1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya Misaada yapeleka misaada katika mji unaoshikiliwa na waasi, Mashariki ya Congo.

Nyanza, Halima3 Novemba 2008

Msafara wa kwanza wa misaada wa umoja wa mataifa, leo umeanza safari yake kuelekea katika mji unaoshikiliwa na waasi, kwa ajili ya kuwasaidia watu wasio na makazi, kutokana na mapigano mashariki ya Congo.

https://p.dw.com/p/FmXF
Maelfu ya watu wasio na makazi, kutoka na mapigano, mashariki ya Congo, sasa wanahitaji msaada wa chakula ili waweze kuishi.Picha: AP

Walinzi wa amani wa Umoja wa mataifa wanasindikiza mlolongo wa misafara ya misaada ya binadamu katika mji huo wa Goma, ulioko katika mkoa wa kivu kaskazini baada ya majeshi ya serikali na waasi kuhakikisha usalama wa misafara hiyo.

Utakua ni msaada wa kwanza katika eneo hilo, kufuatia ule wa awali kusitishwa, kwa sababu ya kupamba moto kwa mapigano wiki moja iliopita .

Waasi kwa upande wao, walikubali kuheshimu usimamishaji mapigano tangu siku tatu zilizopita. Zaidi ya watu milioni 1 na laki sita wametawanyika ndani ya eneo hilo wakikumbwa na janga kubwa kuwahi kushuhudiwa, huku shida iliopo ni kwamba mashirika ya misaada yanashindwa kuwafikia mahala walipo. Hali hiyo inatokana na kambi za wakimbizi kuvunjwa na waasi wa Nkunda na kuwataka wakimbizi hao kurudi katika majumba na maeneo yao. Wengi wanahofia wakisema hakuna usalama.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David Miliband na mwenzake wa Ufaransa Bernard Kouchner walikuweko Tanzania jana, kuzungumza na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais Jakaya Kikwete juu ya hali ya mambo ilivyo baada ya kuwa na mazungumzo mjini Kinshasa na Rais Kabila wa Congo na mjini Kigali na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Waziri Miliband alizitaka pande zote mbili, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Rwanda ziheshimu makubaliano ya amani yaliofikiwa awali mjini Nairobi.

Marais Kagame na Kabila wamekubaliana, kufuatia mazungumzo na ujumbe huo wa Umoja wa Ulaya, kukutana mjini Nairobi kuzungumzia jinsi ya kuutatua mzozo wa mashariki mwa Kongo.

Rwanda inashutumiwa na Congo kumsaidia Nkunda, wakati Rwanda inakanusha na kudai Congo imeshindwa kuwapokonya silaha waasi wa Rwanda wa FDLR, ambao ni pamoja na wanajeshi wa zamani wa nchi hiyo, waliohusika na mauaji ya kimbari 1994.

Wakati huo huo Jenerali Nkunda ametoa tamko leo akisema anataka kukutana ana kwa ana na serikali ya Congo, la si hivyo atahakikisha anaiondoa madarakani. Kadhalika alidai kwamba majeshi yake yanayouzingira mji wa Goma, sasa yameshajiingiza karibu na uwanja wa ndege wa mji huo.

Lakini tayari, serikali ya Congo imeshajibu ikisema haiko tayari hata kidogo, kukutana na Jenerali huyo muasi.

Kwa wakati huu bado hali ni tete ingawa usimamishaji mapigano ungali ukiheshimiwa.