1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

170609 Agrarsubventionen

Charo Josephat22 Juni 2009

Wakulima na makampuni yanayopokea rukuzu ya kilimo kutangazwa hadharani

https://p.dw.com/p/IWhE
Waziri wa kilimo wa Italia Luca ZaiaPicha: picture-alliance/ dpa

Mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya wanaanza mkutano wao wa siku mbili hii leo mjini Luxembourg kujadili orodha ya majina ya wakulima, wafugaji na makampuni yanayopokea ruzuku ya kilimo na ukiukaji wa taratibu za mikataba.

Kufichuliwa kwa orodha ya Wajerumani wanaopokea ruzuku ya kililimo kutoka kwa Umoja wa Ulaya kwa mara nyengine kumechochea mjadala mkali kuhusu sera ya kilimo ya umoja huo. Mnamo mwaka jana kiwango kikubwa cha ruzuku kilikwenda kwa makampuni ya kutengeneza vyakula na kwa mujibu wa takwimu za wizara ya kilimo na chakula ya Ujerumani, jimbo la Schleswig-Holstein hapa nchini lilipokea kiwango kikubwa zaidi. Kutokana na shinikizo la halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ujerumani ilichapisha kwa mara ya kwanza majina ya watu na makampuni yanayopokea ruzuku ya kilimo, lakini mkoa wa Bayern mpaka sasa umekataa kufanya hivyo.

Kamishna wa kilimo wa Umoja wa Ulaya, Mariann Fischer Boel, ana wasiwasi kuhusu swala hilo. Kila mara anapotaka kuuzima mjadala kuhusu kupotea kwa fedha zinatolewa kama ruzuku ya kilimo husisitiza kwamba fedha hizo zinatumiwa kufikia malengo yanayonuiwa na si vinginevyo.

"Ifahamike wazi kwamba hatudhamini viwanja vya mchezo wa golf. Kwa hiyo natumai maelezo hayo yanatosha kuachana na mjadala huu."

Lakini sasa mjadala huo unaweza kufanyika, hata kama ni kwa kiwango kidogo. Uchunguzi wa takwimu mpya katika mtandao wa intaneti zinaonyesha kuna uwanja wa mchezo wa golf katika orodha ya majina ya watu na makampuni yaliyopokea ruzuku ya kilimo. Uwanja huo ulipokea euro 1,273 kutoka kwa makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Ni maelezo ya kuchekesha lakini yanaweza kuzusha moto mkubwa katika sera ya kilimo ya umoja huo.

Kuanzia sasa inawezekena kwenye mtandao wa intaneti kuandika jina na mahala anakoishi mkulima ili kujua ni kiasi gani cha fedha alichopokea kutoka Brussels. Kwa ujumla takriban euro bilioni 5,5 hutolewa kwa wakulima na makampuni ya Ujerumani kila mwaka, lakini hata hivyo wakulima wengi hupokea kiwango kidogo mno. Zaidi ya nusu ya wakulima wa Ujerumani hupokea chini ya euro 5,000 kwa mwaka. Lakini licha ya takwimu hizi mjadala huu hautakuwa na uzito wowote.

Halikuwa jambo la kutarajiwa kwamba kiwango kikubwa cha fedha kilipelekwa eneo la mashariki la Ujerumani kwa ajili ya kilimo. Ruzuku ya kilimo hutolewa kulingana na ukubwa wa shamba. Kwa kila hekta moja Ujerumani hupokea takriban euro 300; hiyo ina maana mkoa wa Mecklenburg Vorpommern unaweza kupokea euro milioni moja.

La kushangaza zaidi ni ruzuku kwa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi. Kwa kuwa bei ya bidhaa nyingi za Ulaya kama sukari na nyama ya nguruwe ziko juu mno katika masoko ya kimataifa, ruzuku hutolewa ili kuzipunguza bei hizo. Takwimu mpya zinaonyesha kuwa kampuni ya sukari ya Südzucker, ilipokea euro zaidi ya milioni 34 kutoka Brussels kama ruzuku ya kuuza sukari katika nchi za kigeni. Kampuni ya maziwa ya Nordmilch hupokea ruzuku kwa kuuza maziwa katika nchi za kigeni.

Wakulima wa mkoa wa Bayern wamewasilisha kesi ya kutaka walindwe kwa mujibu wa sheria ya kulinda maelezo binafasi ya watu. Mahakama ya Luxemburg inasubiriwa kuamua kuhusu kesi hiyo. Halmashauri ya Umoja wa Ulaya haitaki kusubiri kwa muda mrefu. Inaishutumu Ujerumani kwa kushindwa kitimiza majukumu yake ingawa serikali imeidhinisha sheria za kuwepo uwazi.

Kila mwaka Umoja wa Ulaya hutoa kiasi cha euro bilioni 50 kugharamia shughuli za kilimo, kiwango ambacho ni asilimia 40 ya bajeti jumla ya umoja huo. Kati ya fedha hizo, euro bilioni 30 hutolewa kama msaada wa moja kwa moja kwa makampuni milioni saba ya kilimo katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Brand, Katrin/ Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraj