1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashariki ya Kati na vurugu za kisiasa Ujerumani Magazetini

Oumilkheir Hamidou
13 Februari 2018

Sera ya rais wa Marekani Donald Trump kuelekea Mashariki ya kati na vurugu zinazovikumba vyama vikuu vya kisiasa humu nchini ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2saHE
USA Rob Porter zurückgetreten
Picha: Reuters/J. Ernst

Tunaanzia Mashariki ya kati  ambako gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linahisi sera ya rais wa Marekani haitosaidia kumaliza mvutano. Gazeti linaendelea kuandika: "Marekani imepoteza ushawishi wake katika eneo hilo, kinyume na Urusi ambayo ushawishi wake unazidi kupata nguvu. Washington haitosheki pekee na makadirio. Sokomoko pia katika hali yenyewe nchini Israel:Trump amemteuwa mfuasi wa siasa kali kuwa mwakilishi wa Marekani nchini humo na anataka kuuhamishia ubalozi wa nchi yake mjini Jerusalem. Kwamba yote hayo yanautia hatarini utaratibu wa amani ya Mashariki ya Kati, si siri tena na kila mmoja analizungumzia katika ikulu ya Marekani-White House. Kwa mara ya kwanza rais wa Marekani anajitenga na sera ya Israel ya ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi katika maeneo inayoyakalia ya wapalastina. Kidogo kidogo, viongozi mjini Washington wanaanza kutambua hali ya mambo inaanza kwenda kombo Mashariki ya kati. Hapatapita muda, kauli mbiu mjini Washington"America First" itabainika kuwa si chochote si lolote: ni "kauli iliyotolewa bila ya kufikiri na ya hatari"

Vurugu zavikaba vyama vikuu vya CDU na SPD

 Zahma inapiga ndani ya vyama vikuu vya kisiasa nchini Ujerumani tangu makubaliano ya kuunda serikali kuu ya muungano yalipofikiwa kati ya vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU/CSU na SPD. CDU wanalalamika SPD wamepatiwa wizara muhimu katika serikali inayokuja. Vijana wa vyama vyote viwili  wanalalamika pia na kudai wakabidhiwe na wao pia hatamu za uongozi. Katika wakati ambapo SPD wanapanga kuwauliza wanachama wao maoni yao kama wanaunga mkono au la makubaliano yaliyofikiwa, CDU watatamka mkutano mkuu utakapoitishwa february 26 inayokuja. Gazeti la "Rhein Zeitung" linaandika: "Merkel anabidi abainishe kwamba chama cha CDU kina wenyewe. Ujumbe huo mwenyekiti wa CDU anauhitaji kwa kila hali, mamoja wanachama wa SPD wataunga mkono au watapinga makubaliano ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu-GroKo. Pindi wanachama wa SPD wakipinga serikali ya tatu ya muungano wa vyama vikuu, Merkel hatoweza kuepuka kukifanyia mageuzi chama chake cha CDU, ikiwa binafsi  hatopeperushwa na zahma iliyoko."

Vijana wanadai wawajibishwe

Gazeti la "Rhein-Necker Zeitung linamulika madai ya vijana matata wa vyama vyote vitatu vya CDU/CSU na SPD na kuandika: Akina Schulz, Gabriel, Nahles na Merkel wamejitakia wenyewe ghadhabu za vijana wao. Wamepuuza muongozo wa kidemokrasi unaosema fikira zinatokea mashinani na sio kinyume chake. Kwa Merkel kishindo kimesababishwa na kuachilia wizara ya fedha idhibitiwe na SPD, jambo ambalo vijana wa CDU hawakubaliani nalo. Upande wa SPD kigeugeu cha Schulz ndio chanzo cha kuudhika kwao-ingawa hapo watu wanabidi wakiri kwamba kuna waliowasaidia pia."

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/INlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef