1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiondolea vikwazo vya usafiri Chad

11 Aprili 2018

Rais Donald Trump wa Marekani ameondoa vikwazo vya usafiri vilivyokuwa vimewekewa raia wa Chad baada ya serikali yake kuvitathmini upya vikwazo hivyo kwa miezi sita.

https://p.dw.com/p/2vpxY
USA Donald Trump erneuert Einreiseverbot
Picha: picture-alliance/dpa/NOTIMEX/Casa Blanca

Kulingana na Ikulu ya White House, uchunguzi huo uligundua kuwa taifa hilo lililoko Afrika ya Kati lilikuwa limeimarisha viwango vya usalama na utoaji wa mawasiliano kuhusu raia wake kwa Marekani.

Chad ilikuwa miongoni mwa nchi nane zilizolengwa na vikwazo vya usafiri kwa raia wake vilivyowekwa na Marekani. Nchi nyengine ni Iran, Libya, Syria, Somalia, Yemen, Venezuela na Korea Kaskazini.

Katika taarifa yake, Rais Trump amesema nchi nyingine saba bado hazijaimarisha mifumo yao ya utoaji taarifa na zitasalia katika orodha hiyo. Wakosoaji wa Trump wamemtuhumu kwa kuweka vikwazo dhidi ya raia wa nchi nyengine kinyume cha katiba kwa kulenga nchi zilizo na idadi kubwa ya Waislam. Chad inachukuliwa kama rafiki wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi.