1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulinzi wa Syria, Iran na Urusi wakutana Tehran

Mohamed Dahman9 Juni 2016

Waziri wa Ulinzi wa Syria Alhamisi anafanya mazungumzo mjini Tehran na mawaziri wenzake wa Urusi na Iran wakati vikosi vya serikali vikiongeza mashambulizi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1J3ZO
Picha: picture-alliance/AA/E. Leys

Urusi imepeleka ndege za kivita na vikosi maalum kuusaidia utawala wa Rais Bashar al-Assad wakati Iran imewaweka nchini humo washauri wake wa kijeshi na kuwapatia mafunzo pamoja na silaha wanamgambo wanaoiunga mkono serikali.

Ziara ya Generali Fahd Jassem al Freij inakuja wakati serikali ya Syria ikizidisha mashambulizi yake dhidi ya Kundi la Dola la Kiislamu halikadhalika wapiganaji wa waasi katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Allepo ambapo inadai kwamba wapinganaji hao wana mafungamano na kundi la Al Qaeda.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu anakwenda Tehran baada ya Urusi kuahidi kuongeza mashambulizi yake ya anga dhidi ya wapiganaji wa waasi ndani na karibu na Allepo na kuwashutumu waasi hao ambao sio wapiganaji wa jihadi kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi ya Februari yaliyowataka kuvunja ushirikiano wao na kundi la Nusra Front nchini Syria lenye mafungamano na Al Qaeda.

Mwaliko wa Iran

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran (IRNA) mazungumzo hayo nchini Iran yanafanyika kufuatia mwaliko wa Generali Hossein Dehghan wa Iran.

Wapiganaji wa kujitolea wanaoiunga mkono serikali katika jimbo la Raqqa.
Wapiganaji wa kujitolea wanaoiunga mkono serikali katika jimbo la Raqqa.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Kots

Serikali ya Iran imekuwa ikiipatia serikali ya Syria misaada ya kijeshi na kifedha tokea kuanza uasi dhidi ya utawala wa Assad zaidi ya miaka mitano iliopita.

Wakati huo huo mji wa kaskazini wa Allepo umekuwa chini ya mashambulizi katika kipindi cha saa 48 zilizopita ambapo majeshi ya serikali yamekuwa yakifanya mashambulizi ya anga katika sehemu za mashariki mwa mji huo zinazoshikiliwa na waasi wakati waasi nao wakishambulia kwa mizinga sehemu za magharibi ya mji huo zinazoshikiliwa na serikali.

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria limesema watu kumi wameuwawa wakiwemo watoto katika mashambulizi hayo ya Allepo.

Kujiingiza kijeshi kwa Urusi mwezi Septemba mwaka jana kumeimarisha sana msimamo wa serikali katika vita hivyo.Vikosi vya Urusi vilisaidia vikosi vya serikali kuukombowa mji wa kale wa Palymra hapo mwezi wa Machi na hivi sasa vinasaidia kusonga mbele kuelekea kwenye bwawa kubwa kabisa nchini Syria huko Tabqa katika Bonde la Euphrates.

Kikosi maalum cha Ufaransa

Wizara ya ulinzi ya Ufaransa imesema Alhamisi kwamba imeweka vikosi vyake maalum kaskazini mwa Syria kutowa ushauri kwa kundi la waasi la SDF lenye kupambana na kundi la Dola la Kiislamu.

Wapiganaji wa muungano wa waasi wa SDF unaoungwa mkono na Marekani.
Wapiganaji wa muungano wa waasi wa SDF unaoungwa mkono na Marekani.Picha: picture-alliance/NurPhoto/S. Backhaus

Bila ya kutowa ufafanuzi afisa katika wizara hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba shambulio huko Manbiji ni dhahir kwamba linasaidiwa na nchi kadhaa ikiwemo Ufaransa na kwamba huo ni msaada wa kawaida wa ushauri.

Hadi sasa Ufaransa imekuwa tu ikikiri uwepo wa wanajeshi wake maalum 150 katika eneo hilo ambao wamewekwa huko Kurdistan nchini Iraq.

Kundi la waasi la SDF ambao ni muungano wa wapiganaji wa Kiarabu na Wakurdi linaloungwa mkono na Marekani liko kwenye ukingo wa kaskazini mwa mji wa Manbij mji muhimu kimkakati unaoshikiliwa na kundi la Dola la Kiislamu ulioko kati ya mpaka wa Uturuki na ngome kuu ya wapiganaji hao wa jihadi ya Raqa ambao unatumika kuratibu harakati za mapambano.

Hata hivyo afisa huyo wa wizara ya ulinzi wa Ufaransa amesema kikosi hicho maalum cha Ufaransa hakitotumika kuingilia kijeshi na hakitakiwi kuingia katika mapambano na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/

Mahariri: Yusuf Saumu