1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi nchini Kenya bado yanasubiriwa

30 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Chz4

Wakenya hii leo bado wanasubiri matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo Alhamisi iliyopita, huku hali ya wasiwasi ikitanda kote nchini.

Hapo jana kulizuka machafuko kufuatia hatua ya tume ya uchaguzi kuchelewelesha kutangaza matokeo ya urais huku wafuasi wa upinzani wakidai kuna njama ya kuiba kura.

Watu kadhaa waliuwawa katika machafuko ya kikabila nchini Kenya, taifa ambalo linaelezwa kuwa tulivu katika eneo linalokabiliwa na mizozo ya kivita.

Matokeo yaliyotangazwa jana na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini humo, bwana Samuel Kivuitu, yamedhihirisha rais Mwai Kibaki anakaribia kumshinda mpinzani wake Raila Odinga ambaye amekuwa akiongoza tangu kura zilipoanza kuhesabiwa.

Washirika wa kisiasa wa Raila Odinga wakiilaumu serikali kwa kuwa na njama ya kuiba kura, walimtatiza bwana Kivuitu wakati walipokuwa wakitangaza matokeo yaliyompa rais Kibaki ushindi wa kura takriban 120,000.

Lakini baadaye mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi alisema Raila Odinga anaongoza kwa kura 38,000 na kusitisha shughuli hiyo inayotarajiwa kuendelea hii leo.

Chama cha ODM na chama cha PNU vyote vinadai ushindi katika uchaguzi huo.