1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya kikatili yafanyika Syria

Elizabeth Shoo29 Januari 2013

Maiti zisizopungua 65 zimekutwa katika mji wa Aleppo, Kaskazini mwa Syria. Imeripotiwa kwamba maiti hizo ni za watu wanaoelekea kupigwa risasi kichwani na waliokuwa wamefungwa mikono nyuma ya migongo yao.

https://p.dw.com/p/17Tc5
In einem kleinen Fluss, der von dem Stadtteil von Aleppo kommt, der von Regierungstruppen kontrolliert wird, werden am 29.01.2013 Dutzende Leichen gefunden. Die meisten sind auf dem Rücken gefesselt und durch Kopfschuss hingerichtet worden. Helfer, Polizei und Anwohner gehen davon aus, dass sie von Assad-Anhängern getötet wurden. Foto: Thomas Rassloff dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++
Aleppo LeichenfundPicha: picture-alliance/dpa

Miili ya wanaume na vijana hao ilikutwa katika mto mmoja mjini Aleppo. Yote ilikuwa na alama ya risasi kichwani au shingoni. Shirika la kutetea haki za binadamu Syria na lenye makao yake makuu London, Uingereza, limesema kwamba maiti bado zinaendelea kutolewa mtoni na hivyo idadi ya waliouwawa inaweza kufikia 80.

Maafisa wa jeshi huru la Syria wanakisia kwamba idadi yao inazidi 100. Mpaka sasa haifahamiki ni nani aliyefanya mauaji hayo ya kikatili. Hata hivyo, jeshi huru la Syria limenyoosha kidole kwa wanajeshi wa rais Bashar al-Assad na kusema wao ndio waliofanya mauaji hayo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameishutumu serikali ya Syria na vile vile waasi kwa kufanya mauaji ya kinyama katika kipindi cha takriban miaka miwili ambapo mapigano yamekuwa yakiendelea. Mpaka sasa zaidi ya watu 60,000 wamepoteza maisha yao katika vita vya Syria na wengine milioni mbili kulazimika kuyahama makaazi yao.

Mji wa Aleppo umeharibiwa vibaya na mapigano
Mji wa Aleppo umeharibiwa vibaya na mapiganoPicha: DW/A. Stahl

Shughuli za kuzitoa maiti mtoni bado zinaendelea. Mmoja wa watu waliojitolea kufanya kazi hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawafahamu ni akina nani waliouwawa kwani hawakuwa wamebeba vitambulisho.

Kapteni Abu Saba wa jeshi huru la Syria amesema kuwa maiti zitapelekwa katika hospitali moja ambapo watu wanaweza kuja kuangalia kama kuna ndugu yao. Wale ambao hawatatambuliwa na ndugu watazikwa kesho katika kaburi la pamoja.

Michango kwa ajili ya wakimbizi yakusanywa

Hii si mara ya kwanza kwa maiti kukutwa katika mto, kama anavyoeleza Abu Anas wa jeshi huru la Syria. Hata hivyo, ni mara ya kwanza kwa idadi ya maiti kuwa kubwa hivi. "Wanamgambo wa serikali hukamata watu wanaovuka katika vituo vya ukaguzi. Wanawatesa na kuwauwa wengi wao," anaeleza Anas.

Wapiganaji wa jeshi huru la Syria wakiwa wamebeba silaha
Wapiganaji wa jeshi huru la Syria wakiwa wamebeba silahaPicha: Reuters

Leo hii, mashirika ya kutoa msaada yasiyo ya kiserikali, yamekutana nchini Kuwait na kuahidi kutoa jumla ya dola za kimarekani milioni 182 kwa Wasyria walioathiriwa na vita nchini mwao.

Hapo kesho utafanyika mkutano mwingine wa aina hii. Mkutano huo umeandaliwa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. Nchi mbalimbali zinatarajiwa kupeleka mchango au kuweka ahadi ya kutoa fedha zitakazowasaidia wakimbizi hao. Kwa nusu ya kwanza ya mwaka huu inakadiriwa kuwa zinahitajika dola za kimarekani bilioni 1.5 kuwahudumia wakimbizi wa Syria kikamilifu.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman