1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7 wakutana Canada

23 Aprili 2018

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 7 zenye ushawishi mkubwa wa kiuchumi duniani, G7, wamekutana Toronto, Canada wakitafuta mwelekeo mmoja kutokana na kile wanachokiona ni hatua ya kuleta ugomvi kutoka kwa Urusi.

https://p.dw.com/p/2wUvL
Japan Flaggen der G7-Mitgliedsstaaten 2016
Picha: picture-alliance/dpa/K. Ota

Lakini kulingana na afisa mmoja wa Marekani mawaziri hao wameuacha mlango wazi kwa majadiliano na Urusi.

Mataifa hayo saba yenye nguvu za kiuchumi  duniani yanahofia hatua ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kumuunga mkono rais wa Syria Bashar al Assad na utawala wake katika nchi hiyo iliyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na yale madai ya jaribio lake la kumuua jasusi wa zamani wa Urusi nchini Uingereza.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwamba nchi za Magharibi ni lazima zishirikiane kusitisha hatua ya Putin ya kukandamiza demokrasia ikiwemo usambazaji wa habari za uongo.

Hakutatangazwa hatua kamili zitakazochukuliwa Urusi

Mawaziri hao wanatarajiwa kutoa taarifa ya mwisho kuhusiana na mkutano wao baadae Jumatatu. Afisa mmoja anayehudhuria mkutano huo amesema mawaziri hao hawatotumia lugha nyepesi watakapotoa taarifa kuzungumzia suala la Urusi ikizingatiwa yale yaliyofanywa na nchi hiyo kufikia sasa.

Deutschland Energy Transition Dialogue der Bundesregierung
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Lakini kulingana na wanadiplomasia wawili katika mkutano huo mawaziri hao hawatangaza hatua kamili watakazoichukulia Urusi kutokana na kuwa Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Italia ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, umoja ulio na wanachama 28 ambao ni sharti uje na kauli moja kuhusiana na hatua za kuchukuliwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas yeye ameitaka Urusi kusaidia katika kuusuluhisha mzozo wa Syria akisema suluhu haliwezi kupatikana bila Urusi.

Wakati huo huo waziri wa Mambo ya Nje wa Canada Chrystia Freeland pamoja na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini wametangaza mpango wa kufanya mkutano wa mawaziri wote wa mambo ya nje wanawake nchini Canada mwezi Septemba.

Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya nje wa G7 ndio wa kwanza tangu Syria ishambuliwe na Marekani

"Tumefahamu kwamba tuko wengi sana katika mabara tofauti na tunaamini kwamba hii itakuwa njia muhimu ya kufungua njia ya maelewano," alisema Mogherini. "Kama ilivyotajwa tutakuja pamoja kuhakikisha kwamba wanawake na wanaume wanashirikiana ili kuilinda dunia, watu wote na kuhakikisha kwamba kuna amani na usalama," aliongeza Mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya.

Belgien EU-Gipfel - Federica Mogherini
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: Reuters/F. Lenoir

Mkutano wa G7 ndio mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu tangu Marekani, Uingereza na Ufaransa kuzishambulia sehemu zenye silaha za kemikali nchini Syria kujibu madai ya shambulizi la sumu lililofanywa na serikali ya Syria tarehe saba Aprili.

Mazungumzo ya mawaziri hao wa mambo ya nje yanayotarajiwa kukamilika Jumatatu yatasaidia katika maandalizi ya mkutano wa viongozi wa G7 huko Canada mwezi mapema mwezi Juni. G7 inajumuisha Marekani, Uingereza, canada, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Japan.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu