1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya Syria yalivunja sheria ya kimataifa

Daniel Gakuba
21 Aprili 2018

Ripoti ya wataalamu wa masuala ya sheria za kimataifa katika Bunge la Ujerumani imesema mashambulizi yaliyofanywa na Marekani, Uingereza na Ufaransa dhidi ya Syria mapema mwezi Aprili yalikiuka sheria ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/2wRHd
Syrien - US-Militärschlag auf Damaskus
Picha: picture alliance/AP Photo/H. Ammar

Ripoti ya wataalamu wa sheria za kimataifa katika Bunge la Ujerumani, imesema mashambulizi yaliyofanywa na nchi tatu za Magharibi hayakuwa halali kisheria. Marekani, Uingereza na Ufaransa ziliishambulia Syria kwa makombora tarehe 14 Aprili, kwa madai kwamba zilikuwa zikiiadhibu serikali ya Rais Bashar al-Assad, ziliyemshutumu kutumia gesi ya sumu kuwashambulia raia katika mji wa Douma.

''Matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya nchi huru, kama hatua dhidi ya ukiukaji wa sheria na kanuni za kimataifa unaodaiwa kufanywa na nchi inayoshambuliwa, ni uvunjaji a sheria ya kimataifa inayozuia matumizi ya ghasia,'' imesema ripoti hiyo ya wataalamu wa kisheria wa Bunge la Ujerumani, Bundestag. Ripoti hiyo iliombwa na chama cha mrengo wa kushoto (Die-Linke) cha Ujerumani.

Azimio la Umoja wa Mataifa liko wazi

Wataalamu hao wa bunge walilinukuu azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1970, ambalo linatilia mkazo haja ya nchi, katika kuendeleza mahusiano mema ya kimataifa, kujizuia kutumia nguvu za kijeshi, za kisiasa, za kiuchumi au njia nyingine zozote za kushinikiza, dhidi ya uhuru wa nchi nyingine kisiasa, au kuingilia katika himaya yake ya kieneo.

UK Theresa May im Unterhaus
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May,alipigia debe mashambulizi dhidi ya SyriaPicha: picture alliance/AP Photo/PA

Hali kadhalika, Umoja wa Mataifa unapinga ulipaji kisasi wa kutumia nguvu za kijishi, kwa hoja kwamba hauambatani na malengo na maadili ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa.

Aidha, ripoti hiyo ya wataalamu hao wa Bunge la Ujerumani, wamesema sababu zilizotolewa na Uingereza kama msingi wa kujiunga na Ufaransa na Marekani katika kuishambulia Syria, hazina mashiko. Mashambulizi hayo hayakupata ridhaa ya Umoja wa Mataifa.

Serikali mjini London ilidai kwamba inakubalika kisheria  kufanya mashambulizi ya kijeshi ili kuepusha mateso dhidi ya raia. Hata hivyo, wataalamu hao wa Ujerumani walisema yapi maswali yasio na majibu, juu ya iwapo mashambulizi ya nchi hizo tatu za Magharibi yatazuia madhila mengine kwa raia wa Syria.

Msimamo wa Ujerumani

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili, picha zilijitokeza katika vyombo vya habari, zikionyesha watu wanaopata shida kupumua, huku wakitokwa na mapovu mdomoni. Nchi za Magharibi ziliishutu serikali ya Rais Bashar al-Assad kufanya mashambulizi ya gesi ya sumu dhidi ya watu hao, madai ambayo Syria na washirika wake, Urusi na Iran waliyakanusha kwa nguvu.

Syrien Mutmaßlicher Giftgasangriff in Duma
Picha za watoto wanaoteseka kwa kile kinachodhaniwa kuwa shambulizi la gesi ya sumu kiliishitua duniaPicha: Reuters/White Helmets

Ingawa Ujerumani haikushiriki katika mashambulizi ya Aprili 14, Kansela Angela Merkel alisema mashambulizi hayo yalikuwa halali, na kwamba yalihitajika.

Wabunge wa chama cha Die-Linke, Heike Hänsel na Alexander Neu wamesema ripoti hii ya wataalamu wa masuala ya sheria za kimataifa wa Bunge la Ujerumani ni pigo kwa serikali ya Kansela Merkel, naye msemaji wa Chama cha Kijani kuhusu masuala ya kimataifa, Omid Nouripour, ameitaka serikali ya Berlin kukiri hadharani kwamba ilisaidia ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Lakini Roderich Kiesewetter, msemaji wa muungano wa vyama vya kihafidhina unaoongozwa na Kansela Angela Merkel ametetea msimamo wa serikali, akisema ulikuwa wa busara, kwa sababu wakati mwingine inakuwa sahihi kutilia maanani hali halisi kisiasa, katika kuzuia ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,dw

Mhariri:       Isaac Gamba