1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya iliyokuwa Soviet Union yaunga mkono Georgia.

13 Agosti 2008

Historia ya maumivu na kiwewe kutokana na kuwa katika udhibiti wa Urusi ya zamani na hofu iliyopo sasa dhidi ya Urusi ndio msingi wa uungaji huo mkono.

https://p.dw.com/p/EwiV

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa historia ya maumivu na kiwewe kutokana na kuwa katika udhibiti wa iliyokuwa Urusi ya zamani na hofu iliyopo sasa dhidi ya Urusi ndio mzizi wa uungwaji mkono mkubwa kwa Georgia unaotolewa na Poland, mataifa ya eneo la Baltic na Ukraine.

Katika hatua ambayo si ya kawaida jana viongozi wa iliyokuwa kambi ya kikomunist zamani , Poland, Lithuania, Latvia, Estonia na Ukraine walikwenda nchini Georgia kwa kile walichokieleza kuwa ni kuonyesha kuunga kwao mkono jimbo hilo la zamani la jamhuri ya kisovieti baada ya mashambulio yaliyofanywa na Urusi.

Ziara yetu ni ishara ya mshikamano wa mataifa yetu matano na taifa hili la Georgia, ambalo limekuwa muhanga wa uvamizi, rais wa Poalnd Lech Kaczynsnki amewaambia waandishi wa habari.

Kwa mara nyingine tena , Urusi imeonyesha sura yake halisi, amesema.

Siku ya Jumamosi , Poland na mataifa ya Baltic , yametoa taarifa ya pamoja kama mateka wa zamani wa umoja wa kisovieti yakitoa wito kwa umoja wa Ulaya na NATO kupinga sera za kibeberu za Urusi kuelekea Georgia.

Hofu dhidi ya Urusi ni kubwa, amesema Bartosz Cichocki, mtaalamu katika taasisi ya Poland ya masuala ya kimataifa. Mataifa haya bado yanakumbuka jinsi katika mwaka 1939 jeshi la kisovieti lilivyofunga mkataba na kuinyakua Poalnd na mataifa mengine ya Baltic. Na bado yanakumbuka uhuru wao kutoka Urusi, ambao umedumu kwa muda wa miongo mine, ameliambia shirika la habari la AFP.

Poland ambayo imejinasua kutoka udhibiti wa duru ya Urusi mwaka 1989, na mataifa ya Baltic , ambayo kama Georgia na Ukraine yalikuwa sehemu ya umoja wa kisovieti hadi uliposambaratika mwaka 1991, ni waungaji mkono wakubwa wa Georgia.

Katika mataifa ya Baltic na Ukraine , uhuru bado unaonekana kama wa wasi wasi na ambao si lazima kuwa , umejengeka katika hali ya kutodumu. Kwa hiyo iwapo hautalindwa kikweli, hautadumu, Cichocki amesema.

Poland na mataifa ya Baltic yanajiweka kidhati katika upande wa mataifa ya magharibi. Poland imejiunga na NATO mwaka 1999 na umoja wa Ulaya mwaka 2004, wakati mataifa matatu ya Baltic yaliingia yote katika mwaka 2004. Wanaiunga mkono Georgia na juhudi za Ukraine kupata kile wanachokiona kama ngao muhimu.Watu wanawasi wasi kuwa Urusi inaweza kuishambulia Lithuania kama ilivyo hivi sasa Georgia. Na unaona mawazo kama hayo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa amesema mtaalamu wa masuala ya sayansi ya kisiasa Kestutis Girnius.

►◄