1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yazuia dola milioni 65 kwa Palestina

Grace Kabogo
17 Januari 2018

Marekani imezuia Dola milioni 65 ambazo zilikuwa zimepangwa kwa ajili ya kulisaidia shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA.

https://p.dw.com/p/2qxx6
Palästina PK Trump und Abbas
Picha: Reuters/J. Ernst

Uamuzi huo umefikiwa wiki mbili baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kuacha kutoa msaada kwa Wapalestina. Maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani walisema jana kuwa nchi hiyo itatoa Dola milioni 60 kati ya Dola milioni 125 ambazo zilipangwa hapo kabla kwenda katika shirika hilo la UNRWA, lakini fedha zilizobakia zitazuiwa kwa sasa.

Hata hivyo, wizara hiyo imesisitiza kwamba uamuzi huo haujachukuliwa kwa lengo la kuwashinikiza viongozi wa Palestina, bali kwa sababu Marekani inataka nchi nyingine kusaidia katika malipo pamoja na kulifanyia mageuzi shirika hilo. Msemaji wa wizara hiyo, Heather Nauert amewaambia waandishi habari kwamba hatua hiyo haikusudii kumuadhibu mtu yeyote na kwamba kwa muda mrefu Marekani imekuwa mfadhili mkuu wa shirika hilo.

''Serikali ya Marekani na utawala wa Trump unaamini kwamba watu wanatakiwa kuchangia katika mzigo huu wa gharama. Tungependa nchi nyingine, hasa zile zinazoikosoa Marekani kwa kile zinachoamini kuhusu msimamo wetu dhidi ya Wapalestina, kujitokeza na kulisaidia shirika la UNRWA,'' alisema Nauert.

Israel - Palästina | Symbolbild UNWRA
Mwanamke wa Kipalestina akisubiri msaada kutoka UNRWAPicha: Getty Images/AFP/M. Hams

UNRWA yashtushwa na uamuzi wa Marekani

Mkurugenzi wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina, Pierre Krahenbuhl amesema ameshutushwa na uamuzi wa Marekani na amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchangia.

Amesema Dola hizo milioni 60 zingesaidia kuendesha shule na hospitali ambazo zimefunguliwa kwa sasa, lakini fedha hizo ni kidogo ikilinganishwa na zile zilizotolewa na Marekani kwa mwaka 2017, ambazo zilikuwa Dola milioni 350.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hakuarifiwa kuhusu uamuzi huo, lakini taarifa alizozisikia zinampa wasiwasi mkubwa. Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon amesema shirika hilo linazitumia vibaya fedha hizo na zilikua zinatumika kuunga mkono propaganda dhidi ya Israel, kuendeleza shida za wakimbizi wa Palestina pamoja na kuchochea chuki.

Wakati huo huo, viongozi wa Palestina wamesema uamuzi huo wa Marekani unawalenga watu wanaoishi katika mazingira magumu na walioko hatarini zaidi. Mjumbe wa kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Wapalestina, PLO, Hanan Ashrawi amesema serikali ya Marekani inaonekana kufuata maelekezo yanayotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ya kulifunga shirika pekee lililoanzishwa na jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya kulinda haki za wakimbizi wa Palestina na kuwapatia huduma muhimu.

Ashrawi amesema kuzuiwa kwa fedha hizo kunaweza kuleta mzozo wa kibinaadamu na kuwanyima wakimbizi haki ya kupata elimu, huduma za afya, makaazi pamoja na heshima ya maisha.

Aidha, ameionya Marekani kuhusu uamuzi wake huo akisema utaanzisha hali itakayochochea zaidi kukosekana kwa utulivu katika ukanda huo na kuyafanya mazungumzo ya amani kuwa magumu zaidi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA
Mhariri: Saumu Yusuf