1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini madogo baada ya Copenhagen

21 Desemba 2009

Mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa umemalizika Copenhagen bila ya kupatikana makubaliano ya kimataifa ya mazingira. Matokeo ya mkutano huo ni kinyume na vile ilivyotarajiwa.

https://p.dw.com/p/L9mu
Tens of thousands demonstrators take part in a march in the center of Copenhagen Saturday Dec. 12, 2009. Large crowds turned out for a demonstration from the city center to Bella Center, the conference venue where the largest and most important U.N. climate change conference is underway aiming to secure an agreement on how to protect the world from calamitous global warming. (AP Photo/Peter Dejong
Wanaharakati wa mazingira wakiandamana Copenhagen.Picha: AP

Moja lililodhihirika ni kuwa jamii ya kimataifa ina matatatizo ya aina moja, hofu za aina moja na pia matumaini ya aina moja kuwa mabadiliko ya hali ya hewa hayatosababisha maafa.

Mjumbe mmoja wa shirika lisilo la kiserikali kutoka Kamerun alielezea jinsi mama yake ambae hajui kusoma wala kuandika alimuuliza kabla ya kuondoka, iwapo Copenhagen ni bidhaa mpya na iwapo ni nzuri, kwani amelisikia neno hilo mara kwa mara. Akamjibu kuwa bidhaa hiyo Copenhagen bado haipo lakini atakaporejea huenda bidhaa hiyo Copenhagen ikapatikana. Na yeye ndio atakaemuambia iwapo ni nzuri au mbaya.

Mkutano wa Copenhagen hasa ni fadhaa kwa serikali na wakati huo huo ni ishara kuwa umma katika nchi nyingi duniani unaweza kukubaliana katika suali moja: Mkutano wa Copenhagen haukuhusika na hali ya hewa tu bali hata haki ya kuwa na maendeleo, haki ya kujipatia chakula, haki ya kuwa na maji na hatimae haki ya kuendelea kuishi.

Wanasiasa hawajawahi kushinikizwa na kulaumiwa na jamii ya kimataifa kama ilivyokuwa safari hii katika mkutano wa mazingira mjini Copenhagen. Ikiwa ni maandamano na mikutano ya wanaharakati au juhudi za ufanisi za mashirika mengi yasio ya kiserikali. Moja ni dhahiri,sera za kimataifa hazitoamuliwa tena kutoka juu bali kutoka chini vile vile.

Mwanya kati ya matajiri na masikini, kati ya nchi za kaskazini na kusini na kati ya wanaonusurika na wanaokufa unazidi kuwa mpana na ni kama kidonda kinachozidi kuwa kikubwa. Na hiyo si kwa sababu ya majadiliano ya mabadiliko ya hali ya hewa tu bali ni hali inayosababisshwa na jamii nzima duniani. Hicho ni kidonda kinachobainisha hisia mbaya za binadamu: tamaa, kiburi,hofu na hali ya kutoaminiana.

Matatizo hayo yote yanapaswa kupatiwa ufumbuzi. Labda hicho ndio kilichobainika katika mkutano wa Copenhagen - jitahada za kupata ufumbuzi zianzie chini. Kwani ubunifu,mshikamano na shauku iliyoonyeshwa mjini Copenhagen na mashirika yasio ya kiserikali na hata wanasayansi na kwa sehemu fulani miongoni mwa wanauchumi, huenda ikasaidia kuponyesha kidonda cha kimataifa na kupatikana njia ambayo sio tu ya kuhifadhi hali ya hewa bali pia kudhamini mustakabali wa haki.

Mwandishi: H.Jeppesen/ZPR

Mhariri: M.Abdul-Rahman