1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yashutumu vikali kufichuliwa kwa stakabadhi za siri.

Halima Nyanza26 Julai 2010

Marekani imeshutumu vikali kufichuliwa kwa stakabadhi za siri zilizo na maelezo kuhusiana na vita vya Afghanistan na kusema kuwa hali hiyo itahatarisha usalama wa taifa na maisha ya Wamarekani na washirika wao.

https://p.dw.com/p/OVBc
Hamid Gul, aliyekuwa mkuu wa shirika la kijasusi la Pakistan ambaye ametajwa pia katika taarifa hizo.Picha: picture-alliance/ dpa

Nyaraka hizo za siri za kijeshi ambazo zinapatikana katika mtandao wa  Wikileaks, zilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la kila siku la Ujerumani la Der Spiegel, The Guardian la Uingereza na The New York Times.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo zilizofichuliwa jana, Maafisa wa Marekani  kwa muda mrefu walikuwa wakiitilia wasiwasi Pakistan kuwasaidia kisiri wapiganaji wa Taliban, wakati ikipokea msaada mkubwa kutoka Marekani.

Pakistan ni mshirika mkubwa wa Marekani katika eneo hilo.

Aidha nyaraka hizo zinaelezea wawakilishi kutoka mashirika ya kijasusi ya Pakistan, kukutana na Wataliban katika mkutano wa siri kwa ajili ya kuandaa mitandao ya kijeshi kupambana na wanajeshi wa Marekani.

Hata hivyo, katika taarifa yake aliyoitoa kuhusiana na kupatikana kwa nyaraka hizo, Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Rais wa Marekani Barack Obama, Jim Jones amesema kuvuja kwa nyaraka hizo zisizoaminika hakutaathiri ahadi ya kuimarisha uhusiano wao na Afghanistan na Pakistan katika harakati za kumshinda adui wao na kusaidia watu wa Afghan na Pakistan kupata amani.

Licha ya kushutumu kuvuja kwa nyaraka hizo, Marekani imesema haishangazwi na taarifa hizo, na kwamba inafuatilia uhusiano uliopo katimya majasusi wa Pakistan na wapiganaji wa Afghanistan.

Mapema mwaka jana, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates wana wasiwasi na taarifa za shirika moja la upelelezi la Pakistan kuwa na mawasiliano na makundi ya watu wenye siasa kali.

Kwa upande wake Pakistan imesema kuvuja kwa ripoti hizo ni jambo lisilopaswa.

Balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa Hussain Haqqan amesema taarifa hizo zilizotolewa haziendani na ukweli ulioko sasa.

Nyaraka hizo za siri pia zimeelezea madai kwamba Iran nayo inawasaidia kufedha na silaha wapiganaji wa Taliban, na taarifa pia kuhusiana na kusambaa kwa rushwa nchini Afghanistan zinavyokwamisha vita dhidi ya Afghanistan, mapambano ambayo yanafanywa na wanajeshi wa kimataifa.

Nyaraka hizo za siri zilizochapishwa jana katika vyombo vitatu vya habari zinaelezea visa ambavyo havikuripotiwa vya kuuwawa kwa raia wa Afghanistan, na pia kikosi maalum kinachosaka na kuua au kuwakamata viongozi wa Taliban na uasi unaokua kwa usaidizi wa Pakistan.

Wakati huohuo Ujerumani leo imetaka kufanywa uchunguzi juuu ya madai hayo ya Pakistan na Iran kuwasaidia Taliban.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Guido WesterWelle ameyasema hayo pembezoni mwa mkutano pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya uliofanyika Brussels Ubelgiji.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza William Hague amesema wanamatumaini kuwa kuvuja kwa nyaraka hizo hakutaathiri mapambano yanayofanywa nchini Afghanistan.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri:Josephat Charo