1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi Gaza yasitishwa kwa masaa 72

5 Agosti 2014

Israel inasema imeondowa wanajeshi wake wote wa ardhini kutoka Gaza baada ya kukamilisha operesheni yake iliyoanza katikati ya mwezi uliopita, huku muda wa usitishaji mapigano kwa muda wa siku tatu ukianza.

https://p.dw.com/p/1Coxc
Wanajeshi wa Israel wakiondoka kutoka Ukanda wa Gaza usiku wa tarehe 5 Agosti 2014.
Wanajeshi wa Israel wakiondoka kutoka Ukanda wa Gaza usiku wa tarehe 5 Agosti 2014.Picha: GIL COHEN MAGEN/AFP/Getty Images

Msemaji wa jeshi la Israel, Jenerali Moti Almoz, amekiambia kituo cha redio ya jeshi hilo asubuhi ya leo kwamba kulikuwa na wanajeshi kadhaa ndani ya Gaza, lakini kwa sasa wote wameondoka.

Mashahidi wanasema wanajeshi hao wa ardhini walianza kuondoka alfajiri ya leo, muda mchache kabla ya kuanza kwa masaa 72 ya ya kusitisha mapigano ambao ulianza saa 2 asubuhi kwa majira ya Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, Luteni Kanali Peter Lerner wa jeshi la Israel, amesema wanajeshi watawekwa kwenye maeneo ya kujilinda nje ya Gaza, na kwamba watajibu endapo watashambuliwa.

Kwa upande mwengine, ripoti zinasema usiku wa kuamkia leo, maroketi kutoka upande wa Gaza yaliangukia Israel, katika kile Hamas ilichosema ni kulipiza kisasi "mauaji ya maangamizi". Milio ya hadhari ilisikika kaskazini mwa mji wa Jerusalem, lakini hakuna taarifa yoyote ya watu waliouawa ama kujeruhiwa.

Roketi moja liliangukia karibu na nyumba moja mjini Bait-Lahm kwenye Ukingo wa Magharibi. Mkaazi mmoja wa nyumba hiyo, Elias Jubran, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba walisikia mshindo mkubwa usiku wa kuamkia leo, ambapo madirisha na milango ya nyumba kadhaa za eneo hilo ilivunjika, ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kuuawa.

Waziri ajiuzulu Uingereza

Kwengineko, nchini Uingereza, waziri mmoja kwenye serikali ya Waziri Mkuu David Cameron, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake akipinga sera ya nchi yake kuelekea Gaza. Waziri huyo, Sayeeda Warsi, anayeshikilia wadhifa wa juu kwenye wizara ya mambo ya nje na pia ni waziri wa imani na jamii, ametuma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter unaosomeka: "Kwa masikitiko makubwa, asubuhi hii nimemuandikia Waziri Mkuu na kuwasilisha kwake barua yangu ya kujiuzulu. Siwezi tena kuunga mkono sera ya serikali juu ya Gaza." Bado haijaeleweka ikiwa amejiudhulu nyadhifa zake zote mbili.

Wananchi wa Misri wakiandamana mjini Cairo kuwaunga mkono Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza katikati ya mwezi Machi 2014.
Wananchi wa Misri wakiandamana mjini Cairo kuwaunga mkono Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza katikati ya mwezi Machi 2014.Picha: MOHAMMED ABED/AFP/Getty Images

Kufikia sasa, mashambulizi haya ya takribani mwezi mmoja dhidi ya Gaza yamesababisha vifo vya Wapalestina 1,834 na huku Israel ikipoteza wanajeshi 64 na raia watatu.

Mbali na hasara hiyo ya maisha ya watu, pande zote mbili zimehasirika sana kiuchumi. Gaza inakabiliwa na ujenzi mpya wa makaazi na miundo mbinu utakaogharimu dola bilioni 6, huku Israel ikipoteza mamilioni ya dola kwenye sekta za utalii na viwanda.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo