1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini na Somalia ni mataifa fisadi zaidi ulimwenguni

23 Februari 2018

Mabadiliko katika mataifa ya Rwanda na Cape Verde yanaonesha kuwa ufisadi unaweza kudhibitiwa pakiwa na juhudi na nia njema. Matunda ya vita vya muda mrefu katika mataifa kama vile Cote d' Ivore na Senegal yanaonekana.

https://p.dw.com/p/2tCqn
East African Community Gipfel Tansania Arusha
Picha: picture-alliance/dpa/Xinhua

Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi, Transparency International limesema kuwa mataifa yaliyo chini ya jangwa la sahara barani Afrika yanaongoza kwa ufisadi ulimwenguni. Hali hiyo inaelezwa kutokea baada ya mataifa mengi kukokota juhudi zao zinapolikabili suala la ufisadi. Kwenye ripoti yake ya mwaka 2017 shirika hilo limesema kuwa ufichuzi wao unaibua maelezo ya wasiwasi. Kauli mbiu ya Umoja wa Afrika ya mwaka huu ni, Kushinda vita dhidi ya Ufisadi, Njia Endelevu ya kubadilisha Afrika.

Ripoti hiyo inaonesha mabadiliko na kutoa matumaini kwa mataifa ya Afrika. Mabadiliko katika mataifa ya Rwanda na Cape Verde yanaonesha kuwa ufisadi unaweza kudhibitiwa pakiwa na juhudi na nia njema. Matunda ya vita vya muda mrefu katika mataifa kama vile Cote d' Ivore na Senegal yanaonekana.

Kwa upande mwingine kukabili ufisadi katika mataifa yaliyo chini ya orodha ya Shirika la Transparency International kunasalia kuwa kibarua kigumu kwa mfano katika mataifa ya Sudan Kusini na Somalia. Licha ya kuwa Afrika ina mataifa mengi ambayo yanakabiliwa na ufisadi, kuna baadhi ya mataifa yanayopiga hatua kama vile Botswana, Ushelisheli, Cape Verde, Rwanda na Namibia yakilinganishwa na mataifa kama vile Italia, Ugiriki na Hungary. Botswana na Ushelisheli yaliyo na alama 61 na 60 yamefanya vyema zaidi ya taifa kama vile Uhispania ambayo ina alama 57.   

Rwanda yavikabili vita dhidi ya ufisadi kwa ufanisi
Rwanda yavikabili vita dhidi ya ufisadi kwa ufanisiPicha: picture alliance/AP Photo/K. Said

Rwanda yafanya vyema katika vita dhidi ya Ufisadi Afrika Mashariki.

Katika kanda ya Afrika Mashariki Rwanda, inaongoza huku ikiwa katika nafasi ya 48, Tanzania ni ya pili lakini ulimwenguni ni ya 103, Kenya ni ya tatu lakini ya 143 ulimwenguni. Uganda ni ya nne ikiwa ya 151 ulimwenguni na Burundi inaratibiwa ya 157 ulimwenguni. Sudan Kusini na Somalia ndio mataifa fisadi zaidi ulimwenguni zikiratibiwa za 179 na 180 ulimwenguni mtawalia.

Shirika hilo lenye makao yake jijini Berlin linasema kuwa licha ya kuwa pana juhudi za kukabiliana na donda hilo ulimwenguni, kasi ya mataifa mengi ni mdogo.

Ripoti hiyo inaongeza kusema kuwa "kuvikabili vita dhidi ya ufisadi huchukua muda mrefu, miaka sita baadaye mataifa mengi hayajapiga hatua."

Ripoti hiyo imetolewa kutoka vyanzo 13, ikiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Ustawi ya Afrika na Kongamano la Uchumi Ulimwenguni na kufanya uamuzi kutokana na viwango vya rushwa, ugavi wa fedha za umma, matumizi ya afisi za umma kwa maslahi ya kibinafsi na masuala mengine ya ufisadi. Mataifa 180 yaliratibiwa kwenye utafiti huo.

Maeneo bora yalikuwa Ulaya Magharibi na wastani wa alama 66, huku eneo lililofanya vibaya zaidi likiwa ukanda wa mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa jangwa la sahara likiwa na wastani wa alama 32 lifuatwa kwa karibu na Asia ya Kati iliyokuwa na wastan wa alama 34.

Magharibi ya Ulaya yaripotiwa visa vichache vya ufisadi
Magharibi ya Ulaya yaripotiwa visa vichache vya ufisadiPicha: Colourbox/E. Wodicka

Ulaya Magharibi ina visa vichache vya ufisadi.

Kiwango cha wastani ulimwenguni ni alama 43. New Zealand na Denmark ziliongoza kwenye orodha hiyo zikiwa na alama 89 na 88 mtawalia, huku Somalia ikivuta mkia kwa alama tisa, kisha Sudan Kusini ikiwa na alama 12, Syria ikiwa na alama 14 na Afghanistan ikiwa na alama 15.

Uingereza ilitajwa kuwa moja ya mataifa yaliyoimarika kwa kipindi cha miaka sita na kuongeza alama zake kwa nane tangu mwaka 2012 na kufikia alama 82 na kuiweka juu ya Ujerumani kwa alama moja na kukabana koo na Uholanzi, Luxembourg na Canada. Marekani ilitoshana na Austria na Ubelgiji katika nafasi ya 16 kwa alama 75.

Shirika hilo limesema kuwa limekusanya takwimu kutoka kwa Kamati ya Kuwalinda wanahabari na kugundua kuwa wanahabari wamo hatarini kwenye mataifa fisadi.

Kwa miaka sita iliyopita, zaidi ya wanahabari 10 wameuawa katika mataifa yaliyo chini ya alama 45 na mmoja wa wanahabri kati ya watano alikuwa anafanya stori kuhusu ufisadi.

Mkurugenzi wa shirika la Kimaitaifa la Transparency International Patricia Moreira amesema kuwa kampeini zenye kuchafua jina, dhulma, ufisadi ni vyombo vinavyotumika na serikali katika mbinu za kunyamazisha juhudi za kukabiliana na ufisadi.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap, Afp, Transparency International/ https://www.transparency.org/news/feature/a_redefining_moment_for_africa

Mhariri: Josephat Charo