1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya michezo katika juma

14 Desemba 2007

AC Milan kuumana na Boca Juniors kesho kuwanjia ubingwa wa dunia na shutuma za matumizi ya madawa ili kuimarisha misuli yatawala zaukumba mchezo wa baseball nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/CbcY
Nyota wa AC Milan Kaka.Picha: AP

Jumapili asiye na mwana aeleke jiwe na asiye na mguu atiye gongo kwani huko Yakohama nchini Japan AC Milan ya Italia mabingwa wa ulaya wanamenyana na Boca Juniors ya Argentina Amerika kusini katika fainali ya kombe la kilabu bingwa ya dunia.

Utakumbuka Juniors walitinga fainali baada ya kuwabwaga mabingwa wa Afrika Etoile du Sahel ya Tunisia bao moja kwa bila katika mcheuzo wa nusu fainali. Na Milan ikailaza Urawa Reds ya Japan pia bao moja kwa bila lililofungwa na mchezaji nyota wa Brazil Kaka akimalizia mpira uliofanyiwa kazi na Clarence Seedorf.

Kilabu zote mbili zimeshashinda kombe hilo la dunia mara tatu kila moja, mashindano ambayo hadi sasa umekua ni msisimko kati ya Ulaya na Amerika kusini tangu yalipoanzishwa 2005.

Mpambano huo utakua nafasi nyengine kwa AC Milan kujaribu kulipiza kisasi, kwani 2003 ni Boca ilioondoka na ushindi na Kaka anasema safari hii wamejianadaa vyema. Aidha ikiwa Milan itashindwa tena kufua dafu safari hii basi yaliotokea mwaka jana yatajirudia baada ya timu nyengine ya Ulaya – Liverpool ya Uingereza kulala mbele ya waakilishi wa Amerika kusini wakati huo kilabu ya Sao Paulo ya Brazil.

Matumaini ya AC Milan kesho yanaegemea zaidi katika mafanikio yao mwaka huu baada ya kushinda kombe la ligi ya Ulaya champions league na lile linalojulikana kama Super Cup. Lakini wachambuzi wanasema ni vigumu kuzitabiri timu za Amerika kusini. Suali ni jee Milan ilioshindwa na Liverpool katika fainali ya champions league ilikua ya msisimko miaka miwili iliopita na hatimae kulipiza kisasi mwezi Mei na kulitwaa kombe la kilabu bingwa mwaka huu , itafuzu tena mbele ya Boca ? bila shaka firimbi ya mwisho ndiyo muamuzi.

Huko Uingereza chama cha soka cha England hatimae kiliweka wazi kwamba atakayechukua mamlaka ya kuwa kocha wa timu yake ya taifa atakua ni mwalimu kutoka nje na aliyekaribia kujaza nafasi ilioachwa na Steve McClaren aliyejiuzulu baada ya England kushindwa kukata tiketi ya fainali za kombe la ulaya mwaka ujao, ni Mtaliani Fabio Capello. Wakati hadi jana yakisubiriwa makubaliano ya mwisho, Capello atakua raia wa pili wa kigeni kuteuliwa mwalimu wa timu ya taifa ya England baada ya Sven-Goran Eriksson aliyeshika jukumu hilo 2001 hadi 2006.

Capello aliyekua mchezaji wa zamani wa Italia aliichezea timu ya taifa mara 32 na akashinda ligi mara saba akiwa na AC Miland, AS Roma na Juventus. Pia aliifunza Real madrid ya Uhispania na kutwaa ubingwa 1997 na tena msimu uliopita ambapo baadae Real ilimfukuza kazi. Msisimko mkubwa zaidi kwa Capello pengine, ilikua ni fainali ya Champions league ya kilabu bingwa barani Ulaya, pale Milan ilipoilaza Barceloona ya Uhispania 4-0 na kulitwaa kombe hilo.

