1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masai anyakua medali ya dhahabu

16 Agosti 2009

Baada ya Masai wa Kenya kunyakua medali ya kwanza ya dhahabu kwa nchi yake wanariadha wenzake watowa bishara nzuri katika mbio za kuruka viunzi mita 3,000.

https://p.dw.com/p/JCOX
Kenya's Linet Chepkwemoi Masai celebrates after winning the gold medal in the final of the Women's 10,000m during the World Athletics Championships in Berlin on Saturday, Aug. 15, 2009. (AP Photo/Matt Dunham)
Linet Chepkwemoi Masai wa Kenya akifurahia ushindi wa medali ya dhahabu katika mbio ndefu za mita 10,000 wanawake mjini Berlin.Picha: AP

Mpambano wa nusu fainali wa mbio za mita 100 unaowakutanisha wanariadha mashuhuri kabisa duniani Usain Bolt wa Jamaica na Tyson Gay wa Marekani kufanyika usiku huu.

Matumaini ya Wakenya kurudia vitu vyao vya kusomba medali walivyoonyesha katika michezo ya Olympiki katika mbio za kuruka viunzi mita 3,000 wanaume yameendelea kuwa hai leo hii baada ya wanariadha wake watatu hatari kusonga mbele katika fainali bila ya mushkeli.

Bingwa mtetezi wa dunia na Olympiki Brimin Kipruto ameshinda mbio za kundi lake kwa muda wa dakika 8 sekunde 18 nukta 7 wakati wenzake Ezekiel Kemboi na Richard Mateelong pia wamejipatia ushindi katika mbio za makundi yao tafauti.

Kipruto na Kemboi mshindi wa medali ya shaba wa michezo ya Olympiki ya Athens ambaye ana rekodi ya dunia ya kukimbia kwa kasi sana mwaka huu na Mateelong wote watatu walikuwa jukwaani kwa pamoja kutwaa medali katika michezo ya Olympiki mjini Beijing mwaka jana na ni vigumu kuona mmoja wao anashindwa kuwa mshindi wa fainali hizi hapo Jumanne.

Kenya imekuwa ikifurahia ufalme usiokuwa na upinzani katika mbio hizo za kuruka viunzi kwa kushinda mara saba mfululizo ubingwa wa Olympiki kuanzia michezo ya Los Angeles hapo mwaka 1984.

Mkenya wa nne Paul Koech pia amefanikiwa kuingia fainali pamoja na Bob Tahri wa Ufaransa na Ruben Ramolefi wa Afrika Kusini.

Wakati huo huo matumaini ya bingwa mtetezi wa Kenya Janeth Jepkosgei kutetea taji lake katika mbio za mita 800 wanawake yameishia kwa huzuni kubwa katika raundi ya kwanza leo hii katika michuano ya ubingwa huo wa riadha duniani inayoendelea mjini Berlin.

Mwanriadha huyo mwenye umri wa miaka 26 anayeshikilia medali ya fedha ya michezo ya Olympiki ya mwaka 2008 alianguka katika njia ya kukimbia baada ya miguu yake kuingiliana na mkimbiaji nyota wa Afrika Kusini Caster Semanya.

Mkenya huyo aliathirika zaidi baada ya kuanguka na kukanyagwa na wakimbiaji wengine wakati Semanya aliekuwa nusura naye aanguke aliweza kuendelea na kumalizia mbio kwa ushindi wa kwanza kwa kutumia dakika mbili sekunde mbili nukta 51.

Kutokana na ajali hiyo Jepkosgei alimalizia nafasi ya saba.

Kenya imepinga kutolewa kwa mwanariadha wake huyo na Shirikisho la Riadha la Kimataifa hapo kesho linatazamiwa kutowa uamuzi juu ya malalamiko hayo ya Kenya.

Naye Pamela Jelimo mwanariadha mwengine wa Kenya amerudi tena katika jukwaa kuu leo hii baada ya kuingia duru ya pili ya mbio za mita 800 wanawake na anatumai kurudi katika hali iliompa medali ya dhahabu ya Olympiki mwaka jana.

