1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya anga ya Syria na Urusi yaua raia 100

Sylvia Mwehozi
21 Februari 2018

Mashambulizi ya angani ya Syria na Urusi katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Ghouta mashariki yamewaua raia zaidi ya 100 kwa siku ya pili mfululizo na kusababisha hospitali nyingine kufungwa .

https://p.dw.com/p/2t2Bh
Syrien Angriff auf Ost-Ghouta
Picha: AFP/Getty Images/A. Almohibany

Katika mwendelezo wa vita vigumu villiyochukua miaka saba ya Syria, nchi hiyo imewatuma wapiganaji wanaoiunga mkono serikali katika mkoa wa Kaskazini wa Afrin, ambako walikutana na mashambulizi ya vikosi vya jeshi la Uturuki vinavyofanya operesheni katika mkoa huo unoadhibitiwa na Wakurdi.

Nje kidogo ya Damascus, mashambulizi ya angani, maroketi na risasi za moto vimekuwa vikisika eneo la Ghouta mashariki katika maandalizi ya serikali kufanya mashambulizi ya ardhini. Angalau raia 250 wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi hayo siku ya Jumapili, wengi wao ni watoto kwa mujibu wa taarifa ya shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria.

Syrien Angriff auf Ost-Ghouta
Mtoto akipita katika jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya anga huko GhoutaPicha: picture alliance/abaca/A. Al Bushy

Mashambulizi ya Jumanne yamewaua raia 106, wakiwemo watoto 19, limesema shirika hilo. Ilikuwa ni siku ya pili mfululizo vifo vya raia kupindukia 100 baada ya wengine 127 kuuawa siku ya jumatatu Ghouta mashariki. Hospitali ya Arbin ilishambuliwa mara mbili na kushindwa kuendelea na utoaji huduma kwa mujibu wa Mosua Naffa mkurugenzi wa kikanda  nchini Jordan wa taasisi ya huduma za afya ya Syria na Marekani SAMS, ambayo inasaidia hospitali hiyo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "ana wasiwasi sana na vurugu zinazoongezeka Ghouta mashariki na athari za kushangaza kwa raia." Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Heather Nauert amekosoa "mbinu za kuzingirwa na njaa" za utawala wa Assad na kusema "ukomeshwaji wa vurugu ni lazima uanze sasa".

"Mbinu za utawala wa Assad za kuzingirwa na njaa zinatengeneza janga la kiutu, au niseme linaongeza mgogoro wa kibinadamu kule. Hofu ya Aleppo mashariki inajirudia Ghouta mashariki , kwa mauaji yanayoendelea ya wananchi waliokwama na uhaba wa watendaji wa misaada ya kiutu, " alisema Nauert.

Syrien Konflikt in Afrin
Msafara wa wanajeshi anaounga mkono serikali ya Syria wakiwasili AfrinPicha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Ghouta mashariki ina wakazi karibu 400,000 wanaoishi chini ya mzingiro wa serikali, wakiwa na upatikanaji kidogo wa chakula au huduma za afya. Umoja wa Mataifa umesema hospitali sita zimeshambuliwa katika mkoa huo ndani ya masaa 48, ikiwa ni nyongeza ya hospitali nyingine huko Afrin.

Afrin kwenyewe, vikosi vinavyounga mkono serikali vimeingia mkoani humo kuwasaidia wanamgambo wa kikurdi kukabiliana na mashambulizi ya Uturuki, na kuongeza wasiwasi wa kupanuka kwa mgogoro. Muda mchache baada ya ujumbe wa wanamgambo waliokuwa wakipeperusha bendera kuingia Afrin, vyombo vya habari vya umma vya Syria vimeripoti kwamba Uturuki iliwalenga kwa mabomu.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ameuita ujumbe huo kuwa ni "magaidi" yanayofanya kazi peke yake, na kwamba mabomu ya jeshi lake yamefanikiwa kuwarejesha nyuma, ingawa wanamgambo wa kikurdi wamekana madai hayo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Caro Robi