1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajiondoa kutoka baraza la haki za binadamu

Caro Robi
20 Juni 2018

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema Marekani imejiondoa katika baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu akiishutumu asasi hiyo kwa kuwalinda wanaofanya maovu, unafiki na kuionea Israel.

https://p.dw.com/p/2ztBw
USA Washington Ankündigung Austritt aus UN-Menschenrechtsrat | Nikki Haley
Picha: Reuters/T.S. Jordan

Haley na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo wamelishutumu baraza hilo la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kwa muda mrefu kuwalinda wanaokiuka haki za binadamu na kuwa na mapendeleo kuhusu masuala ya kisiasa.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema hatua hiyo ya Marekani inaweza kuhujumu wajibu na hadhi ya nchi hiyo kimataifa ya kuwa mtetezi wa demokrasia.

Marekani yazidi kujitenga na jumuiya ya kimataifa

Hatua hiyo ndiyo ya hivi punde kuchukuliwa na utawala wa Rais Donald Trump kujiondoa katika mikataba ya kimataifa ikiwemo kujiondoa kwenye makubaliano kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran, makubaliano ya kuyalinda mazingira yaliyofikiwa Paris na mikataba kadhaa ya kibiashara.

USA Präsident Donald Trump in Washington
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Mashirika 12 ya kutetea haki za binadamu na ya kutoa misaada yameonya kuwa hatua ambayo Marekani imechukua itafanya kampeni za kuteteta haki za binadamu duniani kuwa hata ngumu zaidi.

Haley amezishutumu Urusi, China, Cuba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Misri ambao ni wanachama wa baraza hilo kwa kuhujumu juhudi za Marekani kulifanyia mageuzi baraza hilo la kutetea haki za binadamu.

Miongoni mwa mageuzi Marekani imekuwa ikitaka ni kuwa rahisi kuwaondoa nchi wanachama walio na rekodi mbovu ya haki za binadamu. Jinsi hali ilivyo hivi sasa, ili kumuondoa mwanachama, thuluthi mbili ya nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kuidhinisha kura ya kuiondoa.

Hayo yanakuja huku Marekani ikikosolewa vikali kutokana na kuwatenganisha watoto na wazazi wao wahamiaji katika mpaka kati ya Marekani na Mexico. Kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Zeid Ra'ad al Hussein ameitaka Marekani kusitisha sera zake katili.

Haley pia amesema Israel imekuwa ikimulikwa sana na imeshuhudia uhasama usiokwisha, thibitisho la wazi kuwa baraza hilo linachochewa na maslahi ya kisiasa na wala sio kusimamia haki za binadamu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaikosoa Marekani

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameupongeza uamuzi huo wa Marekani. Marekani imekuwa ikiikingia kifua Israel katika Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu.

Grenze USA-Mexiko | Zentralamerikanische Asylsuchende - Mutter mit Kind aus Honduras
Utawala wa Trump umekuwa ukizitenga familia za wahamiajiPicha: Getty Images/J. Moore

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameushutumu utawala wa Trump kwa kutolipa kipaumbele suala la haki za binadamu katika sera zake za kigeni.

Wakosoaji wa utawala huo wanasema hii inatuma ujumbe kuwa utawala huo unayafumbia macho maovu yanayokiuka haki za binadamu kwingineko duniani.

Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa Marekani kususia baraza hilo la kutetea haki za binadamu. Lilipoundwa mwaka 2006, Rais George W. Bush alilisusia.

Marekani ilijiunga nalo wakati wa utawala wa Rais Barack Obama. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema Marekani ndiyo inakuwa nchi ya kwanza kujiondoa kutoka baraza hilo lenye wanachama 47 lenye makao yake mjini Geneva.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel