1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa matatu ya Ghuba yawashauri raia wake kuondoka Iraq.

Tatu Karema
4 Oktoba 2019

Mataifa matatu ya Ghuba yamewashauri raia wake kutosafiri kwenda Iraq na wale waliomo nchini humo kuondoka. Wito huo uliotolewa leo na Kuwait, Qatar na Bahrain unajiri baada ya siku tatu za maandamano nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/3QkP5
Irak Anti-Regierungsproteste | Ausschreitungen & Gewalt in Bagdad
Picha: Reuters/T. al-Sudani

Shirika la habari nchini Kuwait (Kuna) limemtaja afisa mmoja mkuu wa wizara ya mambo ya nje akiwahimiza raia wa Kuwait kuepuka kusafiri kwenda Iraq kutokana na maandamano hayo na wale walioko nchini humo kuondoka mara moja na kuepuka maeneo yanapoandaliwa maandamano.

Wizara ya mambo ya nje ya Qatar pia imetoa ombi kama hilo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Bahrain nayo imetoa wito kwa raia wake kutosafiri kwenda Iraq na kuwahimiza wale waliomo nchini humo pia kuondoka mara moja.

Haya yanajiri huku vikosi vya usalama vya Iraq vikiwafyetulia tena risasi waandamanaji waliokusanyika katika eneo la Kati mwa Baghdad na kumjeruhi mtu mmoja katika siku ya nne ya maandamano hayo ya ghasia dhidi ya serikali. Waandamanaji hao walikuwa wamekusanyika katika barabara nyuma ya eneo la Tayaran hii leo wakiimba nyimbo wakati vikosi vya usalama vilipowafyetulia risasi. Kijana mmoja alilengwa mguuni.

Hili ni tukio la kwanza la ufyetuaji wa risasi baada ya mhubiri mmoja mkuu wa dhehebu la Kishia nchini Iraq Grand Ayatollah Ali al-Sistani kutoa wito mapema leo kwa pande zote mbili kusitisha ghasia ambazo zimekumba nchi hiyo tangu siku ya Jumanne.

Matamshi ya mhubiri huyo ni ya kwanza tangu maandamano dhidi ya serikali kuanza na ameishtumu serikali pamoja na viongozi wa makundi mawili makubwa ya ubunge na kusema wameshindwa kutimiza ahadi zao kwa watu wa nchi hiyo. Al-Sistani ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuchukuwa hatua zinazowezekana katika kukabiliana na ufisadi na kwa upande wa serikali kutekeleza jukumu lake la kumaliza mateso kwa watu.

Tangu siku ya Jumanne, vikosi vya usalama vimekuwa vikifyetua risasi moto na gesi za kutoa machozi kila siku kuwatawanya waandamanaji wanaotaka ajira, huduma zilizoimarishwa na kutamatishwa kwa ufisadi. Waziri mkuu wa Iraq, Adel Abdul- Mahdi anayetoka eneo la Nasiriyah, ametoa wito wa utulivu na kusema anashughulika kutekeleza matakwa ya waandamanaji yanayostahili na kuongeza kuwa hakuna suluhu la kimiujiza kwa matatizo ya Iraq. Hotuba ya waziri huyo mkuu ilipeperushwa moja kwa moja kupitia runinga mapema hii leo. Vikosi vya usalama vya Iraq vimeweka amri ya kutotoka nje mjini Baghdad tangu siku ya Jumanne .