Kutokana na majeraha mapema mwaka huu Jelimo hali yake ilikuwa tafauti kabisa na ile ya mwaka 2008 ambapo alishika nafasi ya tatu ya mkimbiaji bora kabisa wa mbio hizo baada ya kujinyakulia medali ya dhahabu Beijing kwa kutumia dakika moja na sekunde 54 nukta moja.

Wanariadha nyota wa Jamaica na Marekani wameingia katika duru ya pili ya mbio za mita 100 wanawake leo hii.

Mkimbiaji wa Marekani Carmelia Jeter aliongoza mbio hizo kwa kutumia muda wa sekunde 11.22 na mwenzake bingwa wa dunia wa mwaka 2005 Lauryn Williams alitumia muda wa sekunde 11.36.

Kwa upande wa Wajamaica anayeshikilia rekodi ya dunia ya mwaka 2009 Kerron Steward alitumia sekunde 11.34 na bingwa wa dunia Shelly-Ann Fraser alitumia sekunde 11.41.

Duru ya pili inafanyika jioni hii na fainali kufanyika hapo kesho.

Katika mbio za matembezi ya kilomita 20 Urusi leo imejinyakulia medali ya pili ya dhahabu baada ya bingwa mtetezi Olga Kaniskina kushinda matembezi hayo ya wanawake.

Bingwa huyo wa Olympiki mwenye umri wa miaka 24 alitumia saa moja dakika 28 na sekunde 9.Olive Loughnane wa Ireland alishika nafasi ya pili na kuondoka na medali ya fedha wakati Hong Liu wa China aliangukia medali ya shaba baada ya kushika nafasi ya tatu.

Sasa tunawadondolea mawili matatu ya matokeo ya jana ambapo kulikuwa na medali za dhahabu kwa Valery Borchin wa Urusi katika matembezi ya kilomita 20 wanaume na Linet Masai wa Kenya kunyakua ile ya mita 10,000 wanawake kwa ushindi wa kusisimua.

Kujitowa kwa bingwa mtetezi mara mbili wa Ethiopia Tirunesh Dibaba kulifunguwa mbio ndefu za mita 10,000 wanawake lakini hakuna alietabiri matokeo yake yatakuwa ya aina yake.

Ni jambo la kawaida kuwaona wanariadha wa Afrika Mashariki wakiwa mstari wa mbele katika mbio hizo wakati Waethiopia watatu na Wakenya wawili wakifukuzana lakini Masai alikuja kushika nafasi ya tatu zikiwa zimebakia mita 250.

Meselech Melakamu wa Ethiopia alichomoka na kudhania kuwa ameshinda ambapo alinyanyua mikono yake juu kusherehekea wakati Masai aliekuwa nyuma yake alipokuja kumpita kwenye mstari wa ushindi kwa sekunde 10.Masai alitumia muda wa dakika 30 sekunde 51.24.

Akina dada wa Ethiopia ambao walishinda michuano ya ubingwa wa dunia iliopita mara tano waliishia kwa medali za fedha na shaba.

Mbio ziliokuwa zimechangamkiwa sana hapo jana zilikuwa za mita 100 ambapo nyota wa mbio hizo Usain Bolt wa Jamaica na Tyson Gay wa Marekani walipuruzia kumaliza mbio hizo kwa urahisi bila ya upinzani ambapo bingwa mtetezi Gay alitumia sekunde 9.98.

Lakini mambo yako leo usiku katika mpambano wa nusu fainali ambapo anayeshikilia medali ya dhahabu ya Olympiki Bolt anakutana kwa mara ya kwanza mwaka huu na Gay bingwa wa dunia mara mbili. Bolt ana rekodi ya dunia ya sekunde 9.69 aliyoweka katika michezo ya Olympiki ya Beijing mwaka jana wakati Gay ana rekodi ya kukimbia kwa kasi kabisa mwaka huu ya sekunde 9.77.

Mwandishi: M.Dahman/DPA/AFPE

Mhariri: P.Martin