1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mayweather amtwanga Pacquiao

3 Mei 2015

Floyd Mayweather amemshinda Manny Pacquiao katika mpambano wa ndodi uliotajwa kuwa wa karne mijini La Vegas Jumamosi (02.05.2015) na kuimarisha nafasi yake miongoni mwa mabondia magwiji duniani.

https://p.dw.com/p/1FJPi
Floyd Mayweather akisheherekea ushindi wa mpambano wake dhidi ya Manny Pacquiao. Las Vegas. (02.05.2015)
Floyd Mayweather akisheherekea ushindi wa mpambano wake dhidi ya Manny Pacquiao. Las Vegas. (02.05.2015)Picha: Getty Images

Sauti za kuzomea zilisikika kutoka kwa mashabiki wa Paquiao waliokuweko kwenye mpambano huo baada ya mabango yote matatu ya kuonyesha matokeo kuthibitisha ushindi wa Mayweather katika mpambano huo wa kusukumiana masumbwi kwa kuviziana.

Mayweather alilidhibiti pambano hilo baada ya raundi nane akikitumia vizuri kimo chake kupanguwa masumbwi ya Mfilipino huyo.Majaji watatu wa mpambano huo walimpa Mayweather ushindi wa pointi 118-110,116-112 na 116-112 dhidi ya Pacquiao.

Ushindi huo umeimarisha rekodi ya ya kutoshindwa ya Mayweather kufikia mapambano 48 bila ya kushindwa kwa kipindi cha miaka 19.

Mayweather bondia wa Marekani mwenye umri wa miaka 38 ametetea mataji yake ya ubingwa wa ndondi uzito wa wastani ya Baraza la Ndondi Duniani na Chama cha Ndondi Duniani na kunyakuwa ukanda wa Pacquiao wa Shirika la Ndondi Duniani kwa kujizolea wingi wa pointi kutoka kwa majaji wote watatu.

Pacquiao mpiganaji mahiri

Mayweather amekaririwa akisema mpinzani wake "alikuwa mpiganaji stadi sana na kwamba imebidi nisiwe na papara na nimuangilie kwa makini."

Manny Pacquiao akimsukumia konde Floyd Mayweather.
Manny Pacquiao akimsukumia konde Floyd Mayweather.Picha: Reuters

Mayweather amesema mapambano yake yote 47 yaliyopita kabla ya kuingia katika pambano hili yalikuwa na dhima kubwa katika maisha yake ya ndondi.Pambano hili inaaminika kuwa ndio lenye faida kubwa katika historia ya ndondi mapato yake yakiwa ni dola milioni mia nne.

Nyota huyo wa Ufilipino Paquiao sasa atakuwa ameshindwa mapambano sita katika historia yake ya ndondi na kushinda 57 na kutoka sare mawili.Ni jambo lilisilokanushika kwamba bondia huyo mwenye umri wa miaka 36 allmpa kibaruwa kigumu Mayweather kuweza kuupata ushindi huo na ngumi za mkono wa shoto mara kadhaa zilimtwanga bingwa huyo wa Kimarekani.

Mpambano ulivyokuwa

Pacquiao alikuwa ndio mchokozi katika pambano hilo na makonde yake ya shoto yaliyokuwa yakituwa kwenye kichwa cha Mayweather yaliweza kumsukuma bondia huyo hadi kwenye kamba za ulingo katika sekunde za mwisho mwisho za raundi za awali.

Heka heka kwenye ulingo.
Heka heka kwenye ulingo.Picha: Reuters

Hata hivyo bondia huyo wa Ufilipino hakuweza kuendeleza machachari yake ya awali hadi raundi zote 12 za mpambano huo na Mayweather ambaye ni mkubwa kiumbo aliweza kupenyeza masumbwi ya kujibu mapigo yaliomfanya Mfilipino ajihami.

Mayweather alivurumisha makonde 435 kulinganisha na 429 ya Pacquiao na asilimia 35 ya makonde yake yalifika mahala pake kulinganisha na asilimia 19 ya Pacquiao.

Maumivu ya bega

Baada ya pambano hilo Pacquiao alisema aliumia bega la kulia wakati wa mazoezi wiki tatu kabla ya pambano na kufikiria hata kuahirisha mpambano huo wa karne.Lakini wiki moja kabla ya pambano alianza kupata nafuu na kuamuwa kuendelea na pambano.

Mashabiki wa Pacquiao wakiliangalia pambano nchini Ufilipino.
Mashabiki wa Pacquiao wakiliangalia pambano nchini Ufilipino.Picha: DW/R.-I. Duerr

Alitaraji angeliweza kuruhusiwa kupiga shindano ya kuzuwiya uvimbe kabla ya pambano hilo lakini Tume ya Riadha ya Jimbo la Nevada ambayo ndio yenye kusimamia ndondi katika jimbo hilo ilimkatalia.

Mwenyewe anasema alidhani kuwa ameshinda mpambano huo kwani anaona kuwa hakuna alichokifanya Mayweather.Nchini Ufilipino baadhi ya mashabiki wake walibwaga vilio na wengine wakitaka kurudiwa kwa mpambano huo kwa hoja kwamba Pacquiao alikuwa ameshinda kwani yeye ndie aliekuwa akimbuburusha Mayweather ulingoni katika raundi zote kumi na mbili.

Mayweather ambaye ameondoka na kitita cha dola zinazokadiriwa kufikia milioni 200 kwa kazi hiyo ya usiku mmoja amesema pambano lake la mwisho litakuwa mwezi wa Septemba na baada ya hapo atajiuzulu masumbwi.Pacquiao atajipatia dola milioni 100 katika mgao wa mapato wa asilimia sitini kwa arobaini waliokubaliana wapiganaji hao kabla ya mpambano huo.

Wakati vitabu vya kihistoria vitakapoandikwa itabainika iwapo kweli mpambano huo ulistahiki kusubiriwa kwa hamu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Amina Mjahid