1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulinzi wa NATO wakutana London

Kalyango Siraj18 Septemba 2008

Mazungumzo yanajikita kuhusu changamoto mpya

https://p.dw.com/p/FKUt
Katibu Mkuu wa NATO Jaap de Hoop SchefferPicha: AP

Mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya Umoja wa kujihami wa NATO wanakutaka nchini Uingereza kudurusu matukio mbalimbali yanayoukabili umoja huo.

Hata hivyo mkutano huo unatazamiwa kugubikwa na mgogoro wa Georgia na Urusi na jinsi unavyoweza kuathiri mustakabla wa ushirika wa kijeshi wa umoja huo.

Msemaji wa Umoja wa NATO, James Appathurai,ameviambia vyombo vya habari katika mkesha wa siku ya alhamisi kuwa mazungumzo ya jijini London yatajikita katika athari za sasa za hali ya usalama kwa umoja huo.

Mawaziri hao hapo kesho Ijumaa, watajadilia jinsi ushirika huo wa kijeshi unapaswa kubadilika ili kuweza kwendana na wakati ambapo utaweza kukabiliana vilivyo na changamoto mpya za kiusalama.

Pia watakuwa na mkutano wa faragha na Waziri mkuu wa Georgia Lado Gurgenidze.

Lakini mazungumzo hayo huwenda yakaikasirisha zaidi serikali ya Urusi,ambayo iliuelezea mkutano wa awali wa tume ya pamoja kati ya NATO na Georgia kama unaopinga Urusi na kuendelea kuwa mkutano huo ni alama bayana kuwa uhasama wa enzi za vita baridi unaendelezwa na NATO.

Mkutano wa tume hiyo umefanyika wiki hii.

Mataifa kadhaa wanachama wa umoja huo wa NATO sanasana mataifa ya eneo la Baltic na Poland,yanataka kuona kuwa ushirika huo unakuwa na silaha kalikali muafaka kukabiliana na tisho la ardhini, baada ya Urusi kutuma vifaru vya kijeshi nchini Georgia Agosti nane,ili kuzuia shambulio la Georgia dhidi ya maeneo yanayotaka kujitenga ya Ossetia ya kusini.Sasa utawala wa Moscow umekwenda mbele zaidi na hapo.Umeyatambua rasmi maeneo ya Ossetia ya Kusini pamoja na Abkhazia kama mataifa huru.

Hatua ya Urusi ya kutuma majeshi nchini Georgia na baadae kuyatambua kama mataifa huru majimbo ya Abkhazia na Ossetia ya Kusini, imevuruga uhusiano wake na mataifa ya magharibi.

Mjumbe wa Urusi katika umoja wa NATO amesema kuwa mawaziri wa ulinzi wa NATO watajadilia kurejesha, pamoja na kuimarisha nguvu za jeshi la Georgia ambazo zilivunjwa na shambulio la Urusi.Aidha amesisitiza kuwa Marekani tayari inausaidia utawala wa Tblisi-mji mkuu wa Georgia,kukarabati mifumo ya ulinzi ya Georgia.

Juhudi za Georgia za kujiunga na ushirika wa kijeshi mkubwa kuliko yote duniani, wa NATO, zimeikasirisha Urusi,ambayo inapinga hatua ya mahasimu wake wa wakati wa vita baridi kuweka zana za kijeshi katika nchi jirani.

Msemaji wa NATO, Appathurai,amesema kuwa mazungumzo ya Ijumaa jijini London yatazungumzia zaidi mkakati wa kubadilisha umoja huo,kama vile jinsi ya kupata ndege za Helikopta za kutosha zinazohitajika.