1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatafakari kuwaondoa wanajeshi Ujerumani

Bruce Amani
30 Juni 2018

Wizara ya ulinzi ya Marekani inaangazia uwezekano wa kuwaondoa wanajeshi wake waliopo Ujerumani baada ya Rais Donald Trump kueleza nia yake azma yake ya kuchukua hatua hiyo

https://p.dw.com/p/30aJp
Deutschland US-Army: Übergabe der Hubschrauberstaffeln in Illesheim
Picha: picture-alliance/dpa/N. Armer

Gazeti la Marekani la Washington Post limeripoti hapo jana likinukuu vyanzo ambavyo havikutaka kutambulishwa vyenye ufahamu kuhusu suala hilo, ambavyo vilisema maafisa wa Marekani walikuwa wakifanya tathmini ya gharama na athari za kuwahamisha ama baadhi yao au wanajeshi wake wote, wapatao 35,000 na kuwapeleka Marekani ama Poland. Kulingana na Washington Post, maafisa wa ngazi za juu wa wizara ya ulinzi hawajashirikishwa kwenye mchakato huo.

Trump alionyesha azma yake hiyo wakati wa mkutano katika Ikulu ya White House mapema mwaka huu baada ya kuelezea mshituko juu ya kikosi cha wanajeshi wa Marekani kilichopo Ujerumani, ambacho ni kikubwa zaidi barani Ulaya. Kulingana na gazeti hilo, maafisa hao wa Marekani wanajaribu kuangalia iwapo hatua hiyo itaakisi azma ya Trump ama ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa kuelekea mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Julai 11-12, mjini Brussels.

Msemaji wa Baraza la Ulinzi wa Taifa katika Ikulu ya White House na Makao makuu ya Ulnzi amesema Wizara ya Ulinzi amesema kila mara hutathmini mipango ya kutumwa nje vikosi vya Marekani.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen na mwenzake wa Marekani Jim Mattis hawakutaja mpango wa aina hiyo baada ya mkutano wao wa wiki iliyopita.

Rais Trump amewashutumu washirika wa NATO katika Umoja wa Ulaya, na hasa Ujerumani, kwa kushindwa kutimiza kiwango cha matumizi ya NATO ya asilimia mbili ya pato jumla la taifa.

Ujerumani ilitumia asilimia 1.24 ya pato jumla lake kwenye ulinzi katika mwaka wa 2017 na inapanga kufikisha asilimia 1.5 ifikapo mwaka wa 2024. Poland ilitumia asilimia 1.99 ya pato jumla la nchi kwenye ulinzi katika mwaka wa 2017 na inatarajiwa kujiunga na nchi nyingine tatu za NATO katika Umoja wa Ulaya – ambazo ni Uingereza, Estonia na Ugiriki – ambazo zimetimiza kiwango hicho cha NATO.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Lilian Mtono