1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya waasi wa ADF nchini DRC kupata suluhu?

Admin.WagnerD2 Juni 2021

Kamanda mpya wa operesheni dhidi ya waasi wa ADF ameingia madarakani katika mji wa Beni. Kamanda huyo atakuwa na changamoto kubwa ambayo ni kuwatokomeza waasi hao wanaotokea Uganda na kumaliza visa vya mauaji ya raia.

https://p.dw.com/p/3uLEk
Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Wakati waasi kutoka Uganda ADF wanazidisha mashambulizi yao katika maeneo ya Beni pamoja na Irumu kaskazini mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kamanda mpya wa operesheni dhidi ya waasi hao, ameingia madarakani katika mji wa Beni. Kamanda huyo atakuwa na changamoto kubwa, ambayo ni kuwatokomeza waasi hao wanaotokea Uganda na kumaliza visa vya mauaji ya raia.

Huyo ni mmoja wa maofisa wa jeshi katika Sekta ya operesheni za kijeshi katika eneo la Kaskazini la mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Sokola1, akisoma barua ya kukabidhiana madaraka, baina ya kamanda wa zamani wa operesheni Meja Jenerali Peter Cirimwami anayeondoka, na kamanda mpya Brigedia Mputela Bertin anaeingia madarakani.

Soma Zaidi: Wanafunzi DRC washinikiza Rais Tshisekedi kuzuru Beni

Makabidhiano hayo ya madaraka kati ya makamanda hao wawili yanafanyika, wakati waasi kutoka Uganda ADF wanazidisha mashambulizi yao dhidi ya vijiji mbalimbali huku wakiwauwa raia wangi.

Siku ya Jumatatu,waasi hao waliwauwa si chini ya raia mia moja katika vijiji vya Tchabi na Boga, mashariki ya wilaya ya Irumu katika mkoa wa Ituri.

Demokratische Republik Kongo | Überfall auf UN-Lager in Beni
Wanavijiji katika eneo la Beni wamekuwa wakiwindwa na wanamgambo wa ADF na kushambuliwa kila wakati.Picha: picture-alliance/dpa/0AP Photo/A.-H. K. Maliro

Raia wazidi kuuawa wilayani Beni.

Na jana Jumanne, ADF waliwauwa watu watano katika kijiji cha Mayimoya, kaskazini mwa mji mdogo wa Oicha mji mkuu wa wilaya ya Beni.

Akiwa na changamoto zinazomsubiri katika uongozi wa jeshi katika eneo hili, Brigedia Mputela Bertin anawaomba maofisa atakaofanya nao kazi, kuwa tayari kuitumikia nchi huku akiwaonya kutokuwa na undumilakuwili.

"Mie nawapenda wachapa kazi,msiwe wanafiki, mkono mkononi, tuchape kazi pamoja. Msiwe kama nyoka aliye na vichwa viwili, tuko hapa kwa ajili ya kupigania nchi yetu. Kama munadhani kwamba hamuko tayari kufanya kazi pamoja na mimi hapa muda ndio huu. Mimi napenda kwenda kwenye uwanja wa mapambano. Kwa hiyo munatakiwa kuwa tayari kwa wakati wowote na nafasi zote na hiyo kwa masaa ishirini na manne kwa ajili ya kazi." alisema Brigedia Bertin

Kwa upande wake, mkuu wa majeshi ya ardhini katika jeshi la Congo Luteni Jenerali Fall Sikabwe, akiwa ziarani Beni kukadiria operesheni dhidi ya makundi ya uasi, na kubwa kuliko yote likiwa ni lile la ADF ametangaza kwamba kuna vifaa vya kisasa vitakavyotumika kwa ajili ya kuwashughulikia waasi. Ametangaza pia kutumwa hapa kwa vikosi vipya vilivyomaliza mafunzo tayari.

Alisema, "Tunavyo vifaa vya teknolojia ya kisasa ambavyo tutaviweka hapa kwa ajili ya kukesha ili kulinda mipaka yetu, na tunavyo vikosi ambavyo vimemaliza mafunzo na vitakavyotumwa hapa ili kuilinda mipaka yetu kwanza, na pili kuyatokomeza makundi yote ya waasi yaliyoko ndani ya nchi, iwe makundi ya uasi ya ndani na yale ya uasi kutoka nje ya nchi."

Demokratische Republik Kongo | Überfall auf UN-Lager in Beni
Wanajeshi wa kulina amani nchini DRC wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo kutoka kwa raia wakidai kushindwa kulinda amani nchini humo.Picha: Reuters/File Photo/O. Oleksandr

Raia waombwa kuunga mkono operesheni za kijeshi.

Nazo operesheni kabambe za kijeshi zinazotarajiwa hapa, kufuatia kutangazwa na rais Tshisekedi kwa hali ya dharura katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri, ili zifanikiwe, raia wanatakiwa kuwaunga mkono viongozi wapya wa kijeshi katika ngazi zote. Na ni kwa mantiki hiyo ndio mwenyekiti wa mashirika mapya ya kiraia katika eneo hili Moise Kiputulu anawaomba wakaazi kuwapatia viongozi taarifa kuhusu mahala wanakojificha waasi.

Kutupulu alisema "Tunawaomba wakaazi kuendelea kuwaunga mkono na kuwaletea habari vyombo vya kijasusi na hasa viongozi wapya walioteuliwa wakati huu wa hali ya dharura, ili kuwasaidia viongozi hao kukamilisha kazi yao kwa muda mfupi."

Kwa kipindi cha wiki moja, waasi kutoka Uganda ADF, wamewaua raia karibia mia mbili, katika mashambulizi mbalimbali yaliyolenga vijiji kwenye wilaya ya Beni, hasa katika sekta ya Ruwenzori mkoani Kivu ya Kaskazini, na pia katika vijiji vya Boga na Tchabi, katika wilaya ya Irumu mkoani Ituri.

Muungano wa mashirika ya kitamaduni wa mkoa wa Ituri,umemuomba rais Félix Tshisekedi kutangaza siku tatu za maombolezo ili kuomboleza na familia zilizowapoteza wapendwa wao katika mashambulizi ya vijiji vya Boga na Tchabi, yaliyogharimu maisha ya watu karibia mia moja siku ya Jumatatu.

John Kanyunyu DW Beni.