1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ujerumani wasema uamuzi juu Murat Kurnaz ulikuwa sahihi.

29 Machi 2007

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Frank Walter Steinmeier atetea uamuzi wa serikali juu ya kumpeleka Murat Kurnaz nchini Uturuki badala ya kumruhusu kurejea Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHH9
Frank Walter Steinmeier
Frank Walter SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Frank Walter Steinmeier leo ametetea uamuzi wa serikali ya Ujerumani juu ya kukataa kumruhusu bwana Murat Kurnaz kurejea nchini Ujerumani baada ya kushikiliwa kwenye jela ya Marekani ya Guantanamo . Bwana Kurnaz, ambae ni mjerumani mwenye nasaba ya kituruki alishikiliwa kwa muda wa miaka minne kwenye jela hiyo kwa tuhuma za kuwa gaidi.

Waziri Steinmeier amesema uamuzi wa serikali ulikuwa sahihi wakati huo, kwa sababu kulikuwa na msingi wa kuamini kwamba bwana Murat Kurnaz alikuwa tishio la usalama. Akizungumza kwenye kamati maalum ya bunge la Ujerumani inayochunguza mkasa wa bwana Kurnaz waziri huyo ameeleza kuwa ulikuwa wajibu wake wakati huo kama mkuu wa idara za upelelezi kuhakikisha usalama wa nchi na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara kwa serikali ya Ujerumani wakati huo kumpeleka bwana Kurnaz nchini Uturuki na siyo kumrejesha Ujerumani ,

Hapo awali aliekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani bwana Otto Schily pia aliiambia kamati hiyo ya bunge kuwa bwana Kurnaz alikuwa tishio la usalama.
Mjerumani huyo mwenye asili ya kituruki alikamatwa nchini Pakistan wiki tatu baada ya kutokea mashambulio ya kigaidi nchini Marekani mnamo mwaka 2001. Alikamatwa kwa tuhuma za kuwa gaidi na kupelekwa katika jela ya Marekani ya Guantanamo ambapo alishikiliwa hadi alipoachiwa mwaka jana.Lakini hakufunguliwa mashtaka.

Tuhuma juu ya bwana Kurnaz zilijengeka kufuatia safari yake nchini Pakistan mnamo mwaka 2001. Kuna madai kwamba mjerumani huyo mwenye nasaba ya kituruki alienda nchini Pakistan bila hata ya kuijulisha familia yake ya mjini Bremen. Alienda kupata mafunzo pamoja na wanaitikadi kali wa kiislamu.

Na ABDU MTULLYA