1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masuala mengi kuhusu ugaidi wa aina mpya Ujerumani

16 Novemba 2011

Je, maafisa wa idara ya kuhifadhi katiba ya Ujerumani, walikuwa na dhima gani katika mauaji kadhaa yanayoshukiwa kuhusika na ugaidi wa itikadi kali za mrengo wa kulia?

https://p.dw.com/p/Rwku
Der parlamentarische Geschäftsführer der SPD-Bundestagsfraktion, Thomas Oppermann, spricht am Mittwoch (23.02.2011) im Deutschen Bundestag in Berlin. Zuvor hatte Bundesverteidigungsminister zu Guttenberg (CSU) Stellung zu den gegen ihn erhobenen Plagiatsvorwürfen Stellung genommen. Der Politiker, der wegen Plagiatsvorwürfe im Rahmen seiner Doktorarbeit, in die Schlagzeilen geraten ist, nahm an einer Aktuellen Stunde mit Regierungsbefragung und anschließender Fragestunde zum Fall Guttenberg teil. Foto: Wolfgang Kumm dpa/lbn +++(c) dpa - Bildfunk+++
Thomas Oppermann, mwenyekiti wa kamati ya bunge PKGPicha: picture-alliance/dpa

Hilo ni suala ambalo hivi sasa pia linashughulikiwa na kamati ya bunge inayodhibiti idara za upelelezi - PKG- iliyokutana hapo jana mjini Berlin.

Katika katiba ya Ujerumani, kipengele cha 45 kinasema, kamati ya kudhibiti shughuli za idara tofauti za upelelezi nchini Ujerumani, inaundwa na bunge la taifa. Serikali kuu inawajibika kuiarifu kamati hiyo kuhusu shughuli za kawaida za idara za upelelezi na juu ya hatua zilizo na umuhimu maalum.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge, Thomas Oppermann amesema, kikao maalum kiliitishwa Novemba 23 baada ya kupata habari mpya kuhusu mauaji yaliyotokea kati ya mwaka 2000 na 2007 ambayo yanashukiwa kuhusika na ugaidi wa itikadi kali za mrengo wa kulia.

Wajumbe 11 wa kamati hiyo ya PKG huchaguliwa kutoka bunge la taifa na wao wanawajibika kuweka siri. Kwa hivyo, ni nadra sana kwa wajumbe hao kutamka cho chote hadaharani. Baada ya kikao hicho maalum, Opperman wa chama cha SPD amezungumzia kile alichokiita "uhalifu wa kukirihisha kabisa" nchini Ujerumani tangu miaka 60 iliyopita. Akaongezea:

"Naona aibu kuwa taifa letu halikuweza kutoa kinga dhidi ya magaidi hao, kwa wale waliouawa na wengine waliojeruhiwa. Kwa hivyo, ninaamini pia kuwa taifa hili la kidemokrasia linapaswa kuwaomboleza waliouawa. "

Oppermann na wenzake wengine katika kamati ya PKG wanashinikiza kuelezwa haraka, kwanini washukiwa hao waliweza kufanya mauaji hayo bila ya shida yo yote, licha ya maafisa wa idara ya kuhifadhi katiba kuwafahamu watu hao tangu miaka ya tisini. Ionekanavyo, sababu kuu ni uhaba wa mawasiliano kati ya maafisa wa kuhifadhi katiba majimboni Hesse na Thuringia na ofisi kuu ya kulinda katiba (BfV).

Ukubwa wa ugaidi uliofanywa na wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia, umetoa sura mpya na mara nyingine tena, masuala yanaulizwa kuhusu dhima ya chama chenye sera kali za mrengo wa kulia NPD, kinachowakilishwa katika mabunge ya majimbo mawili. Mwaka 2003, jaribio la kukipiga marufuku chama hicho halikufanikiwa katika mahakama ya katiba. Sababu ni kwamba katika chama cha NPD kulikuwepo majasusi wengi wa idara ya kuhifadhi katiba. Hata hivi sasa bado wapo.

Mwenyekiti wa PKG, Oppermann alie pia kiongozi wa wabunge wa chama cha upinzani cha SPD, anatumaini kuwa jaribio la pili hatimae litafanikiwa kukipiga marufuku chama cha NPD.

Mwandishi: Fürstenau, Marcel/ZPR

Tafsiri:Martin,Prema

Mhariri: M.Abdul-Rahman