1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini katika kambi ya kocha Löw

30 Mei 2014

Dimba la Kombe la Dunia linang'oa nanga katika kipindi cha wiki mbili zijazo, na baada ya wiki iliyojaa misukosuko, hatimaye kuna habari nzuri kwa kikosi cha Ujerumani chake kocha Joachim Löw

https://p.dw.com/p/1C9ba
Deutsche Fußballnationalmannschaft Trainingslager Südtirol Besprechung
Picha: picture-alliance/dpa

Mlinda lango nambari moja Manuel Neuer na nahodha Philip Lahm wameanza kufanya mazoezi na timu ya taifa baada ya kupona majeraha.

Manuel Neuer na nahodha Philip Lahm wamekuwa wakimkosesha usingizi kocha wa timu ya taifa Joachim Löw kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita, tangu Lahm alipojeruhiwa mguu wake naye Neuer akapata jeraha la bega wakati akiichezea Bayern Munich katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB dhidi ya Borussia Dormtund mjini Munich.

Miongoni mwa wachezaji wengine wanaompa wasiwasi Löw ni beki wa kushoto Marcel Schmelzer, ambaye bado anauguza jeraha la goti, na kiungo Bastian Schweinsteiger, aliyejiunga na wenzake kikosini kwa mazoezi ya kawaida. Kiungo Sami Khedira amerejea kambini lakini hajapona kikamilifu kutokana na jeraha lake la goti.

Kiungo Sami Khedira amejiunga na wenzake kikosini
Kiungo Sami Khedira amejiunga na wenzake kikosiniPicha: picture alliance/augenklick/GES

Kiungo huyo wa Real Madrid ambaye alicheza kwa saa moja katika fainali ya Champions League mjini Lisbon anasema atakuwa tayari kwenda Brazil. Khedira anasema "Niko sawa. Kuna mambo madogo tu, ambayo mwenyewe nastahili kuyaimarisha. Sasa ninaendelea na mazoezi na ninaweza kupambana. Sasa mambo ya majeraha hayamo tena kichwani mwangu"

Lahm, Neuer, Schweinsteiger na Khedira ni wachezaji muhimu katika kikosi cha Ujerumani, ambacho kina mechi mbili za kirafiki dhidi ya Cameroon kesho Jumalili na Armenia mnamo Juni 6.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu