1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajiondoa kwenye mkataba wa TPP

Bruce Amani
24 Januari 2017

Mataifa kadhaa yameelezea matumaini kuwa mkataba wa biashara katika ukanda wa Pasifik utadumishwa, baada ya uamuzi wa Rais Donald Trump kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo kuuweka mustakabali wake katika hatari kubwa

https://p.dw.com/p/2WIAs
Barack Obama Handelsabkommen TPP
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Walsh

Waziri Mkuu wa Australia Malcom Turnbull amekiri kuwa hatua ya Trump ni pigo kubwa kwa makubaliano hayo yanayoyahusisha mataifa 12, lakini akadokeza kuwa nchi nyingine, kama vile China, huenda zikasaidia kujaza pengo lililoachwa na Marekani. Lakini hata hivyo ameelezea matumaini kuwa Marekani huenda ikabadilisha hatua hiyo "tutambue kuwa waziri wake wa mambo ya nje Rex Tillerson kwa muda mrefu amekuwa mpiganiaji wa mkataba huo. Wajumbe wa chama cha Republican katika Baraza la Congress wamekuwa wakiunga mkono mpango wa TPP hivyo kuna uwezekano kuwa sera ya Marekani huenda ikabadilika baadaye kuhusu hilo kama ilivyotokea kwa mikataba mingine ya biashara".

Turnbull amesema hivi karibuni aliujadili mustakabali wa mkataba huo na mawaziri wakuu wa Japan, Singapore na New Zealand, ambazo zote ni wanachama wa TPP, na anaamini muafaka huo utadumu bila ya Marekani. Wanachama wengine wa TPP ni Canada, Mexico, Chile, Peru, Vietnam, Malaysia na Brunei.

Australien Abe und Turnbull in Sydney
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenzake wa Australia Malcolm TurnbullPicha: Reuters/B. Mitchell

Kama ilivyotarajiwa, Trump alitumia mojawapo ya hatua zake za kwanza madarakani kuufuta rasmi mkataba huo wa biashara, akisema kuwa una madhara kwa kampuni za Marekani. Anapendelea makubaliano baina ya nchi na nchi badala ya mikataba ya kundi la nchi nyingi.

Viongozi wa baadhi ya mataifa mengine 11 yanayohusika na mkataba huo awali walisema kuwa watasonga mbele na makubaliano hayo katika muundo mwingine iwepo au isiwepo Marekani. Hatua ya Marekani kujiondoa kwenye ushirikiano huo ni pigo kwa viongozi wa mataifa mengine ya TPP ambao waliwekeza mtaji mkubwa wa kisiasa katika kuupigania mpango huo kuidhinishwa.

Miongoni mwao ni Waziri Mkuu Shinzo Abe, ambaye amewaambia wabunge wakati wa kikao cha bunge kuwa anatumai  kuupata uelewa wa Trump kuhusu umuhimu wa TPP. Abe amesema anatumai kukutana na Trump haraka iwezekanavyo. Japan ilikamilisha wiki iliyopita mchakato wa kuuidhinisha mkataba huo, ikifahamu kuwa Trump alipanga kujiondoa. Abe amesema malengo ya muafaka huo bado ni muhimu kwa Japan na TPP huenda ikawa mfano wa mikataba ya biashara na mataifa mengine, yakiwemo ya Ulaya.

Turnbull amesema kinadharia, China inaweza kujiunga na mkataba huo kufuatia kujiondoa kwa Marekani. Lakini hilo litahitaji marekebisho makubwa kwa makubaliano hayo. Katika muundo wa sasa, TPP inaweza tu kutekelezwa baada ya kuridhiwa na nchi sita ambazo zinajumuisha asilimia 85 ya pato jumla la pamoja la nchi zote wanachama. Marekani ilijumuisha asilimia 60 ya pato jumla la pamoja la TPP, hivyo haungeweza kutekelezwa kama ulivyo sasa.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Caro Robi