1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yampongeza Mursi

Admin.WagnerD25 Juni 2012

Rais wa Marekani Barack Obama amempongeza rais mpya wa Misri Mohammed Mursi huku magazeti makubwa ya nchi hiyo yakisema ushindi wake ni hatua muhimu kuelekea demokrasia ya kweli.

https://p.dw.com/p/15KvC
Rais mpya wa Misri, Mohammed Mursi.
Rais mpya wa Misri, Mohammed Mursi.Picha: AP

Rais Obama alimpigia simu rais Mursi jsiku ya Jumapili na kumuahidi ushirikiano wa Marekani katika kuhakikisha nchi hiyo inaendeleza demkorasia na kusisitiza nia yake ya kufanya kazi pamoja na rais huyo mpya wa Misri katika misingi ya kuheshimiana na kuendeleza yale yote ya manufaa kwa mataifa haya mawili.

Obama pia alimpigia mgombea aliyepoteza, Ahmed Shafique na kumhimiza kuendelea kutoa mchango kwa kushikiriana na rais mpya kuwaunganisha raia wa misri. Habari zinasema Shafique amekubali kushindwa na amepongeza rais mpya na kuahidi kushirikiana naye.

Rais wa Marekani Barack Obama amesema yuko tayari kushirikiana na Mursi.
Rais wa Marekani Barack Obama amesema yuko tayari kushirikiana na Mursi.Picha: AP

Kumekuwepo na maoni tofauti miongoni mwa raia wa misri na pia ya kimataifa kuhusiana na ushindi wa Mohammed Mursi. Rana Gaber ni miongoni mwa waandamanaji walikokuwa katika viwanja vya Tahrir wakati matokeo yakitangazwa: "Nina furaha isiyo kifani kwamba Shafique ameshindwa. Furaha yangu juu ya kushindwa kwake inazidi furaha ya kushinda kwa Mursi. Na ushindi wa Mursi unamaanisha kuwa mapinduzi yanaendelea," alisema

Lakini Amira Salem yeye anaonyesha khofu juu ya ushindi huu wa Mursi: "Nina wahofia Udugu wa Kiislam. Mursi anatafuta uongozi kwa muda mrefu na Misri haiwezi kuwa kama Iran au Afhghanistan."

Asisitiza ataapa mbele ya Bunge tu
Wakati huo huo rais huyo mpya amesema atakula kiapo tu mbele ya bunge la Misri ambalo hata hivyo lilivunjwa na mahakama ya katiba siku kadhaa zilizopita na sasa anapaswa kula kiapo hicho mbele ya mahakama ambayo ililibatilisha Bunge hilo.

Furaha ya ushindi. Waandamanaji wakishangilia katika viwanja vya Tahrir.
Furaha ya ushindi. Waandamanaji wakishangilia katika viwanja vya Tahrir.Picha: AP

Lakini Waandamanaji nao wamesema hawatafanya makosa waliyoyafanya huko nyuma na wameapa kutoondoka tahrir hadi pale matakwa yao yote yatakapotimizwa ikiwa ni pamoja na kufuta marekebisho ya katiba ya kurejesha Bunge.

Hamada Ramadhan Abdulazizi ni moja wa waandamanaji walioko Tahrir na anasema haondoki mpaka kileleweke: "Nitalala hapa Tahrir hadi matakwa yote ya mapinduzi yafikiwe. wafute makrekabisho ya katiba na warudishe Bunge, wafute na sheria ya dharura ili niweze kujiskia huru nchini Misri."

Magazeti nchini Marekani yataka majenerali washinikizwe
Magazeti nchini Marekani yameitaka serikali yao ambayo ndiyo mfadhili mkuu wa jeshi la Misri, kuwashikiza majenerali kumkabidhi rais mteule mamlaka yake yote. Katika tahrir zake, magazeti ya Washington Post, Newyork Times na Wall Street Jounral yamemtaka pia rais huyo mpya kuwaondolea wasiwasi wale wote wanaohofia utawala wa sharia.

Fataki zikirushwa baada ya kutangazwa kwa ushindi wa Mursi.
Fataki zikirushwa baada ya kutangazwa kwa ushindi wa Mursi.Picha: AP

Mohammed Mursi ambaye chama chake kimetangaza anaacha majukumu yake chamani baada kushinda kiti cha urais, ni msomi aliyebobea katika fani ya uhandisi na aliwahi kufanya kazi katika shirika la Marekani la Safari za anga za juu (NASA) na watoto wake wawili wana uraia wa Marekani.

Lakini Israel ina wasiwasi kwamba ushindi wake unauweka hatarini mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 1979 kati yake na Misri ambao wachambuzi wanasema umeisadia kuokoa kiasi cha dola bilion 270 za Marekani katika kununua vifa vya ulinzi. Gazeti moja la Iran la Far limesema Mursi aliahidi kurejesha uhusiano baina ya Misri na Iran ambao ulivunjwa miaka 30 iliyopita baada mapinduzi nchini Iran.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE\APE\AFPE.
Mharir: Mohammed Abdul Rahman.