1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamnyonga Davis licha ya shinikizo la kimataifa

22 Septemba 2011

Licha ya shinikizo la kimataifa kupinga hukumu ya kifo dhidi ya Troy Davis, jimbo la Georgia nchini Marekani limemnyonga kijana huyo na kuzusha shutuma kubwa kutoka ulimwengu na wanaharakati wa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/12eS5
Troy Anthony Davis katika uhai wake.
Troy Anthony Davis katika uhai wake.Picha: AP

Saa 5:00 usiku kwa saa za Marekani, Davis alipigwa sindano ya sumu na akafariki dakika nane baadaye. Dakika hizi za mwisho za Davis hazikuwa ngumu kwake tu, bali kwa waungaji mkono wake wengi waliokuwa wamepigania kwa siku kadhaa kusitishwa kwa adhabu hii.

Mwandishi wa habari, John Lewis, ambaye ameshuhudia Davis akinyongwa, amesema kuwa kuwa kijana huyu, Mmarekani mwenye asili ya Afrika, amekufa huku akishikilia msimamo wake wa kukataa kuhusika na mauaji ya Mark MacPhail, hapo mwaka 1984.

"Kimsingi, Davis amefariki kwa utulivu kabisa. Familia ya MacPhail na marafiki walikaa kwenye safu ya mbele wakiangalia. Msimamizi wa magereza alisoma amri ya kunyongwa, akimuuliza Davis kama alikuwa na chochote cha kusema, na Davis akanyanyua kichwa na kuangalia safu ya mbele na akatoa kauli kwamba alitaka kuzungumza na familia ya MacPhail. Akasema kwamba licha ya hisia waliyonayo familia hiyo, yeye siye aliyemuua mtu wao. Kwamba yeye binafsi hakuhusika na kilichotokea usiku ule MacPhail alipouawa, na kwamba yeye hakuwa na bastola. Aliiambia familia hiyo kuwa anasikitishwa na kumpoteza mpendwa wao, lakini si yeye aliyechukuwa maisha ya mtoto, baba na kaka yao." Amesema Lewis.

Hukumu hii ilikuwa kwanza itekelezwe saa 1:00 magharibi kwa saa za Marekani, lakini ikaakhirishwa wakati Mahakama Kuu ilipokuwa ikipitia rufaani ya mwisho iliyowasilishwa na mawakili wa Davis. Hata hivyo, baadaye Mahakama hiyo iliikataa rufaani hiyo.

Waungaji mkono wa marufuku ya adhabu ya kifo wakifarijiana baada ya Davis kunyongwa.
Waungaji mkono wa marufuku ya adhabu ya kifo wakifarijiana baada ya Davis kunyongwa.Picha: AP

Kwa zaidi ya mara tatu, hukumu hii ilikuwa imecheleweshwa kutokana na hoja za mawakili kwamba saba kati ya mashahidi tisa dhidi ya Davis, aidha walijikanganya au walipotosha ushahidi wao.

Mapema hapo jana, wakati Mahakama Kuu ilipokuwa haijafanya maamuzi, mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya gereza kwenye mji wa Jackson, jimbo la Georgia, wakipiga mayowe ya kutaka maisha ya Davis yanusuriwe. Waandamanaji pia walikusanyika nje ya Ikulu ya Marekani, jijini Washington, wakiwa na ujumbe huo huo.

Taarifa za kucheleweshwa zilipowafikia, walirukaruka kwa furaha lakini furaha hii haikudumu baada ya kufahamika kuwa Davis angelinyongwa usiku wa jana.

Msemaji wa Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International, Laura Moye, amesema kwamba hukumu hii inafadhaisha sana.

"Tumepigwa na bumbuwazi. Tumefadhaishwa na tumekasirishwa sana kwamba serikali ya jimbo la Georgia imemnyonga Troy Davis licha ya kuwepo ushahidi wa kutosha unaotilia shaka kesi dhidi yake. Hatuwezi kuwa na uhakika ikiwa mtu asiye na makosa ameuliwa usiku wa jana na serikali ya Georgia imefanya uonevu mkubwa ambao umepuuza uungaji mkono wetu dhidi ya adhabu ya kifo Marekani." Amesema Moye.

Amnesty International inasema baadhi ya mashahidi waliotoa ushahidi dhidi ya Davis walitumiliwa nguvu na polisi.

Kesi hii ya Davis ilizoa umashuhuri mkubwa duniani, ambapo maandamano kadhaa ya kupinga hukumu ya kifo dhidi yake yalifanyika. Hapo jana Ufaransa ilitoa ombi la msamaha kwa Davis, ikisema kuwa kunyongwa kwake kungelikuwa kosa lisilorekebishika.

Ombi la Ufaransa lilitanguliwa na maombi kama hayo kutoka kwa watu maarufu duniani, kama vile mkuu wa kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Benedict wa 16, rais wa zamani Marekani, Jimmy Carter na Askofu Desmond Tutu wa Afrika ya Kusini.

Karibuni watu milioni moja duniani walisaini hati ya kutaka kuzuiwa kwa hukumu hii.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman