1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashabiki wa Brazil kusaidia au kuua matumaini ya "selecao"

11 Juni 2014

Hadithi ya ari ya mashabiki wa Brazil itatekeleza jukumu muhimu wakati timu yao ikilenga kunyakua Kombe la Dunia kwenye ardhi ya nyumbani, lakini matarajio yao makubwa mno pia yataiwekea shinikizo kubwa ‘selecao’

https://p.dw.com/p/1C3de
Fussball Brasilien Fans
Picha: picture-alliance/dpa

Brazil inajivunia kwa kiasi kikubwa mafanikio yao ya ushindi wa mara tano wa Kombe la Dunia, na ushabiki wao wa imani utakamatika wakati Brazil itakapofungua dimba dhidi ya Croatia mnamo Juni 12. Kuandaa Dimba hilo kunaambatana na kumbukumbu ya machungu ya mwaka wa 1950, mara ya mwisho dimba hilo liliandaliwa nchini humo, wakati Uruguay iliizaba Brazil magoli mawili kwa moja katika mechi ya kuamua mshindi wa taji hilo.

Wabrazil watatarajia kuwa timu ya taifa – selecao, itaweza sasa mara hii kuliondoa kosa ililofanya katika mwaka wa 1950. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, shabiki wa wastani wa Brazil amekuwa akiyaongeza matumaini kuwa mara hii wataweza kushinda Kombe la Sita la Dunia.

Ushindi wa Brazil katika dimba la Kombe la Mashirikisho, ambalo liliandaliwa mwaka jana, ulisaidia kuyaamsha mapenzi ya mashabiki kwa timu yao.

Brazil walipasha misuli moto kabla ya dimba la Kombe la Kombe la Dunia, kwa kunyakua Kombe la Mabara mwaka wa 2013
Brazil walipasha misuli moto kabla ya dimba la Kombe la Dunia, kwa kunyakua Kombe la Mabara mwaka wa 2013Picha: picture-alliance/dpa

Selecao waliwachabanga Uhispania magoli matatu kwa sifuri katika fainali, na kujipiga kifua katika uwanja wa Maracana -- mahali ambako walipewa kichapo mwaka wa 1950 – na kujipa kila sababu ya majivuno dhidi ya Uhispania ambao ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia. Umati wa mashabiki uliofurika uwanjani kwa kuvaa rangi za kijani na njano, uliendelea kuimba wimbo wa taifa hata baada ya wimbo wenyewe kukamilika kuchezwa, na bila shaka hilo lilichangia katika ushindi huo mkubwa wa Brazil dhidi ya Uhispania. Walinguruma wakisema kuwa “Bingwa amerudi” wakati nahodha Thiago Silva aliponyanyua kombe la Mashirikisho. Na sasa Kombe la Dunia litawapandisha hamasa mashabiki hata zaidi.

Kocha wa Brazil Luiz Felipe Scolari anasema Brazil ina kitu ambacho timu nyingine hazina, ambacho ni mchezaji wa 12. Anaongeza kuwa timu yao sasa ina mashabiki milioni 200 ambao, hawatakuwa uwanjani, lakini watajumuika nao.

Lakini kwa upande mwingine wa juhudi za mashabiki wa Brazil ni uwezekano wa uzito wa matarajio hayo kuiangusha timu ya taifa.

Kocha wa timu ya Brazil Luiz Felipe Scolari anataka kuhakikisha Kombe la Dunia linabakia Brazil
Kocha wa timu ya Brazil Luiz Felipe Scolari anataka kuhakikisha Kombe la Dunia linabakia BrazilPicha: Reuters

Wabrazil wanaweza kuwa na uchungu sana kwa timu yao wakati inaposhindwa kuwapa kinachofahamika kama ‘jogo bonito’ – mchezo mzuri – wanaoutaka na ilikumbwa na dhihata na kuzomewa kwa kuondolewa katika robo fainali za vinyang’anyiro viwili vilivyopita vya Kombe la Dunia.

Kama Brazil itashindwa kutimiza matarajio ya mashabiki katika mechi zao za mwanzo, athari zake zinaweza kuiyumbisha timu. Pia kuna hofu kuwa kama timu ya Brazil itapata matokeo duni, hali hiyo huenda ikawasha moto wa vuguvugu la maandamano ambalo lilizuka mwaka jana kupinga gharama za kiasi cha dola bilioni 11 zinazotumika kuandaa dimba la Kombe la Dunia katika nchi ambayo ina mahitaji ya elimu, afya na usafiri.

Maandamano hayo yamegeuka na kuwa vurugu wakati mwingine, ikiwa ni pamoja na wakati wa fainali ya Kombe la Mabara, wakati harufu ya mabomu ya kutoa machozi yaliyotumiwa kuwatawanya waandamanaji ilipoingia katika uwanja wa Maracana hata wakati timu ya Brazil ilikuwa ikishangilia ushindi wao.

“hakutakuwa na Kombe la Dunia!” ndiyo kilio kipya cha vuguvugu hilo la maandamano. Kama litapata msukumo wa kutosha wa kuvuruga tamasha hilo au kupotelea ndani ya msisimko wa Kombe la Dunia huenda ikategemea kwa sehemu Fulani na mchezo wa timu ya taifa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu