1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matayarisho ya kura ya maoni Sudan yaingia hatua mpya

Admin.WagnerD25 Oktoba 2010

Matayarisho ya kura ya maoni ya Sudan ya Kusini yanaingia hatua muhimu baada ya kupatikana kwa madftari ya wapiga kura na waasi wa Darfur wametangaza azma ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo na serikali ya Khartoum.

https://p.dw.com/p/PnJ0
Upigaji kura nchini Sudan
Upigaji kura nchini Sudan

* Kura inatarajiwa kupigwa Januari 9

* Sudan ya Kusini yaanza kutafuta wimbo wa taifa

* Waasi wa Darfur kurudi kwenye mazungumzo

Sasa kuna dalili kwamba ule mkwamo wa kura ya maoni ya Sudan ya Kusini unakwamuka. Kwa mujibu wa afisa wa Kamisheni inayoratibu kura hiyo, Jamal Mohammed Ibrahim, hapo jana (24 Oktoba 2010) wachapishaji wa Afrika ya Kusini waliwasilisha madaftari zaidi ya 500,000 ya kusajili wapiga kura, ambayo yanatosha kwa Wasudan ya Kusini wanaoishi kwenye majimbo 15 ya Kaskazini. Mamilioni ya madaftari mengine yatawasili hivi karibuni katika mji mkuu wa Sudan ya Kusini wa Juba.

Kamisheni hiyo pia imetangaza tarehe 14 Novemba hadi 1 Disemba mwaka huu kuwa ni siku za usajili wa wapiga kura na kwamba orodha ya mwisho ya wapiga kura itachapishwa tarehe 4 Januari mwakani, ikiwa ni siku tano tu kabla ya upigaji wenyewe.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan
Rais Omar al-Bashir wa SudanPicha: picture-alliance/dpa/Montage DW

Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Chan Reek Madut, aliliambia Shirika la Habari la Reuters, na hapa namnukulu: "Hii ni hatua kubwa sana...Vifaa vinapokuwepo karibu, kila mtu hupata imani kwamba mambo yanasonga mbele." Aliongeza kwamba hadi sasa wanatarajia kura itapigwa siku ile ile ya Januari 9 kama ilivyopangwa hapo awali.

Hakikisho la Khartoum

Na si hayo tu, bali mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya nje ya Baraza la Seneti la Marekani, John Kerry, alisema hapo jana (24 Oktoba 2010) kwamba ana hakikisho la kimaandishi la serikali ya Sudan kwamba itaheshimu maamuzi yoyote yatakayofanywa na wapiga kura hapo Januari 9 mwakani. Hapo kabla, Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa na wasiwasi na msimamo wa Rais Omar Al-Bashir wa Sudan, hasa aliponukuliwa akisema kwamba hakubaliani na chochote zaidi ya umoja wa Sudan, kauli iliyochukuliwa kwamba inamaanisha hatakubaliana na kujitenga kwa Kusini.

Lakini akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Seneta Kerry alisema, na hapa namnukuu: "Serikali ya Sudana imenikabidhi maazimio ya kimaandishi yanayoapa kwa lugha fasha na makini kwamba itaheshimu maamuzi ya kura ya maoni, vyovyote yatakavyokuwa, na itawapa majirani zao wa kusini ushirikiano mkubwa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama."

Hakikisho la sasa la serikali ya Sudan, limechukuliwa na wengi kwamba ni hatua nyengine kubwa katika kuhakikisha nchi hiyo haingii tena kwenye machafuko baada ya makubaliano ya 2005 yaliyomaliza miaka 22 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wimbo wa taifa wa Sudan ya Kusini

Wakati hayo yakiendelea, mashindano ya kutafuta wimbo wa taifa wa Sudan ya Kusini yanaendelea. Hapo jana, vikundi kumi vya wanamuziki vilishindana kuweka sauti nyimbo zilizochaguliwa kutoka mashindano ya washairi na waandishi, mwezi uliopita. Baadaye jopo la wanamuziki wa Sudan ya Kusini watachagua nyimbo tatu, na mwishoni mwa mwaka huu, serikali itamtangaza mshindi.

Waasi wa Darfur wataka mazungumzo tena na serikali

Kwengineko, jimboni Darfur, kundi la wapiganaji wa Harakati za Haki na Usawa, JEM, limetangaza kwamba litapeleka ujumbe wake nchini Qatar kujadili masharti yake ya kurejea kwenye mazungumzo na serikali ya Sudan. Msemaji wa kundi hilo, Ahmed Hussein, aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba, ujumbe wake utaonana na wapatanishi wa Qatar ili kuangalia uwezekano wa kuendeleza mazungumzo.

Kundi hili lilisaini makubaliano ya kuacha mapigano na serikali ya Khartoum jijini Doha mwezi Februari mwaka huu, lakini mazungumzo yalifeli na muda uliowekwa na makubaliano hayo ulimalizika tarehe 15 Machi na tangu hapo mamia ya watu wameshakufa kwenye mapigano baina ya pande hizo mbili.

Darfur, ambalo ni jimbo lenye ukubwa, sawa na nchi ya Ufaransa, limekuwa likishuhudia machafuko tangu mwaka 2003, ambayo tayari yameshagharimu maisha ya watu 300,000 na kuwageuza wakimbizi wakaazi wapatao milioni 3.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters

Mhariri: Othman Miraj