1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya Wazimbabwe

L-Schadomsky - (P.Martin)11 Februari 2009

Morgan Tsvangirai hii leo ameapishwa Waziri Mkuu mpya wa Zimbabwe na hivyo kumaliza mgogoro wa miezi mitano na Rais Robert Mugabe kuhusu makubaliano ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.

https://p.dw.com/p/Gs2J
Morgan Tsvangirai, leader of Zimbabwe's main opposition party, addreses a press conference in Harare, Tuesday, Feb. 10, 2009. Tsvangirai announced the names of Ministers from the opposition party who would be part of the inclusive government, ahead of his inauguration as Zimbabwe's Prime Minister on Feb. 11.(AP Photo/Tsvangirayi Mukwazhi)
Waziri Mkuu mpya wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai.Picha: AP

Ni matumaini ya Wazimbabwe wanaoteseka kwa mfumuko wa bei na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu,kuwa serikali mpya yenye mawaziri 31 itawaondosha kutoka janga hilo.

Mpinzani mashuhuri wa siasa za ubaguzi na mtengano wa Afrika Kusini Desmond Tutu alipoeleza maoni yake kuhusu serikali ya mpito katika nchi jirani alisema,mkataba wa ushirikiano hauna hata thamani ya karatasi iliyoandikiwa.Kwa maoni yake,bila ya Mugabe ndio mabadiliko yataweza kupatikana nchini Zimbabwe.Hiyo bila shaka ni njozi ya Askofu Mkuu Tutu, kwani Mugabe hatoondoka madarakani kabla ya kumalizika kipindi cha mpito cha miezi 18 ambapo kutafanywa uchaguzi mpya.

Lakini hivi sasa alieshika wadhifa muhimu kabisa ni Tendai Biti, mwanasheria na mtaalamu wa masuala ya uchumi wa chama cha MDC. Kama ilivyotarajiwa na wengi,Biti ameteuliwa na Morgan Tsvangirai kuiongoza wizara ya fedha.Kama Zimbabwe inayokabiliwa na mfumuko wa bei wa asilimia milioni 230 itaachilia sarafu yake kujitafutia thamani yake katika soko la fedha, itarejesha imani ya wafadhili na mashirika ya fedha na kufufua uchumi- yote hayo hutegemea kwa sehemu kubwa maamuzi ya mwanasiasa huyo mwenye miaka 42 .

Ikiwa Biti ataifanya kazi yake vizuri,basi yale yaliyotokea nchini Afrika ya Kusini katika miaka ya 90 yataweza pia kushuhudiwa Zimbabwe.Wakati huo Trevor Manuel Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini, alifanikiwa kuondosha wasi wasi katika masoko ya fedha na kuvutia uwekezaji nchini Afrika ya Kusini. Ikiwa Biti ataweza kuzuia mapambano na Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe Gideon Gono alie mshirika mkubwa wa Mugabe, basi kama ilivyoahidiwa nchi za Ulaya kwa haraka na bila ya urasimu zitaanza kutoa msaada na ikitakikana zitafikiria upya sera zake kuhusu vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.