1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini madogo kuhusu mkutano wa Annapolis

P.Martin26 Novemba 2007

Mkutano ulioitishwa na Marekani katika juhudi mpya ya kutafuta suluhisho la amani katika Mashariki ya Kati unaanza rasmi leo hii mjini Annapolis katika jimbo la Maryland nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/CTQf
Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert
Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Ehud OlmertPicha: AP

Kijujuu yaonekana kana kwamba kila kitu ni barabara kwa mkutano wa Mashariki ya Kati mjini Annapolis:kwani nchi muhimu zimekubali kuhudhuria mkutano huo,mojawapo ikiwa ni Saudi Arabia.Na zaidi kilichowashangaza wengi,ni kushiriki kwa Syria,inayohesabiwa na Rais wa Marekani George W.Bush kama mojawapo ya nchi iliyo korofi kwa sababu ya uhusiano wake wa karibu pamoja na Iran. Mkutano huo ukichunguzwa kwa makini,yadhihirika kuwa itakuwa vigumu mno kuwasilisha mpango wa kusuluhisha mzozo wa Mashariki ya Kati,sembuse kutekelezwa.Majadiliano ya juma lililopita kati ya Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert yalidhihirisha kuwa misimamo ya pande hizo mbili bado inatofautiana sana.

Kwenye mkutano wa Annapolis,Olmert anataka kusisitiza kuwa mpango wa amani unaojulikana kama Roadmap utekelezwe.Huo ukitazamwa kama ni njia pekee ya kupata amani katika Mashariki ya Kati na unahimizwa na kundi la pande nne tangu miaka kadhaa.Pande hizo nne ni Marekani,Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa na Urusi.Hata Rais wa Wapalestina Abbas anauunga mkono mpango huo lakini yeye na Olmert wanatofautiana katika masuala muhimu kwenye utaratibu huo wa amani.

Abbas anasema,kabla ya kundwa kwa taifa la Palestina,suluhisho lapaswa kupatikana kuhusu wakimbizi wa Kipalestina,Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi na vile vile iache kuweka vikwazo katika maeneo ya Wapalestina.

Kwa upande mwingine Olmert amezungumzia juu ya kuwa na maafikiano yanayoumiza lakini kwanza kabisa amesema,mashambulizi yanayofanywa dhidi ya Israel yakomeshwe na makundi ya kigaidi yatokomezwe ili majadiliano ya amani yaweze kuanza kwa dhati.Lakini Olmert anafahamu vyema kuwa hayo ni mambo yasiyoweza kutekelezwa na Abbas.

Hata hivyo,kiongozi wa Wapalestina anautaka mkutano wa Annapolis uweke utaratibu maalum wa kufuatilizwa.Muhimu kabisa anatazamia kuwa tarehe maalum ya kuanzishwa majadiliano ya amani itapangwa kwenye mkutano wa Annapolis.Kwani anafahamu vyema kuwa hawezi kurejea nyumbani mikoni mitupu,ama sivyo atapoteza uso katika kinyanganyiro cha mamlaka na kundi la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza.Chama cha Hamas kinapinga mkutano wa Annapolis na hata mchakato wa amani na ikiwa mkutano huo utakuwa na mafanikio madogo tu,basi hali hiyo itatumiwa na Hamas kuhalalisha upinzani wake.

Waziri Mkuu Olmert pia hataki kujikuta katika hali ya kulazimika kukubaliana na baadhi ya mambo.Kwani yeye vile vile anashinikizwa nyumbani na wahafidhina katika baraza lake la mawaziri na hata upande wa upinzani.Na hata yeye binafsi, licha ya matamashi yake ya kutaka amani,ni miongoni mwa vigogo vya kihafidhina ambao kimsingi,wanapinga kuridhia ardhi na kuundwa kwa taifa la Palestina.