Wakati ripoti zinasema Capello anapanga kuwa na wasaidizi kutoka Italia wakati akiinoa timu ya England, tayari kumekuweko na malalamiko miongoni mwa Waingereza wakisema ni aibu kwa soka la nchi hiyo kuwa na kocha wa taifa kutoka nje. Lakini wengine walikumbusha kwamba ni wachezaji wa kigeni walioifanya ligi kuu ya England kuwa ya kusisimua duniani.“

Kuikosoa hatua hiyo ya kuwa na kocha wa kigeni kwa timu ya taifa ya England ni Kocha wa Ufaransa Raymond Domenech ambaye alisema ni aibu kwa makocha wakiingereza . Katika mahojiano na stesheni moja ya redio, Domenech alisema hatua hiyo ni sawa na kuwaambia makocha wa kiingereza kuwa nyote hamfai. Shabiki mmoja wa soka hata hivyo alisema Domenech mwenye anafaa akumbuke kwamba timu ya taifa ya Ufaransa anayoiongoza binafsi kama kocha ,umashuhuri wake unatokana na wengi wa wachezaji nyota wenye asili za kigeni.

Kocha wa zamani wa Brazil na Real Madrid ya Uhispania Vanderlei Luxemburgo ametangaza kwamba anaiacha mkono timu yake ya Santos ya Brazil akiashiria juu aya uwezekano wa kujiunga na timu moja katika ligi ya England Luxemburgo alisema hatorefusha mkataba wake na Santos kilabu ya mfalme wa zamani wa soka duniani Pele, pale utakapomalizika tarehe 31 ya mwezi huu wa Desemba. Alisema sababu kubwa ni kushindwa kuafikiana na Santos juu ya mkakati wake kwa ajili ya misimu miwili ijayo ya ligi.

Barani Afrika, Shirikisho la kandanda la Ivory Coast limekanusha taarifa za magazeti ya kimataifa kwamba imetangaza kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki katika fainali za kombe la mataifa ya Afrik mwezi ujao nchini Ghana. Shirikisho hilo lilisema katika taarifa yake mjini Abidjan kwamba, hakuna afisa yoyote wa ngazi ya juu aliyechapisha orodha ya awachezaji watakaokuwemo katika kikosi hicho kama ilivyoripotiwa na magazeti ya ndani na nje. Likasema litatangaza orodha ya kwanza ya wachezaji 50 wiki ijayo, kabla ya kuchujwa na kubakia 23 tayari kwa mashindano hayo yatakayoanza Januari 20 hadi Februari 10.

Wimbi la matumizi ya madawa aya kuimarisha misuli na nguvu miongoni mwa wachezaji wa fani mbali mbali, limechukua hatua nyengine huko Marekani, baada ya baadhi ya wachezaji maarufu wa mchezo wa baseball nchini humo kutaajwa katika ripoti ya uchunguzi ilioongozwa na Seneta George Mitchell Katika ripoti hiyo imefahamika kwamba matumizi ya dawa za kuimarisha nguvu kinyume ana maumbile, ni jambo lilokua likiendelea bila ya ukaguzi kwa zaidi ya miaka 10 na kwamba timu zote 30 katika ligi kuu ya baseball zimekua na mchezaji mmoja au zaidi waliohusika.

Ametaka ukaguzi wa matumizi ya madawa uimarishwe, akiongeza kuwa ni kisa kilichogeuka kuwa cha hatari kwa vijana hata katika timu za vyuo vikuu na hasa kwa mustakbali wao.

Ripoti hiyo imekuja wiki chache baada ya bingwa wa medali tano za olimpik katika ukimbiaji msichana Marion Jones kukiri kwamba alikua akitumai madawa ya kuimarisha misuli baada ya kukana hapo kabla. Jones alipokonywa medali zote hizo Jumatano wiki hii, ambazo alizinyakua wakati wa mashindano ya Olimpik ya Sedney Australia 2000.