1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamtaka Hariri akajiuzulu rasmi akiwa Lebanon

Mohammed Khelef
11 Novemba 2017

Mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon umeingia hatua nyengine mpya, baada ya Marekani kumtaka waziri mkuu aliyejiuzulu akiwa Saudi Arabia, Saad Hariri, kurejea nchini mwake na kufanya hivyo akiwa huko.

https://p.dw.com/p/2nRVk
Saad Hariri
Picha: picture-alliance/AP Photo/H.Malla

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, amesema kuwa Hariri anapaswa kurejea nchini mwake ili kuifanya hatua yake ya kujiuzulu kuwa "rasmi". 

Hariri alijiuzulu katika hali ya kutatanisha Jumamosi iliyopita (4 Novemba) akiwa nchini Saudi Arabia, hali iliyochochea uvumi kwamba anashikiliwa kinyume na matakwa yake na mamlaka za Saudia. Hata hivyo, Tillerson amesema hajaona ishara yoyote kuashiria kuwa "huo ndio uhalisia", ingawa anasema ikiwa Hariri anataka kujiuzulu, anapaswa "kurejea Lebanon na kujiuzulu huko rasmi ili serikali yake iweze kufanya kazi kikamilifu."

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alisema kuwa ameizungumzia hali ya Hariri na mwenzake wa Saudi Arabia, ambaye alimuhakikishia kuwa uamuzi wa Hariri ulikuwa wake mwenyewe. 

Marekani imezionya pande zinazoshiriki mzozo huo ndani na nje ya Lebanon kutokuitumia nchi hiyo kama uwanja wa vita vyao. Akizungumza kwenye ndege akiwa njiani kuelekea Vietnam, Tillerson alizionya Saudi Arabia na washirika wake na pia kundi la Hizbullah linaloungwa mkono na Iran dhidi ya kuiangamiza Lebanon.

Guterres aonya dhidi ya madhara mabaya kabisa Mashariki ya Kati

Saad Hariri na Mfalme Salman wa Saudi Arabia mjini Riyadh, muda mchache kabla ya kutangaza kujiuzulu.
Saad Hariri akiwa na Mfalme Salman wa Saudi Arabia mjini Riyadh, muda mchache kabla ya kutangaza kujiuzulu.Picha: picture-alliance/AA/Bandar Algaloud

Hayo yanakuja katika wakati ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akisema kuwa lazima amani idumishwe nchini Lebanon, na akionya kwamba mzozo mpya unaweza kuja kuwa na madhara mabaya kabisa kwa eneo zima la Mashariki ya Kati.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliwaambia waandishi wa habari jijini New York hapo jana (Ijumaa, 10 Novemba) kwamba amekuwa na mazungumzo ya kina ya ngazi za kisiasa na kidiplomasia nchini Saudi Arabia na Lebanon, na pia nchi nyengine kwenye eneo hilo "au zilizo na ushawishi kwenye Mashariki ya Kati."

"Nimewaambia viongozi hao wa kisiasa na kidiplomasia kwamba ni muhimu kuulinda umoja na utulivu wa Lebanon na utendaji kazi wa taasisi za serikali ya Lebanon," alisema Guterres, akiongeza kuwa Umoja wa Mataiga una wasiwasi sana, lakini wanatarajia kwamba haitoshuhudiwa "hali ikizidi kuwa mbaya ambayo itazaa matokeo mabaya kwenye eneo hilo." 

Hizbullah yasema iko tayari kupambana 

Kiongozi wa Hizbullah, Hassan Nasrallah, anasema Israel haiwezi kufanya kosa la kuishambulia Lebanon wakati huu.
Kiongozi wa Hizbullah, Hassan Nasrallah, anasema Israel haiwezi kufanya kosa la kuishambulia Lebanon wakati huu.Picha: picture-alliance/dpa

Naye kiongozi wa kundi la Hizbullah lenye nguvu kubwa za kijeshi na kisiasa nchini Lebanon, Hassan Nasrallah, amesema hakuna uwezekano wa kutokea vita baina ya nchi hiyo na Israel, licha ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na kujiuzulu kwa Hariri.

Kiongozi huyo mwenye usemi mkubwa alisema kwenye hotuba yake ya Ijumaa kwamba Hizbullah inafuatilia kwa karibu jaribio lolote la Israel kutaka kuutumia mkwamo huo wa kisiasa kuanzisha ugomvi dhidi ya Lebanon, ingawa hadhani ikiwa Israel "itafanya upumbavu huo kwa sasa."

"Israel isidhanie kamwe kwamba tuna matatizo makubwa kiasi hicho. Hapana. Kwa hivyo, isije ikafanya kosa la kutushambulia. Leo, sisi tunajiamini zaidi na tunajihisi kuwa madhubuti zaidi mbele ya kitisho chochote kile," alionya Nasrallah.

Kauli ya Nasrallah inakuja huku raia kadhaa wa mataifa ya Ghuba ya Arabuni wakianza kuondoka nchini Lebanon kufuatia serikali zao kuwataka kufanya hivyo. Mamia ya wanaume na wanawake kutoka Saudi Arabia, Kuwait na Bahrain walionekana asubuhi ya Ijumaa wakisafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rafik Hariri mjini Beirut. 

Mataifa hayo pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu zimewataka raia wake kuondoka Lebanon.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/dpa
Mhariri: Yusra Buwayhid