wa Urusi kuifanya Rasi ya Crimea kuwa sehemu ya himaya yake, akilitaja jimbo hilo kuwa takatifu kwa Urusi.

Putin Rede an die Nation 04.12.2014
Rais wa Urusi Valdmir Putin akilihutubia taifaPicha: picture-alliance/dpa/Sergei Ilnitsky

Putin autetea msimamo wa Urusi kuhusu Ukraine

Putin aliutetea msimamo wa Urusi kuhusiana na suala la Ukraine, lakini akasema serikali yake haitaharibu mahusiano yake na nchi za Magharibi licha ya kuwepo malumbano na Umoja wa Ulaya na Marekani. Amepuuzilia mbali masaibu ya nchi hiyo wakati uchumi ukiendelea kuporomoka kutokana na vikwazo vya nchi za magharibi pamoja na kupungua bei za mafuta.

Kwingineko, kamanda mmoja wa ngazi ya juu wa waasi mashariki mwa Ukraine amekiri kuwa waasi wamefanya mashambulizi ya makombora dhidi ya wanajeshi wa serikali kutoka maeneo ya makaazi lakini akasema kuwa wanasitisha vitendo hivyo.

Idadi kubwa ya makaazi katika mji wa mashariki wa Donetsk, ambao ni ngome ya waasi, yameshambuliwa na makombora yanayoaminika kufyatuliwa na majeshi ya serikali yanayopambana na waasi wanaoiunga mkono Urusi.

Kando na hayo, waangalizi wa kimataifa wamesema kuwa majeshi ya Ukraine na waas wanaopigania kujitenga katika eneo jirani la Luhansk wamekubaliana kuhusu mpango mpya wa kusitisha mapigano kuanzia leo. Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden amemwambia Rais wa Ukraine Petro Poroshenko kwa njia ya simu kuwa Marekani na Ulaya itaendelea kutoa msaada wa kifedha ili kuisaidia Ukraine kuimarisha uchumi wake.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri. Josephat Charo