1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapiga marufuku raia wake kwenda Korea kaskazini

Sekione Kitojo
1 Septemba 2017

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imepiga marufuku raia wake kwenda Korea kaskazini hatua ambayo inaanza rasmi leo Ijumaa (01.09.2017),wakati nchi hizo zikilumbana kuhusu dhamira ya Pyongyang kujitengezea silaha.

https://p.dw.com/p/2jBrQ
Nordkorea - US-Student Otto Warmbier
Otto Warmbier alipokamatwa na polisi wa Korea kaskaziniPicha: picture alliance/dpa/MAXPPP

Wakati  huo  huo waziri  wa mambo  ya  kigeni  wa  Ufaransa amesema  Korea  kaskazini ina uwezo wa  kurusha makombora ya  masafa marefu  katika  miezi michache  ijayo na  kuitaka  China  kuchukua  hatua  zaidi  kutatua mzozo  huo.

Hatua  ya  kupiga  marufuku  raia  wa  marekani  kutembelea  Korea kaskazini  imechukuliwa  kutokana  na  kifo  cha  mwanafunzi  Otto Warmbier  mwezi  Juni, siku  chache  baada  ya  kijana  huyo mwenye  umri  wa  miaka  22  kurejeshwa  nyumbani   akiwa hajitambua  kufuatia  kufungwa  jela  kwa  zaidi  ya  mwezi  mmoka nchini  humo.

Nordkorea Kim Jong-Un
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong UnPicha: Reuters/KCNA

Alihukumiwea  kwa  kosa  la  kula  njama  dhidi  ya  taifa  hilo  kwa kujaribu  kuiba  bango  la  propaganda  kutoka  katika  hoteli  mjini Pyongyang  na   kuhukumiwa  kifungo  cha  miaka  15  na  kazi ngumu, huku  rais  Donald Trump  akiulaumu  utawala  wa  kinyama wa  Pyonyang , kwa  hali  madhara  aliyoyapata.

Katika  tovuti  yake , wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Marekani imesema  imechukua   uamuzi  huo  kutokana  na "hali  mbaya  na kitisho  kinachoongezeka  cha  kukamatwa  na  kufungwa  kwa kipindi  kirefu raia  wa  Marekani".

Wamarekani  watatu  wanaoshutumiwa  kwa  uhalifu mbali  mbali dhidi  ya  taifa  hilo  wako jela  nchini  Korea  kaskazini, nchi  ambayo imo  katika  hali  ya  mvutano  na  wasi  wasi  mkubwa   na  utawala wa  Trump  kuhusiana  na  mpango  wake  uliopigwa  marufuku  wa silaha  za  kinyuklia.

Mapema  wiki  hii  Pyongyang  ilifyatua  kombora  kupitia  anga  ya Japan , katika  hatua  ya  juu  kabisa  ya  kuchochea  mzozo  huo, na imetishia  kurusha  makombora  zaidi  kuelekea  kisiwa  cha  Guam ambacho  kinamilikiwa  na  Marekani  katika  bahari  ya  Pasifiki.

Majaribio  ya  Korea  kaskazini

Mwezi  Julai  Korea  kaskazini  ilifanya  majaribio  yake  mawili yaliyofanikiwa   ya  makombora  ambayo  yana uwezo  wa  kuruka kutoka  bara  moja  kwenda  lingine, na  hatimaye  kuweza  kufika nchini  Marekani.

Nordkorea Raketenstart
Kombora la Korea kaskazini Picha: Reuters/KCNA

Marufuku  hiyo  hata  hivyo  haiwagusi waandishi  habari, wawakilishi wa  shirika  la  msalaba  mwekundu, wale  wanaosafiri  kwa madhumuni  ya  kutoa  msaada  wa  kiutu , ama  safari  ambazo wizara  ya  mambo  ya  kigeni  inaziona  kuwa  na  maslahi  na Marekani. Lakini  asasi  za  kijamii  zinazofanyakazi  nchini  Korea kaskazini kibinafsi  zimeeleza  wasi  wasi  wake  juu  ya  vipi  hatua hiyo  itafanyakazi  na  athari  zake  katika  kazi  yao. 

Raia wachache  wa  Marekani  ambao  wamebaki  nchini  humo wameondoka  siku  ya  Alhamis, zimesema  baadhi  ya  ripoti. Waziri anayehusika  na  kuziunganisha  Korea mbili  wa  Korea  kusini  Lee Eugene amesema  Korea  kaskazini  inapaswa  kuacha  uchokozi.

"Korea  kaskazini  inaendelea  kufanya uchokozi. Msimamo  wa serikali  yetu  kwamba  tunahitaji  suluhisho  la  amani katika  suala la  kinyuklia  la  Korea  kaskazini  na rasi  ya  Korea haujabadilika. Pia , tunaitaka  Korea kaskazini  kuacha kutoa  matamshi  ya ukosoaji  na  vitisho  na  kuchukua  njia  ya  mazungumzo na ushirikiano."

Zentralafrika Bangui - Französischer Verteidigungsminister Jean-Yves Le Drian bei Militärbasis
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian Picha: Reuters/Stringer

Wakati  huo  huo waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ufaransa  Jean-Yves Le Drian  amekiambia  kituo  cha  redio  cha  RTL  kwamba hali  ni  mbaya , tunaona  Korea  kaskazini  ikiwekea  malengo  ya kesho  ama  kesho  kutwa  kurusha  makombora  yenye  vichwa  vya kinyuklia. Kwa  wakati  huu  ambapo  Korea  ya  kaskazini  ina uwezo  wa  kushambulia  Marekani , hata  Ulaya, lakini  hasa  Japan na  China, hali  itakuwa  mbaya  zaidi.

Le Drian  ambae  alizungumza  na  mwenzake  wa  China  siku  ya Alhamis , amesema  kila  kitu kinapaswa  kufanywa  kuhakikisha vikwazo  vya  hivi  karibuni  vya  umoja  wa  Mataifa  vinatekelezwa na  kuitaka  China , mshiriam mkubwa  wa  kibiashara  wa Pyonyang, kuchukua  juhudi  zote  kuvitekeleza.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre

Mhariri:   Idd Ssessanga