1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa G8 kuiijadili Korea kaskazini .

25 Juni 2008

Ni kuhusiana na mipango yake ya kinuklea.

https://p.dw.com/p/EQgS
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong-Il.Picha: AP

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi zilizoendelea kiviwanda -kundi linalojulikana kama G8, wanakutana nchini Japan leo, huku mazungumzo yao yakitarajiwa kutuwama juu ya tangazo la Korea kaskazini linalongojewa kwa muda mrefu sasa, juu ya mipango yake ya nuklea.

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa kundi hilo la G8 linalozijumuisha Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Urusi na Marekani watakua na mazungumzo ya siku mbili katika mji wa magharibi wa Kyoto, kuandaa mkutano wa viongozi wakuu wa nchi hizo tarehe 7 hadi 9, mwezi ujao.

Japan ambayo imetaka msimamo mkali uchukuliwe dhidi ya Korea kaskazini, unatarajia kuutumia mkutano huo kushinikiza juu ya mbinyo wa kimataifa kwa Korea kaskazini na Iran kuhusu malengo yao ya nuklea. Lakini mkutano wao unatazamiwa kugubikwa na matukio kutoka upande wa Korea kaskazini. taifa hilo linatarajiwa kukabidhi hii leo, ikiwa ni takriban miezi saba baadae, taarifa juu ya mipango yake ya nuklea, kama ilivyoagizwa kutokana na makubaliano ya mataifa sita kuhusu utaratibu wa kuukongoa mradi wake huo.

Mpatanishi mkuu wa Marekani Christopher Hill aliyefanikisha kupatikana makubaliano mwaka jana, aliwasili Kyoto jana, siku moja kabla ya kuwasili Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condolezza Rice, ambaye ataelekea huko akitokea akitokea Ujerumani ambapo alihudhuria mkutano wa wafadhili kuhusu uimarishaji wa vyombo vya usalama katika maeneo ya wapalestina.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Japan mwenyeji wa mkutano huo Masahiko Komura aliwaambia waandishi habari hapo awali kwamba wanaamini kundi la G8 linawajibu wa kutuma risala nzito, kuitaka Korea kaskazini iheshimu makubaliano yaliofikiwa na kuachana na mradi wake kamili wa kinuklea.

Lakini ukizingatiwa muda uliopangwa na Korea kaskazini kutoa taarifa yake, huenda shinikizo la Japan lisizae matunda.

Marekani imekubali kuiondoa Korea kaskazini katika orodha yake ya mataifa yanayounga mkono ugaidi, ili badala yake Korea kaskazini itowe tamko la kuridhisha na kukubali kuukongoa mradi wake wa kinuklea.

Hatua hiyo itaifungulia njia nchi hiyo inayoandamwa na umasikini kupokea msaada wa Marekani na mikopo ya kimataifa.

Kuhusu Iran waziri wa masuala ya kigeni wa Japan, alisema anatumai watazungumza kwa sauti moja kwamba Iran inapaswa iheshimu maazimio ya baraza la usalama la umoja wa mataifa, yanayoitaka nchi hiyo isitishe urutubishaji wa madini ya uranium.

Aidha alisema pia kwamba mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje wa mataifa hayo manane yalioendelea kiviwanda wataijadili pia hali nchini Zimbabwe, ambako kiongozi wa chama kikuu cha upinzani MDC Morgan Tsvangirai amejitoa katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais, kutokana na kupamba moto kwa machafuko na ukandamizaji dhidi ya wapinzani, vinavyodaiwa kufanywa na wafuasi wa chama tawala ZANU-PF cha Rais Robert Mugabe.

Kandoni mwa mkutano huo wa mawaziri wa kundi la G8, wanaharakati wamepanga maandamano kupinga utandawazi na kutaka kumalizwa harakati za kijeshi zinazoongozwa na Marekani nchini Afghanistan na Iraq.