1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamuwekea vikwazo mkuu wa jeshi la Eritrea

24 Agosti 2021

Marekani imemuwekea vikwazo mkuu wa wafanyikazi wa jeshi la Eritrea Filipos Woldeyohannes juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika jimbo la Tigray.

https://p.dw.com/p/3zP0z
Äthiopien I Situation in Tigray
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Eritrea imekanusha kuwa wanajeshi wake wamehusika na matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia. 

Vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Jenerali Filipos Woldeyohannes, vinafuatia ripoti kuwa Eritrea imepeleka wanajeshi zaidi katika jimbo la Tigray linaloshuhudia mapigano.

Marekani imesema itazizuia mali zote za Filipo na kwamba raia wa Marekani watazuiliwa kufanya biashara ya aina yoyote na mkuu huyo wa wafanyikazi wa jeshi la Eritrea.

Soma zaidi: Vikosi vya Ethiopia vyatuhumiwa kufanya uhalifu wa kingono

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema katika taarifa kuwa, chini ya usimamizi wa Woldeyohannes, wanajeshi wa Eritrea walihusika na ubakaji, uporaji, na unyanyasaji wa kijinsia.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa wanajeshi wa Eritrea waliwabaka, kuwatesa na hata kuwaua raia katika jimbo la Tigray.

Eritrean refugees protest conditions at Tigray camps in Addis Ababa
Wakimbizi kutoka Eritrea wakiandamana kulalamikia juu ya hali mbaya kwenye kambi za wakimbizi mjini Addis AbabaPicha: REUTERS

Eritrea hata hivyo, kwa hasira iliyapinga madai hayo kwa kusema hayana msingi wowote. Wizara ya mambo ya nje ya Eritrea, imesema hio sio mara ya kwanza kwa Marekani kuanzisha kampeni yenye nia ya kuipaka tope Eritrea.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken kupitia taarifa, amesema Marekani inalaani kwa nguvu zote ukiukaji wa haki za binadamu nchini Eritrea.

Blinken ameitolea mwito serikali ya Eritrea kuviondoa kabisa vikosi vyake vya ulinzi kutoka Ethiopia.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani ameonyesha wasiwasi wake juu ya kurudi tena kwa vikosi vya ulinzi vya Eritrea vya EDF baada ya kuondoka Ethiopia mwezi Juni.

Amelihimiza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kushirikiana ili kutafuta suluhu ya mzozo unaoendelea huko Tigray.

Soma zaidi: Serikali ya Ethiopia yatishia kufanya operesheni tena Tigray

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, "Raia wa Ethiopia wameteseka sana. Hali ya kibinadamu ni mbaya mno. Mamilioni ya watu wanahitaji msaada. Miundo mbinu imeharibiwa. Na tumepokea ripoti kuwa wanawake wamefanyiwa ukatili. Kuendelea kwa mapigano kumewatia watu hofu zaidi."

Kwa miezi kadhaa, serikali za Ethiopia na Eritrea zilikanusha kuhusika na mapigano katika jimbo la Tigray kinyume na ushuhuda kutoka kwa waakazi wa jimbo hilo pamoja na kauli za makundi ya kutetea haki za binadamu, wafanyikazi wa misaada na hata baadhi ya wanadiplomasia na maafisa wa jeshi.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed hatimaye alikiri juu ya uwepo wa vikosi vya ulinzi vya Eritrea mnamo mwezi Machi wakati alipokuwa akilihutubia bunge na aliahidi wakati huo, kwamba wanajeshi hao wataondoka.

Eritrea yenyewe iliapa kuondoa wanajeshi wake Tigray mnamo mwezi Aprili, lakini hilo limeonekana kuwa ni ahadi hewa.