1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajitayarisha tena na kimbunga Nate

Sekione Kitojo
7 Oktoba 2017

Kimbunga Nate kimepata nguvu zaidi  wakati kinaelekea katika rasi ya Yukatan nchini Mexico baada ya kusababisha mvua kubwa  katika eneo la Amerika ya kati na kusababisha vifo vya karibu watu 21.

https://p.dw.com/p/2lPdY
Puerto Rico Hurrikan Maria
Picha: Getty Images/AFP/R. Arduengo

Watabiri  wa  hali  ya  hewa  wamesema  upepo  huo mkali  na  mvua  huenda  ukafika  katika  pwani  ya ghuba  ya  Marekani  kama  kimbunga  mwishoni  mwa juma.

Maafisa  wa  Louisiana na  Mississippe  wametangaza  hali ya  hatari  na  Louisiana  wameamru  baadhi  ya  watu waondolewe  katika  maeneo  ya  pwani na  visiwa  vya vizuwizi  kabla  ya  kutarajiwa  kuwasili  kwa  kimbunga hicho  leo  Jumamosi  usiku  ama  mapema  Jumapili. Uondoaji  wa  watu  ulianza  katika  maeneo  ya  nje baharini  katika  maeneo  yanayochimbwa  mafuta  katika eneo  hilo  la  ghuba.

Puerto Rico Hurrikan Maria
Upepo mkali na mvua nyingi huambatana na vimbungaPicha: Getty Images/AFP/R. Arduengo

Serikali  ya  jimbo la  Mississippi  imesema  itafungua vituo  11 vya  kuhifadhi  watu katika  maeneo  nje  ya eneo  la  karibu  la  pwani, ambapo  mabasi yametayarishwa  kwa  ajili  ya  watu  ambao  hawana magari.

Kituo  kinachohusika  na  masuala  ya  vimbunga  nchini Marekani  kimeonya  kwamba  kimbunga  Nate kinaweza kupandisha  viwango  vya  bahari  kwa  zaidi  ya  futi  nne hadi saba , mita  1.2 hadi  mita 2.1  , kutoka  mji  wa Morgab, Louisiana , hadi  mpaka  kati  ya  Alabama  na florida. Kimbunga  hicho  tayari  kimesababisha  mafuriko makubwa  katika  eneo  kubwa  la  Amerika  ya  kati.

Kituo  hicho  kimeongeza  mji wa  New Orleans  na  ziwa Pontchartrain katika  orodha  ya hivi  karibuni  kabisa  ya tahadhari  kwa  kimbunga  hicho.

Dominikanische Republik Hurrikan Maria
Mvua kubwa na upepo , wanawake hawa wanatembea katika mvua na upepo mkali kabla ya kuwasili kimbunga Maria katika Jamhuri ya DominikaPicha: Reuters/R. Rojas

Kimbunga kinaongezeka  nguvu  na  kasi

Kimbunga  hicho  ambacho  kina  wastani  wa  upepo unaokwenda  kasi  ya  kilometa  65  kwa  saa  ilipofika jana  Ijumaa  mchana  na  huenda  kikaongezeka  nguvu wakati  kikiwa  katika  eneo  la  bahari  la  kaskazini magharibi la   visiwa  vya  Karibiki  kabla  ya  kuingia katika  eneo la  Cancun  mwishoni  mwa  rasi  ya  Yucatan nchini  Mexico. Inaweza  kulikumba  eneo  la  ghuba  ya pwani  ya  Marekani  karibu  na  New Orleans.

Kimbunga  hicho  kilionekana  kiasi  ya  kilometa  145 kaskazini  mashariki  mwa  mji  wa  kitalii  nchini  Mexico wa  Cozumel  na  kuongeza  kasi  kuelekea  upande  wa kaskazini  na  kaskazini  magharibi hadi  kilometa  35  kwa saa. Maafisa  walifuta  masomo kwa  wanafunzi  siku  ya Ijumaa  mchana  katika  maeneo ya  jimbo  la  pwani  ya Karibiki katika  jimbo  la  Quintana Roo,  ambako  Cozumel na Cancun  zinapatikana.

Dominica Hurrikan Maria
Nyumba ikiwa imeharibiwa kabisa na kimbunga katika kisiwa cha Saint-MartinPicha: Getty Images/AFP/H. Valenzuela

Gavana  Carlos  Joaquin  amesema  inaonekana  kwamba kimbunga  hicho  kitabakia  nje  ya  pwani  na hakitashambulia  eneo  la  ndani , na  kuongeza , kwamba , "naamini , ni  habari  nzuri."

Shule zilifungwa Nicaragua

Nchini  Nicaragua , kuwasili  kwa  kimbunga  Nate kunafuatia  wiki  mbili  za  mvua  ambayo  ilikuwa inanyesha  karibu  wakati  wote  ambayo  imeacha  ardhi ikiwa  na  maji  mengi  na  mito  kujaa  maji. Maafisa wameiweka  nchi  yote  katika  hali  ya  tahadhari na kuonya  kwamba  mafuriko  na  maporomoko  ya  ardhi huenda  yakatokea.

Puerto Rico Hurrikan Maria
Picha ya satalaiti ya kimbunga kinachovuma na upepoPicha: Reuters/NASA

Makamu  wa  rais  wa  Nicaragua  na  msemaji  wake, Rosario Murillo, wamesema  kwamba  kiasi  watu 11 wamefariki  nchini  humo  kutokana  na  kimbunga  hicho. Mapema  siku  ya  Alhamis  alisema  watu  15  wamefariki kabla  na  baadaye  kubadilisha  na  kusema  baadhi  yao wanahesabiwa  kwamba  hawajulikani  waliko.

Hakutoa  maeneo  zaidi  kuhusu  vifo  vyote, lakini amesema  wanawake  wawili  na  mwanamume  mmoja ambaye  alikuwa  akifanya kazi  katika  wizara  ya  afya walichukuliwa  na  mafuriko  katika  mrefeji  uliojaa  maji katika  mji  wa  kati  wa  Juagalpa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Lilian Mtono