1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini yajitokeza nchini Myanmar

Josephat Charo9 Novemba 2007

Kiongozi wa upinzani anayetumikia kifunga cha nyumbani, Aung San Suu Kyi, amesema ana matumaini makubwa baada ya kukutana na na afisa wa utawala wa kijeshi ya Myanmar. Sambamba na hayo, Umoja wa Ulaya umesema huenda ukaunda kikosi kitakachosaidia juhudi za Umoja wa Mataifa kuutanzua mgogoro wa Myanmar.

https://p.dw.com/p/CH78
Aung San Suu Kyi
Aung San Suu KyiPicha: AP

Wanachama wanne wa chama cha upinzani cha National League for Democracy, NLD, wamekutana na Aung San Suu Kyi mapema leo kwa muda unaokaribia saa nzima kwenye nyumba moja ya wageni inayomilikiwa na serikali mjini Yangon. Aung San Suu Kyi amekutana pia na afisa wa utawala wa kijeshi wa Myanmar kwa muda kama huo.

Katika taarifa yake aliyowasomea waandishi wa habari mjini Yangon hii leo, msemaji wa chama cha National League for Democracy, Nyan Win, amesema Aung San Suu Kyi, anaamini utawala wa kijeshi wa Myanmar una ari ya kuwa na maridhiano ya kitaifa.

Aung San Suu Kyi amekutana na viongozi watatu wa ngazi ya juu wa chama cha NLD, Aung Shwe, Lwin, Nyut Wai na baadaye akakutana na msemaji wa chama Nyan Win, kabla kukutana na afisa wa utawala wa kijeshi, Aung Kyi, ambaye ni waziri wa mahusiano. Waziri huyo aliyeteuliwa na makamanda wa jeshi la Myanmar awe mpatanishi kufuatia kuzuka hasira kubwa ulimwenguni kote wakati wanajeshi walipotumia nguvu kupita kiasi kuyazima maandamano yalioongozwa na watawa wa kibuda mjini Yangon mnamo mwezi Septemba mwaka huu.

Aung San Suu Kyi amesema matukio ya mwezi Septemba na Oktoba ni mabaya na ya kuhuzunisha, sio tu kwa chama cha NLD, bali pia kwa serikali na wananchi wote wa Myanmar. Aidha kiongozi huyo ameongeza kusema kuwa ipo haja ya kufanya juhudi za kuendeleza mchakato wa kutafuta msamaha na kuponya hisia za wengi zilizoathirika, lakini hakufafanua.

Alipoulizwa aulinganishe mkutano uliofanyika mnamo mwaka wa 2004 na mkutano uliofanyika leo Ijumaa mjini Yangon, msemaji wa chama cha NLD, Nyan Win, amesema mazungumzo ya leo yamedhihirisha kuwepo matumaini makubwa na utawala wa kijeshi uko tayari kushirikiana na upinzani. Haya yamedhihirika pia wakati wa mkutano kati ya Aung San Suu Kyi na afisa wa serikali.

Mikutano ya leo imefanyika baada ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Myanmar, Ibrahim Gambari, kukamilisha ziara yake ya siku sita nchini humo. Gambari amesema sasa kuna mchakato unaoendelea ambao unatakiwa kusaidia kuwepo mazungumzo ya maana kati ya serikali ya Myanmar na kiongozi wa upinzani, Aun San Suu Kyi.

Wakati haya yakiarifiwa, mjumbe maalumu wa Umoja wa Ulaya nchini Myanmar, Piero Fassino kutoka Italy, amesema umoja huo huenda ukaunda muungano wa nchi zinazohusika kwa karibu na mzozo huo, ili kuzisaidia juhudi za Umoja wa Mataifa kuumaliza mgogoro wa Myanmar. Fassino amesema muungano huo utafanana na ule wa nchi sita zinazoujadili mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini au pande nne zinazodhamini mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.

Kiongozi huyo amemsifu mjumbe wa Umoja wa Mataifa bwana Ibrahim Gambari kwa kufaulu kuwakutanisha viongozi wa upinzani na Aung San Suu Kyi na afisa wa serikali ya Myanmar, akisema Gambari anaungwa mkono kikamilifu na jumuiya ya kimataifa.