1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Mashariki ya Kati

Admin.WagnerD5 Oktoba 2010

Kila upande unaohusika na mazungumzo ya Mashariki ya Kati unachukua jitihada zake zenyewe kuona kwamba hatimaye mazungumzo yanakwamuka na amani inafikiwa, lakini misimamo mikali kutoka kila upande inayahatarisha.

https://p.dw.com/p/PVlg
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas (kushoto), Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Barack Obama wa Marekani
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas (kushoto), Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP/DW

Leo hii Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, anakutana na Rais wa Misri, Husni Mubarak, mjini Cairo kujadiliana juu ya kukwama kwa mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Wakati huo huo, Netanyahu naye anakutana na timu yake ya mawaziri saba wa ngazi za juu katika serikali yake, mjini Jerusalem, kujadiliana kipi watoe na kipi wapokee kwenye mazungumzo haya yaliyokwama. Wote wawili, Abbas na Netanyahu, wanajitayarisha kwa maazimio ya Mkutano wa Nchi za Kiarabu unaoanza Ijumaa hii nchini Libya, ambao wengi wanauangalia kama muamuzi wa mwisho wa hatima ya mazungumzo haya.

Wakati anakutana na mawaziri wake, matarajio ya Netanyahu ni kwamba mkutano huu wa nchi za Kiarabu, utaweza kumshawishi Abbas kurudi kwenye meza ya mazungumzo, lakini hofu yake ni kwamba sharti litakuwa ni lile lile la Palestina, yaani Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi kwa maslahi ya kuendeleza mazungumzo.

Ingawa ajenda za mkutano wa Netanyahu na mawaziri wake hazijawekwa wazi, lakini vyombo vya habari vya Israel vinasema kwamba uwezekano ni kuwa mjadala wao utatuwama kwenye hoja na haja ya kuongeza muda wa usitishwaji wa ujenzi chini ya kivuli cha ahadi ya ulinzi kutoka Marekani.

Katika taarifa ambazo maafisa wa Israel na Marekani hawataki kuziweka wazi, msaidizi mkuu wa Rais Barack Obama kwa Mashariki ya Kati, Dennnis Ross, anaripotiwa kukubaliana na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak, mambo kadhaa muhimu ambayo Israel ilikuwa ikiyataka muda mrefu kutoka Marekani.

Miongoni mwa mambo hayo ni hakikisho kwamba Marekani itaunga mkono hatua ya Israel kuweka vituo vya kijeshi katika eneo lake na mpaka wa dola inayotarajiwa ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi na mpaka wa Jordan ili kuzuia uingizaji wa silaha katika ardhi ya Palestina.

Jengine ni ahadi ya Washington kwamba italipigia kura ya turufu azimio lolote lile dhidi ya Israel kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakalokuja ndani ya mwaka mmoja ujao na pia Marekani itatoa msaada zaidi wa silaha, yakiwemo makombora, ndege za kivita na satalaiti.

Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo haya, Seneta George Mitchell, anaripotiwa kwamba amekuwa akiwatembelea viongozi mbalimbali wa nchi za Kiarabu, ili kuwashawishi wamruhusu Abbas kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Na ingawa hadi sasa hakuna kiongozi wa nchi ya Kiarabu aliyetoa tamko la moja kwa moja, tayari uongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, na wa kundi la Fatah la Rais Abbas mwenyewe, wameshamtaka Abbas asirudi kwenye mazungumzo haya, hadi hapo Israel itakapositisha ujenzi wa makaazi ya walowezi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mhariri: Charo, Josephat