1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi makubwa yafanyika dhidi ya mji wa Sirte

7 Oktoba 2011

Wapiganaji walio tiifu kwa utawala wa mpito nchini Libya leo wameanzisha mashambulizi makubwa ya silaha nzito na mizinga katikati ya Sirte mji alikozaliwa kiongozi wa nchi hiyo aliepinduliwa madarakani Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/Rpcn
Wapiganaji wa Kimapinduzi wakiwa na maguruneti yanayovurumishwa na maroketi huko Sirte, Libya.
Wapiganaji wa Kimapinduzi wakiwa na maguruneti yanayovurumishwa na maroketi huko Sirte, Libya.Picha: dapd

Mashambulizi hayo yanakuja wakati Gaddafi akitoa wito kwa wananchi wa Libya kujitokeza kwa mamilioni kupinga watawala wapya wa nchi hiyo huku vikosi vyake vikijibu mapigo katika mji wa Sirte uliozingirwa.

Mashambulizi yanayoendelea hivi sasa yanawalenga vichwa ngumu walio tiifu kwa Gaddafi ambao wamejichimbia ndani ya mji huo wa mwambao wa Sirte ambao mara kadhaa umeepuka majaribio ya kutekwa na wapiganaji dhidi ya Gaddafi katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.

Kituo cha televisheni cha Al Jazeera kimewakariri makamanda wanaompinga Gaddafi wakisema kwamba wanaamini maafisa waandamizi wa utawala wa zamani akiwemo al - Moatessam mtoto wa kiume wa Gaddafi wanajificha ndani ya mji huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya al Jazeera silaha nzito na mabomu yanatumika katika mashambulizi hayo mapya dhidi ya vikosi vya Gaddafi.

Msafara wa wapiganaji wa utawala mpya wakielekea mji wa Bani Walid.
Msafara wa wapiganaji wa utawala mpya wakielekea mji wa Bani Walid.Picha: dapd

Sirte na Bani Walid mji wa jangwani ulioko kama kilomita 170 kusini mashariki mwa Tripoli ni ngome mbili za mwisho za Gaddafi. Hapo jana wapiganaji wa Baraza la Mpito la Taifa walizuia mashambulizi ya vikosi vya Gaddafi na kuweza kusonga mbele kwa miguu kati ya majumba licha ya kukabiliwa na mashambulizi ya maroketi na risasi kutoka kwa wadunguaji mjini Sirte.

Wanajeshi zaidi wa Baraza la Taifa la Mpito pia wanapelekwa katika mji wa Bani Walid kwa shambulio jengine dhidi ya vikosi vya Gaddafi vinavyouhami vikali mji huo.Kwa mujibu wa Mussa Ali Yunes kamanda wa kikosi cha Jado shambulio dhidi ya mji huo linaweza kufanyika katika kipindi cha siku mbili na kwamba juhudi zinafanyika kuishawishi asilimia 10 ya wakaazi wa mji huo kuondoka kabla ya kufanyika kwa shambulio hilo baada ya kuzingirwa kwa mwezi mmoja. Amesema kuna silaha nyingi katika mji huo wa Bani Walid, silaha za teknolojia ya hali ya juu zikitokea Urusi hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Yunes mtoto wa kiume wa Gaddafi, Seif al Islam yuko Bani Walid na yumkini hata Gaddafi mwenyewe ambaye hadi hivi sasa hajulikani alipo ingawa inaaminika kwamba bado yuko nchini Libya.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen.Picha: dapd

Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wamefikia muafaka juu ya masharti ya kukomesha mashambulizi yao ya anga nchini Libya kwa kuahidi kwamba wataendelea kufanya mashambulizi hayo ya mabomu hadi hapo vikosi vya Gaddafi vitakapoacha kuwashambulia raia na utawala mpya utakapoweza kuhakikisha usalama nchini kote.

Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo ya NATO Anders Fogh Rasmussen amesema kwamba ni jambo lililo wazi kuwa vikosi vya Gaddafi vinapigana bure kwani tayari vimeshindwa.Amesema wameazimia kuendeleza operesheni yao kwa kadri vitisho vitakapoendelea kuwepo nchini Libya.

Kwa upande mwengine Kanali Muammar Gaddafi ametoa wito kuwataka wananchi wajitokeze kwa mamilioni kupinga watawala wapya wa nchi hiyo. Katika ujumbe wa sauti uliotangazwa hapo jana na kituo cha televisheni cha Arrai kilichoko Syria, Gaddafi amewataka wananchi wasihofu kwa kuwa wao ndio wananchi na ndio wenye nchi hiyo.

Kutekwa kwa mji wa Sirte kutaongeza morali ya watawala wapya wa Libya ambao wamechelewesha kutangaza serikali mpya hadi hapo Libya nzima itakapokuwa imekombolewa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri: Josephat Charo