1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya Haki za Binadamu nchini Ufaransa yakosoa ziara ya kiongozi wa Libya nchini humo.

Halima Nyanza10 Desemba 2007

Mashirika ya Haki za Binadamu nchini Ufaransa yamekosoa ziara ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi nchini humo, ambapo leo anaanza ziara rasmi nchini humo kwa shutuma kwamba ni mvunjifu wa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/CZoE
Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi ambaye ziara yake nchini Ufaransa inashutumiwa na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo.Picha: AP

Ziara hiyo imeelezewa kuwa itaiwezesha Ufaransa kusaini mikataba mizito na Libya

Akiwa ziarani nchini Ufaransa kiongozi huyo wa Libya Muammar Gadhafi anampango wa kusaini mkataba wa kununua mtambo kudhibiti nyuklia na ndege aina ya Airbus.

Awali katika mahojiano na gazeti moja, mtoto wa kiongozi huyo wa Libya Seif Al -Islam ameeleza kuwa Libya itanunua ndege aina ya Airbus yenye thamani ya zadi ya euros bilioni 3 pamoja na kinu cha kudhibiti nyuklia na pia zana za kijeshi.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alitoa mwaliko huo kwa kiongozi huyo wa Libya, baada ya Libya mwezi Julai mwaka huu, kuwaachia huru madaktari wa kigeni wapatao sita waliokuwa wakishtakiwa kwa kuwaambukiza watoto wa Libya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Kanali Gadhafi kutembelea Paris, tangu kupita kipindi cha miaka 34.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Bernard Kouchner amesema Ufaransa ni lazima iwe mwangalifu na haki za binadamu na wakati huo huo pia kulinda maslahi yake ya kiuchumi.

Ameelezea kuwa Libya imebadilika na kwamba mabadiliko hayo mapya ndio yaliyowavutia mpaka kukawepo kwa ziara ya kanali Gadafi.

Hata hivyo akizungumzia zaidi kuhusiana na demokrasia nchini Libya, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa alikuwa na haya ya kusema

’’Demkrasia nchini Libya ni suala la mabishano, lazima uwe mkweli, ni rahisi kukaa ghorofani na kueleza juu ya wapita njia, lakini ni vigumu kuyaeleza na kuyapima yote mawili kwa wakati mmoja’’.

Kwa upande wao, wapinzani nchini Ufaransa, wamemuelezea Rais Sarkozy, kwamba ametanguliza biashara zaidi kabla ya haki kufuatia mwalio huo alioutoa kwa kiongozi wa Libya.

Rais Nicolas Sarkozy anaweka rekodi kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi za magharibi kwa kumkaribisha nchini mwake kanal Gadhafi tangu kiongozi huyo wa Libya alipokorofishana na nchi za magharibi kwenye miaka ya 80.

Ni mara chache kwa kiongozi huyo wa Libya kualikwa na nchi za magharibi, lakini ushirikiano na nchi hiyo na nchi za magharibi umeongezeka tangu nchi hiyo ilipokubali kulipa fidia kwa familia za wafiwa katika shambulio la ndege ya Pan Am lililotokea katika anga ya Scotland mwaka 1988.

Kufuatia tukio hilo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea vikwazo vya kiuchumi Libya, nchi ambayo pia ilikuwa ikituhumiwa kufadhili vikundi vya kigaidi.

Lakini hata hivyo, vikwazo hivyo viliondolewa baada ya nchi hiyo kukiri kuhusika na shambulio hilo na kuwa tayari kulipa fidia kwa familia za wafiwa wa abiria waliokuwemo katika ndege zilizolipuliwa.
Baadaye Libya pia ilitangaza uamuzi wake wa kuachana na silaha za maangamizi, hali ambayo imeifanya nchi hiyo kupata nafasi ya kurejesha upya uhusiano wake na jumuiya za kimataifa.