1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaufunga ubalozi wake mdogo mjini Jerusalem

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
4 Machi 2019

Hatua ya Marekani ya kuufunga ubalozi wake mdogo mjini Jerusalem ni hatua ya kuuteremsha hadhi uwakilishi wake wa kibalozi kwa Wapalestina. Uamuzi huo umetangazwa Jumatatu na wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3EPap
Israel US-Botschafter David Friedman Eröffnung amerikanische Botschaft in Jerusalem
Picha: Getty Images/L. Mizrahi

Kwa miongo kadhaa ubalozi huo mdogo katika mji wa Jerusalem ulitambulika kama ubalozi wa Marekani katika mamlaka ya Palestina. Nakuanzia sasa jukumu la ubalozi huo uliofungwa litatimizwa na kitengo cha masuala ya Wapalestina chini ya mamlaka ya ubalozi mkuu.

Kutokana na mabadiliko hayo ya kiishara, mamlaka juu ya shuhguli za kibalozi za Marekani katika Ukanda wa Gaza na kwenye Ukingo wa Magharibi zitakabidhiwa kwa balozi David Friedmanm ambaye ni muungaji mkono mkubwa na pia mfadhili wa mipango ya kuendeleza ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye maeneo ya Wapalestina. Balozi huyo pia mkosoaji mkubwa wa uongozi wa Wapalestina.

Uamuzi huo uliotangazwa mapema leo na wizara ya mambo ya nje ya Marekani unaanza kutekelezwa leo hii. Msemaji wa wizara hiyo ameeleza kwamba, unatokana na juhudi ambazo Marekani inafanya duniani kote kwa lengo la kuongeza tija katika shuhguli zake za kidiplomasia.

Balozi wa Marekani nchini Israel David Frieman
Balozi wa Marekani nchini Israel David FriemanPicha: picture-alliance/Zumapress/M. Brochstein

Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje Robert Palladino amehakikisha kwamba, hatua hiyo haina maana ya kubadilisha sera ya Marekani juu ya Jerusalem, Ukingo wa magharibi au Ukanda wa Gaza. Uamuzi wa Marekani uliwakasirisha Wapalestina ulipotangazwa kwa mara ya kwanza na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo mnamo mwezi wa Oktoba mwaka uliopita.

Wapalestina wanatuhumu kwamba Marekani inalenga shabaha ya kutambua sera ya Israel ya kuyadhibiti maeneo ya Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi ambayo Wapalestina wanatumai kuwa katika nchi yao hapo baadae. Mjumbe wa baraza la Wapalestina Saeb Erakat amesema hatua ya Marekani inamaanisha mwisho kabisa wa dhima ya Marekani katika juhudi za kuusuluhisha mgogoro wa Israel na Wapalestina.

Mwaka uliopita Marekani iliutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na iliuhamishia ubalozi wake kwenye mji huo kutoka Tel Aviv. Uamuzi huo ulioatangazwa mapema leo ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na utawala wa Trump za kuiunga mkono Israel na kuwatenga Wapalestina.

Marekani pia imepunguza misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina ikiwa pamoja na misaada kwa ajili ya hospitali na miradi ya ujenzi. Utawala wa Marekani umechukua hatua hizo kwa madai kwamba Wapalestina wanakataa kufanya mazungumzo ya amani na Israel. 

Vyanzo: /APE/AFP