1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoinukia kiuchumi yakutana Delhi

Saumu Ramadhani Yusuf29 Machi 2012

Kundi la nchi zinazoinukia kiuchumi duniani, BRICS, linakutana nchini India na kuweka azimio la kuzishinikiza nchi za maghiribi kuruhusu usawa kwenye taasisi za kuchumi duniani likiwemo Shirika la Fedha Duniani, IMF.

https://p.dw.com/p/14UJT
Kutoka Kushoto, rais wa Brazil Dilma Rousseff, rais wa Urusi Dmitry Medvedev, waziri mkuu wa India Manmohan Singh, rais wa China Hu Jintao na rais wa Afrika Kusini
Kutoka Kushoto, rais wa Brazil Dilma Rousseff, rais wa Urusi Dmitry Medvedev, waziri mkuu wa India Manmohan Singh, rais wa China Hu Jintao na rais wa Afrika KusiniPicha: AP

Katika azimio lao la kwanza la mkutano huo unaofanyika New Delhi nchini India, mataifa hayo ambayo ni Brazil, China, Afrika Kusini, Urusi na India yamepaza sauti zao kuhusu kasi ndogo ya mabadiliko ndani ya Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, na pia kutaka kuwepo kwa uwazi katika mchakato wa kumpata rais ajaye wa taasisi hiyo.

Wakiwa na matumaini ya kuleta mabadiliko ambayo yatawapa nguvu ya haki ya kupiga kura katika maamuzi mbalimbali ndani ya IMF, bado matumaini hayo yako mashakani kwani yanategemea pia uungwaji mkono wa Marekani.

Mashaka hayo yanazidi kuwa makubwa hasa linapokuja suala la mtafaruku wa kundi la G7 pamoja na kukosa nafasi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Brazil na India zimekuwa zikipigania kupata uwakilishi wa kudumu kwa muda mrefu sasa.

Wito wa kusitisha kuyumba kwa uchumi duniani

Tamko la azimio hilo limetoa wito kwa nchi zilizoendelea kuacha kutengeneza mianya ya kuyumba kwa uchumi wa dunia. Kauli hiyo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na mataifa yanaoendelea ambayo uchumi wake umeathirika na mtikisiko wa kuiuchumi ulioikumba dunia katika miaka ya hivi karibuni.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, nchi nchi pekee ya kiafrika katika kundi la BRICS
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, nchi nchi pekee ya kiafrika katika kundi la BRICSPicha: Reuters

Hata hivyo kundi hilo la BRICS hadi sasa bado halijaonyesha juhudi za wazi za kuunga mkono mgombea yoyote kati ya watatu wanaotarajiwa kuchukua nafasi ya urais wa Benki ya Dunia kutoka kwa Mmarekani Robert Zoellick.

Waziri wa Viwanda na Biashara wa India Fernando Pimentel aliliambia Shirika la Habari la Reuters siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo kuwa, nchi yake ina matumaini na ujumbe utakaotolewa katika mkutano huo utafanikiwa na kuleta mabadiliko ya sera ambazo kundi la BRICS linazitazama kama zisizo na usawa kutokana na maamuzi ya mataifa ya Ulaya na Marekani.

Muungano wa masoko ya kifedha

Mataifa hayo matano ambayo yanakusanya karibu ya nusu ya watu wote duniani yanatarajiwa kutangaza hatua za umoja wa kiuchumi miongoni mwao ikiwa ni pamoja na kuunganisha masoko yao ya fedha na mpango wa kuwa na mfuko wa fedha kwa ajili ya maendeleo pamoja ndani ya Benki ya Dunia

Kundi hilo limekuwa likikosolewa kwa muundo wake hauwezi kuwa na mafanikio, lakini mwanauchumi Jim O´Neill anasema kuwa kitendo cha nchi hizo kukutana tu, kinatosha kufikisha ujumbe kwa wahusika.

Mwanauchumi huyo analitazama kundi hilo kama kengele inayolikumbusha kindi lingine la G7 na mataifa ya magharibi kuwa yanahitaji kufanya mabadiliko na kutoa fursa kwa mataifa ya G20, IMF na Benki Ya Dunia kushiriki katika masuala ya fedha ya kidunia kwa uhuru zaidi.

Mkutano huo pia utajadili masuala mengine ya utawala,mabadiliko ya hali ya hewa duniani, ugaidi, pamoja na masuala ya chakula usalama.

Suala la hali ya usalama katika eneo la mashariki ya kati pia litajadiliwa katika mkutano huo pamoja na mpango wa nyuklia wa Iran.

Mwandishi: Stumai George/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef