1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani leo wanapiga kura kumchagua mrithi wa Obama

Grace Kabogo
8 Novemba 2016

Wamarekani leo wanapiga kura kumchagua atakayerithi kiti cha Rais Barack Obama huku kukiwa na ushindani mkali kati ya wagombea wawili, Hillary Clinton wa chama cha Democratic na Donald Trump wa chama cha Republican.

https://p.dw.com/p/2SJUA
Bildkombo Hillary Clinton und Donald Trump
Picha: Reuters/R. Cook/C. Keane

Uchaguzi wa leo unafanyika baada ya wagombea wote wawili kukamilisha kampeni zao katika majimbo muhimu. Katika kampeni yake ya Pittsburgh, Clinton amewataka wapiga kura kukumbatia kile alichokiita matumaini na kuwaleta watu pamoja, kusikilizana na kuheshimiana. 

Clinton ambaye amekamilisha kampeni yake usiku wa manene huko North Carolina amesema, ''kuna vitu kadhaa nataka muelewe, kwanza sio suala la jina langu na mpinzani wangu kwenye sanduku la kura, ni aina ya nchi tunayoitaka kwa ajili ya watoto na wajukuu zetu. Nitafanya kazi kwa moyo wangu wote kama rais kuyafanya maisha yawe rahisi kwa ajili yenu na familia zenu. Hivyo usiku huu naomba kura yako, tuweke historia kwa pamoja,'' mwisho wa kunukuu.

Clinton ambaye ameziita kampeni za mpinzani wake kama zilizoleta mgawanyiko, ameahidi iwapo atashinda kuwa rais wa Marekani, ataiunganisha tena nchi hiyo ambayo imegawika kutokana na kampeni mbaya kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani.

Uchaguzi wenye ushindani mkali

Kwa upande wake Trump akiwahutubia wafuasi wake huko Raleigh, North Carolina, ametaka kuungwa mkono katika vita vyake vya kupambana na mfumo wa ufisadi. ''Uchaguzi huu utaamua kama tunatawaliwa na kundi la wanasiasa mafisadi au tunatawaliwa na watu na kwamba mfumo wa kisiasa ulioshindwa haujaleta chochote bali umasikini, matatizo na hasara,'' alisema Trump.

USA Wahlkampf um Präsidentschaft Kombi Anhänger Clinton / Trump
Wafuasi wa Clinton na TrumpPicha: picture-alliance/AP Photo/R. D. Franklin/ G. Herbert

Trump aliendelea kulikosoa Shirika la Upelelezi la Marekani-FBI, baada ya mkuregenzi wake James Comey, siku ya Jumapili kusema kuwa Clinton hawezi kushtakiwa kutokana na kutumia anuani binafsi ya barua pepe wakati akiwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo.

Karibu kura za mapema milioni 24 zimepigwa kuzunguka Marekani wakati Comey alipotangaza hapo awali kwamba ataanzisha upya uchunguzi wa kashfa mpya ya barua pepe dhidi ya Clinton. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la Associated Press, idadi hiyo inawajumuisha zaidi ya nusu ya kiasi ya watu milioni 42.5 ambao wamepiga kura zao hadi jana Jumatatu mchana. 

Naye, Rais Obama amewasihi Wamarekani kuweka historia kwa kumchagua Hillary Clinton ili aweze kumrithi na kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Marekani. Akizungumza katika kampeni iliyofanyika Ann Arbor, Michigan, Obama amewasihi wapiga kura wampe Hillary heshima kama waliyompa yeye.

Clinton amemalizia kampeni zake kwenye majimbo muhimu ya North Carolina, Pennsylvania na Michigan, huku Trump akielekea kwenye majimbo ya Florida, North Carolina, Pennsylvania, New Hampshire na Michigan.

Takwimu za mwisho kabisa zinaonyesha kuwa Clinton anaongoza kwa ushindi mwembamba dhidi ya Trump. Utafiti wa maoni uliotolewa na kituo cha Televisheni cha ABC na Jarida la Washington Post umeonyesha asilimia 47 ya wapiga kura 1,763 wanamuunga mkono Clinton, huku asilimia 43 wakimuunga mkono Trump.

Matokeo ya uchaguzi huo yanasubiriwa kwa hamu kubwa na yanatarajiwa kuanza kutangazwa hapo kesho.  


Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu